VIDEO: Mkongo wa Taifa Tanzania kupenya nchi za SADC

Wednesday August 14 2019

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu sekta ya mawasiliano katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika( SADC). Picha na Ericky Boniphace 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Sekta ya Mawasiliano nchini Tanzania imejipanga kuunganisha huduma za mawasiliano katika nchi zote 15 za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC) kwa kutumia huduma ya mkongo wa Mawasiliano wa Taifa.

Mkongo wa mawasiliano ni njia inayowezesha mawasiliano kupita na kusafiri kwa kasi kubwa kwa kutumia mfumo wa mwanga na tabia zake halisi. Mkongo huo una uwezo mkubwa wa kupitisha na kusafirisha mawasiliano data aina zote katika mawasiliano ikiwamo huduma za intaneti na sauti za simu.

Kwa mujibu wa SADC, Sekta ya Mawasiliano ni sehemu ya sekta tano zilizopo katika Idara ya Miundombinu chini ya Sekretarieti ya SADC inayolenga kuanzisha mfumo wezeshi, nafuu, wenye kasi katika huduma za mawasiliano miongoni mwa nchi zote za jumuiya hiyo.

Idara hiyo inatekeleza Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Miundombinu katika mtangamano(RIDMP), utakaofikia ukomo wake 2027 ambapo unatarajia kuimarisha sekta usafirishaji, nishati, Teknolojia ya habari na Mawasiliano(Tehama), vyanzo vya maji na hali ya hewa. 

Akizungumza na wanahabari leo Jumatano Agosti 14, 2019 Jijini Dar es Salaam, kuhusu mkakati katika nchi za Jumuiya hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, amesema tayari Serikali ya Tanzania imeshafikisha huduma za mkongo huo Msumbiji na Zambia.

“Tumekuwa na mikutano ya ukanda Mwanza na tuna mikakati ambayo tumeshaanza kuipanga kuhakikisha nchi zote za SADC zinaunganishwa ili kuwa na mawasiliano rahisi, kwa hiyo tumejipanga kikamilifu na tumekuwa na vikao vya kila mwaka ili kuhakikisha tunafanikisha mpango huo,”  amesema Nditiye.

Advertisement

Aidha Nditiye alisema kutokana na changamoto za udukuzi, Serikali imeanza mchakato wa kuandaa muswada wa kulinda taarifa za mtumiaji wa simu za mkononi (Data Protection Bill) , itakayowasilishwa wakati wowote bungeni baada ya kukamilika mchakato wake.

Hata hivyo Nditiye hakueleza zaidi maudhui ya muswada huo licha ya kudai itakuwa suluhisho la udukuaji wa taarifa za watumiaji wa simu.

“Kwa sasa iko katika mchakato wa kisheria nisingependa kuzungumzia zaidi lakini kimsingi itashughulikia maeneo mengi sana, itakapokuwa tayari tutaeleza wananchi,” amesema Nditiye  wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.

Advertisement