Mkandarasi, Wizara ya Maji warushiana mpira Serengeti

Wednesday December 5 2018

By Anthony Mayunga, Mwananchi [email protected]

Serengeti. Ukata umemkimbiza mkandarasi wa Kampuni ya Urban and Rular Enginering Services Ltd inayotekeleza mradi wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Kijiji cha Kitunguruma wilayani Serengeti.

Mradi huo unaogharimu Sh1.1 bilioni, unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wakazi 7,500 wa Kijiji cha Kitunguruma na Mbalibali.

Mradi huo utakaokuwa na vituo 15 vya maji na mabirika mawili ya kunyweshea mifugo ulianza kutekelezwa Juni na utakamilika Juni 2019.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali kutoka halmashauri ya Serengeti, hati ya kuthibitisha kukamilika kwa hatua moja ya kazi ili mkandarasi aweze kulipwa sehemu ya fedha zake bado haijatekelezwa na Wizara ya Maji ambayo haijatoa fedha. Kazi zilizokwishafanyika ni pamoja na ufyatuaji matofali, uchimbaji mitaro na ununuzi wa vifaa kama mabomba.

Pia, baadhi ya vibarua waliochimba mitaro, wauzaji wa vifaa vya ujenzi na kazi za ulinzi hawajalipwa kwa muda na hawajui hatima yao baada ya wahusika kuondoka bila kuwaaga.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Juma Hamsini alisema, “kwa mujibu wa mkataba hakuna sehemu inayoonyesha kuwa kutatolewa malipo ya awali kwani taarifa yake ya kifedha alionyesha kuwa yuko vizuri, sijui wamekwama nini kama walichowasilisha kilikuwa na uhalisia.”

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, mwakilishi wa kampuni hiyo Robert Martine alikiri kuwa wanakabiliwa na ukata ndiyo maana wamelazimika kusimama wakisaka fedha ili waweze kuendelea na mradi.

“Tangu tumeanza ukaguzi umefanyika zaidi ya mara mbili na kuandikiwa cheti, Juni tuliomba fedha, lakini hatujapata, mkurugenzi wangu anahangaika ili kupata fedha ili tuweze kuendelea na ukamilishaji, maana vifaa vyote vimeshanunuliwa,” alisema.

Alikiri vibarua wanadai zaidi ya Sh4 milioni,” tunaamini tukipata fedha tutamaliza mradi kwa muda uliopangwa maana sehemu kubwa ya vifaa tunavyo,” alisema.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo alipoulizwa sababu za mradi huo kukwama wakati Serikali ilidai fedha zipo, alisema hana taarifa kuhusu mradi huo. “Kuna wataalamu wetu huko halmashauri wao wanasemaje?” alihoji.

Alipojibiwa kuwa mlipaji ni Wizara ya Maji na wao walishamaliza kazi ya ukaguzi na kutoa hati. “Huyo mkandarasi naye ni changamoto kama hana uwezo wa kifedha, nafuatilia ili nipate majibu sahihi,”alisema.

Advertisement