Mkurugenzi mpya CRDB ataja vipaumbele vitano

Muktasari:

Nsekela aliyechukua mikoba ya Dk Charles Kimei hivi karibuni ametambulishwa rasmi leo kwa umma na kubainisha vipaumbele vyake atakavyoshirikiana na menejimenti kuvitekeleza

Dar es Salaam. Mkurugenzi mtendaji mpya wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amewahakikishia wadau wake kuendeleza ufanisi uliokuwapo huku akibainisha maeneo matano atakayoyapa kipaumbele.

Amebainisha maeneo hayo kuwa ni uboreshaji wa mifumo ya huduma, kuongeza weledi na umahiri wa wafanyakazi, kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa na kukuza biashara katika nyanja zote.

“Lengo ni kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na mahitaji halisi ya wateja na soko. Vilevile, tunataka kuendana na kasi ya mabadiliko ya mahitaji ya wateja,” amesema Nsekela.

Nsekela amesema hayo leo, Oktoba 10 alipokuwa anatambulishwa kwa umma tangu achukue nafasi hiyo nyeti ndani ya benki hiyo mwanzoni mwa mwezi huu.

Sambamba na kuboresha huduma, Nsekela amesema katika kipindi kifupi kijacho CRDB itajikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidigitali ili kuwafikia wateja wengi na kuwapa huduma kila wanapohitaji.

“Tunatumia fursa kwani zaidi ya Watanzania milioni 19.3 wanatumia simu za mkononi kufanya miamala yao kuwashawishi kutumia bidhaa zetu za SimBanking na SimAccount ambazo zinatoa huduma kwa kupitia simu za mkononi pia,” amesema.

Nsekela amemrithi Dk Charles Kimei aliyeiongoza benki hiyo kwa zaidi ya miongo miwili na kuipa mafanikio makubwa akiiwezesha kupata faida kwa miaka kadhaa mfululizo.

Katika kipindi ch auongozi wake, Dk Kimei amefanikisha kuifanya CRDB kuwa benki pekee ya Kitanzania yenye tawi nje ya nchi (Burundi).