Mtoto aliyekuwa na uvimbe afariki dunia, waziri azungumza

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa ORCI, Julius Mwaiselage alisema mgonjwa huyo alifariki dunia jana alfajiri wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Maria Amrima (17) mkazi wa Mtwara, aliyekuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kutokana na uvimbe mkubwa begani, amefariki dunia.

Mkurugenzi wa ORCI, Julius Mwaiselage alisema mgonjwa huyo alifariki dunia jana alfajiri wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Maria ambaye alitakiwa kufanyiwa upasuaji Muhimbili mwaka mmoja uliopita wakati uvimbe huo ukiwa mdogo, alitoweka na kwenda katika tiba za asili kabla ya kurejea hospitalini hapo Januari 3 akiwa katika hali mbaya na kuhamishwa ORCI.

Kuhusu kifo hicho, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema mwili wa marehemu ulisafirishwa jana mchana kwenda mkoani Mtwara kwa maziko.

“Inasikitisha kwani wamejitokeza dakika ya mwisho, msaada wetu haukuweza kuokoa maisha yake, tutaongeza jitihada zaidi kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwahi hospitalini kufanyiwa uchunguzi,” alisema.

Waziri huyo ambaye alimtembelea Mariam wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alisema, “Wananchi wanapaswa kufuata maelekezo ya madaktari ikiwamo kuanza matibabu mara moja na si kwenda kukaa nyumbani na mgonjwa.”

Awali, jopo la madaktari bingwa kutoka vitengo vitatu vya Muhimbili na Ocean Road, walikutana kujadili namna ya kumtibu mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka 17 baada ya tiba ya upasuaji kushindikana.