VIDEO-Mkuu wa KKKT: hatutakubali kunyamazishwa

Muktasari:

  • Dk Shoo, ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini alitoa kauli hiyo jana katika Usharika wa Masama Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro katika ibada ya Jumapili ya Matawi baada ya mchungaji kiongozi wa usharika huo, Pray Usiri kuusoma waraka huo ambao ulianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu Jumamosi.

Siku moja baada ya Baraza la Maaskofu la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kutoa waraka mzito wa ujumbe wa Sikukuu ya Pasaka, mkuu wa kanisa hilo, Dk Frederick Shoo amesema wasinyamazishwe kwa kuwa jukumu la viongozi wa dini ni kuonya na kusema ukweli.

Dk Shoo, ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini alitoa kauli hiyo jana katika Usharika wa Masama Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro katika ibada ya Jumapili ya Matawi baada ya mchungaji kiongozi wa usharika huo, Pray Usiri kuusoma waraka huo ambao ulianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu Jumamosi.

“Sisi viongozi wa dini hatutanyamaza na hatutawaachia. Wajibu wetu tunaonya, tunashauri, tunakemea na tunasema. Asijaribu mtu kutuzuia kufanya hivyo,” alisema Dk Shoo katika ibada hiyo jana.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, KKKT ilitoa waraka ambao mbali na kuzungumzia masuala ya kiroho, umetaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini wake “ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.”

Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la “Taifa Letu Amani Yetu” na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

Alichosema Askofu Shoo jana

Akifafanua msingi wa kutolewa waraka huo, Dk Shoo alisema wameutoa baada ya kufunga na kuomba ili Mungu awawezeshe kutoka na ujumbe mahsusi kwa waumini wa kanisa hilo, huku akiwakemea wanaouhusisha na siasa.

Alianza kwa kuwapongeza maaskofu waliochangia kuutoa waraka huo aliouita kuwa ni wa kinabii na kuwataka kuendelea na ujasiri huo.

Dk Shoo alisema walipofunga waliomba wapewe ujumbe utakaosaidia Taifa na wakaona hawawezi kukaa kimya hata kama utakuwa ujumbe mzito.

Alisema walikubaliana waufikishe kwa waumini wao na nchi kwa ujumla, huku akiufananisha na uliotolewa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

“Tuupokee ujumbe huu siyo kwa kukurupuka, tuupokee, tuusikilize, kuutafakari na tuombe sana ili Mungu atupe macho ya kiroho, tufahamu Mungu anataka kutuambia nini kwa ajili ya nchi yetu,” alisema Dk Shoo na kuongeza:

“Tuweke itikadi ya vyama na kisiasa pembeni, tumuulize Mungu unataka kutwambia nini kwa ajili ya nchi yetu ya Tanzania. Tunawasihi kwa machozi, tumeandika pale, tunawasihi kwa machozi Watanzania, yapo mambo Mungu anayaona, anayaangalia, anaona haya ni mema yatendeni hayo.”

Alisema yako mambo Mungu anayaona kuwa ni maovu na kama Tanzania inayaona hakika mwisho wake hautakuwa mwema.

“Mungu anasema hayo mema yanayotendeka yatafanyika hayo yatendeni, yale maovu yaacheni,” alisema Dk Shoo na kuongeza:

“Yako mambo ambayo tumeyataja katika waraka huo, Mungu atujalie tuyatafakari na kuyatenda kwa ajili ya Taifa letu, yale ya kukataa na kukemea tuyaache kwa ajili ya kulipenda Taifa letu.”

Dk Shoo alisema wao kama viongozi wa kiroho wamefanya hivyo kwa kumheshimu Mungu, kwa kutambua nafasi yao na utume waliopewa.

“Wengine mnaweza kudhani (waraka) ni wa chama fulani au itikadi fulani, hapana! Tumefanya kwa wajibu wetu, hatujafanya na hatutafanya kutoa ujumbe eti kwa sababu ya upande fulani wa chama.

“Isitokee kikundi cha watu kinachoweza kufikiri kitaziba sauti ya Mungu, hatuwezi kunyamaza neno la Mungu halituruhusu kufanya hivyo na ninaomba wajue kutofautisha sauti ya nabii wa Mungu na propaganda za kisiasa zinazoweza kupingwa na wengi.

“Tutofautishe ushabiki pamoja na kauli mbiu za kisiasa au za wanasiasa na matamko ambayo misingi yake ni upendo wa dhati kwa nchi hii, ni uzalendo wa dhati kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema.

Alifafanua kuwa anaogopa watu wanapokaa na kuanza kuwa na hofu ya maisha na uhai wao, jambo alilosema ni hatari hivyo lazima waseme hapana.

“Mungu wetu ni Mungu wa uhai si wa kifo, si wa mauti,” alisema Dk Shoo na kuwaomba wautafakari waraka huo ili kuona wapi Mungu anataka wabadilike ili iwe Tanzania ya amani.

Alisema wapo watakaoupokea waraka huo kwa fikra mbalimbali, hivyo akawataka watakaofanya hivyo kuweka pembeni fikra zao na kuangalia nia njema.

“Sisi Walutheri si wasikilizaji, ni watendaji na huu uwe ni mchango wetu kwa ajili ya nchi yetu,” alisema.

Akitoa wito kwa wanasiasa, Askofu Shoo alisema: “Nawasihi wanasiasa na vyama vyao, msije kutugawanya gawanya nchi yetu katika vipande vipande, Tanzania ni nchi yetu sote, msije kuigawanya hii nchi na kuipeleka mahali kubaya.”

Askofu mstaafu azungumza

Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Martin Shao alisema: “Ninafahamu kwamba kwa kutoa huu waraka maaskofu hawa 27 wanaweza kupigwa vita, lakini wasimame hata kama kwa msimamo huo itawagharimu.”

Huku akiwapongeza kwa kutoa waraka huo, Askofu Shao alisema ameusikiliza waraka huo kwa makini na kubaini umetolewa wakati mwafaka.

“Nikiwa askofu mstaafu nimekutana na watu kabla ya tamko hili, wananiuliza askofu unasemaje kuhusiana na hali ya maisha ya Watanzania kwa sasa?

“KKKT haikurupuki tu kusema, huwa inatafakari sana kabla ya kutoa tamko, huu ni ujumbe wa Mungu kwetu sisi na Watanzania wote. Ujumbe wenu umefika kwa Wakristo wengi na Watanzania. Tutatenda kulingana na hayo mliyoyasema,” alisema Shao ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini waliohudhuria ibada hiyo.

Viongozi wengine wa dini waliokuwapo ni msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Elingaya Saria, katibu mkuu wa dayosisi hiyo, Arthur Shoo na wachungaji kutoka sharika za jirani.

Ibada ya Matawi

Ibada hiyo ya Jumapili ya Matawi ambayo hufanyika wiki moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka, ilihudhuriwa na viongozi katika makanisa mbalimbali nchini.

Rais John Magufuli aliungana na waumini wengine katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam. Rais Magufuli alikuwa na mkewe Janeth na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa

Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walihudhuria ibada hiyo katika Kanisa la Azania Front.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Hai), Ibrahim Yamola, Pamela Chilongola na Fortune Francis (Dar)