Mradi wa kukusanya takwimu za samaki Bahari ya Hindi waanza

Monday September 16 2019

Mkurugenzi mtendaji wa wakala wa elimu na

Mkurugenzi mtendaji wa wakala wa elimu na mafunzo ya Ufundi (FETA) Ally Yahaya Mgawe akizungumza wakati wa ufunguzi wa mi tano wa tasmini ya wadau wa samaki na uvuvi kwa nchi zilixopo ukanda wa kusini wa Afrika mashariki  mkutano huo umefanyika Dar es Salaam. Picha na Said khamis 

By Muyonga Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaaam. Nchi tatu za ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi Tanzania, Kenya na Msumbiji zimeanzisha Mradi wa Ukusanyaji Takwimu za Samaki kwa Ukanda wa Afrika Mashariki (Fidea) ili kuwa na taarifa za pamoja zitakazosaidia kulinda na kujua hali ya viumbe hao.

Katika kikao cha pamoja cha kujadili mradi huo, wadau kutoka nchi wanachama wameshiriki kutoa maoni yao kuhusu mradi huo unaofadhiliwa na nchi ya Ujerumani.

Mtendaji mkuu Wakala wa Elimu wa Mafunzo ya Uvuvi, Yahya Mgawe amesema takwimu hizo zitakusanywa kwa njia ya kiteknolojia katika timu ya wasimamizi wa nchi zote tatu.

Amesema takwimu zitachakatwa na kupata habari zitakazosaidia kufanya uvuvi endelevu.

"Tulikuwa na ukusanyaji wa takwimu uliozoeleka ila sasa kumetokea mapinduzi makubwa ya kutoa taarifa kiteknolojia, takwimu sio zikusanywe na wanasayansi peke yao bali pia hata wadau kama wavuvi na wote wanaofanya shughuli zinazohusu rasilimali ya uvuvi," amesema Mgawe.

Ameeleza madhara ya kutokuwa na takwimu za samaki  ni kuisha kwa rasilimali hizo huku akitolea mfano wa Canada Mashariki kuwa wamezuia shughuli za uvuvi kwa miaka 30 kwa uvuvi uliopitiliza bila ya kuwa na kumbukumbu.

Advertisement

Mgawe ameeleza kuwa Tanzania bado tupo katika hali nzuri ya uvuvi kutokana na usimamizi na ukusanyaji wa takwimu uliokuwapo.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), Dk Semvua Mzighani amesema hatua mbalimbali zinachukuliwa baada ya ukusanyaji wa taarifa.

Amesema kwa hapa nchini mwaka 2007 walifungia uvuvi wa kamba (prawns) hadi  2016 baada ya Tafiri kujiridhisha.

"Jana Septemba 15 watafiti wameenda Ziwa Victoria kufanya utafiti kwenye samaki waliopo. Baada ya Operesheni Sangara hali ya samaki hao imeimarika kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka jana, " amesema Mzighani.

"Ili kupunguza nguvu ya uvuaji wa samaki tumeanza kufundisha watu na kuhamasisha kufuga nje ya yale maji ya asili," amesema Mzighani.

Msimamizi wa Fidea, Dk Rushingisha George amesema wananchi wa kawaida watanufaika na mradi huo kwa kujua taarifa sahihi za hali halisi ya samaki na hatua zitakazochukuliwa baada ya wao kuwasilisha tafiti zao.

Advertisement