Mkurugenzi Halmashauri Msalala anusurika ajalini

Mkurugenzi wa msalala Simon Belege kulia akiwa hosptali ya igunga anakotibiwa kulia mkurugenzi wa mji wa kahama Anderson Msumba

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala,  Simon Belege na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mibako Mabubu wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wamepanda kugonga ng’ombe katika mteremko wa mlima Sakenke

Kahama. Mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala,  Simon Berege na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mibako Mabubu wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wamepanda kugonga ng’ombe katika mteremko wa Mlima Sakenke.

Viongozi hao walikuwa wakitokea mkoani Dodoma kuelekea Igunga, Tabora kuwahi kikao cha utekelezaji wa ilani ya CCM kitakachofanyika kesho Jumamosi Septemba 15, 2018.

Akizungumza na MCL Digital leo Ijumaa Septemba 14, 2018 Berege amesema amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga baada ya kupata ajali hiyo, akieleza kuwa ilitokana na kutaka kuwahi kikao hicho.

Amesema wakati wakimaliza kupita eneo la mlima huo, lilitokea kundi la ng’ombe na alijaribu kuwakwepa na kugonga ng’ombe watatu hali iliyosababisha gari kukosa mwelekeo na kugonga gari jingine lililokuwa mbele yao.

Berege amesema katika gari hilo alikuwa pamoja na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, mweka hazina, Masatu Mnyoro na mwanasheria wake, Mashaka Mabula.

“Mnyoro na Mibako hawakuumia sehemu yoyote. Tulikuwa tunawahi kikao ndiyo maana tulikuwa tumebanana wengi kwenye gari moja ili tuweze kuwahi kufika,” amesema Berege.

“Bahati mbaya tukapata ajali hiyo lakini hali zetu sio mbaya sana tunaendela vizuri ingawa gari imekwisha kabisa kule mbele.”

Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Bonaventura Kalumbete amesema  Berege na Mabula ndiyo waliokuwa wamelazwa lakini baada ya kuwapatia matibabu hali zao zinaendelea vizuri na wakati wowote wataruhusiwa.

 “Mkurugenzi alikuwa ameumia kifua na  alikuwa amefunga mkanda lakini tumeangalia hana madhara pamoja na mwanasheria wake (Mabula) aliumia mkono lakini wote hali zao nzuri baada ya kupata matibabu. Wote wataruhusiwa kuondoka wakishafika ndugu zao au jamaa zao,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamlingi Macha amesema wanawasiliana na waliopata ajali na kwamba leo watakwenda Kahama kw aajili ya uchunguzi zaidi wa afya zao.