Msaada wa Kuwait kuokoa maisha ya watoto 1,0

Wednesday May 16 2018

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Meneja wa Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Almas Jumaa  baada ya kuwasili jana katika halfa ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa taasisi hiyo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile. Picha na Herieth Makwetta 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Idadi ya watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi watakaofanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi), inatarajiwa kufikia 1,000 kwa mwezi.

Kwa sasa idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji huo ni kati ya 500 hadi 700 kwa mwezi.

Hayo yalisemwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan baada ya ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania kuipatia Moi msaada wa vifaa vya upasuaji vyenye thamani ya Sh258 milioni.

Vifaa hivyo vitafungwa katika chumba maalumu kwa ajili ya upasuaji wa watoto wenye tatizo hilo pekee. Awali, upasuaji ulikuwa ukifanyika katika vyumba vya upasuaji vya kawaida.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Samia alisema, “kuwa na vifaa ni hatua moja na kuvitunza ni hatua nyingine, natumaini mtavitunza vyema.”

Makamu wa Rais aliiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha inatoa ushirikiano kwa Kuwait ili kuomba vifaa tiba.

“Mazungumzo yangu (na balozi wa Kuwait) hivi karibuni nilimuomba vifaa vya akina mama vya kujifungulia akaniahidi kwamba ataleta, lakini anachoomba ni barua rasmi kutoka wizarani ili naye awasilishe Kuwait yawe ni maombi rasmi na vifaa viweze kupatikana,” alisema Makamu wa Rais.

“Si vibaya pia tunapopokea vifaa kama hivi vya leo kuwapelekea barua za shukrani zikiambatana na picha tunazopokea ili naye aweze kupeleka kwao kuonyesha kwamba vimepokewa na mtu wa pili serikalini ndiye aliyepokea vifaa hivi, hii inasaidia kuonyesha imani kule kwamba kweli tunathamini na wao kupata imani ya kuleta zaidi.”

Naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile aliwaagiza watumishi waliopo chini yake kuwasilisha barua hiyo kwa ubalozi ndani ya wiki mbili kuanzia jana. “Msaada huu umekuja wakati ambao Serikali tunaboresha sekta ya afya hasa huduma za upasuaji,” alisema.

Naibu waziri huyo alisema Serikali imetoa Sh16.5 bilioni kwa Moi ili kukamilisha ununuzi wa vifaa tiba vitakavyofungwa katika jengo jipya.

“Vitakapokamilika kufungwa, Moi itakuwa na vyumba vinane vya upasuaji kutoka sita vilivyopo sasa na kimoja kitakuwa maalumu kwa ajili ya watoto,” alisema.

Balozi wa Kuwait nchini, Jassem Al Najem aliyemkabidhi vifaa hivyo Makamu wa Rais alisema, “msaada huu ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Kuwait uliotengewa Dola 500,000 za Marekani (zaidi ya Sh1.3 bilioni)kusaidia nchi zenye uhitaji.”

Balozi huyo pia alikabidhi msaada wa miguu bandia kwa watoto wawili akiahidi kuwa yuko tayari kutoa msaada huo kwa wahitaji.

Pia, aliomba ushirikiano wa karibu kutoka Wizara ya Afya ili azidi kuwasaidia Watanzania ikiwa ni pamoja na kupatiwa barua ya maombi ya msaada.

Advertisement