Mkuchika apigilia msumari malipo ya mafao kwa walioghushi vyeti

Muktasari:

  • Hakuna atayelipwa hata kama alibakiza mwaka mmoja kustaafu

Dodoma. Kwa mara nyingine tena, Serikali imeendelea kupigilia msumari kwa watu walioondolewa kwenye utumishi kutokana na vyeti feki kwamba hakuna malipo yoyote watakayolipwa.

Kauli hiyo ilitolewa leo Bungeni wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ambaye amesema hakuna malipo yoyote wanayodai.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Haida Kenani, aliiomba Serikali kufikiria upya ni kwa nini isiwalipe hata watumishi waliobakiza mwaka mmoja kustaafu.

"Tatizo la Serikali mnaangalia vyeti hamuangalii taaluma ya watu na hata wabunge wengine mlifundishwa na hao lakini mnawatosa ni kwa nini,” alihoji Kenani.

Mkuchika alisema katika hali ya kawaida mwajiri alipowaajiri watumishi hao walionyesha kuwa na elimu stahiki na hivyo walipata mishahara kulingana na viwango vyao vya elimu wakati ni kosa.

Alisema sheria haimruhusu mtu kulipwa wakati inajulikana amedanganya.