VIDEO: Mwanakwaya alivyowaaga wazazi, jirani kabla ya kuuawa

Haikuwa rahisi kuvumilia wingu zito la simanzi lililokuwa limeugubika msiba wa mwimbaji wa Kwaya ya Vijana ya Kanisa la AICT-Chang’ombe (CVC) jijini Dar es Salaam, Mariam Lutonja.

 

BY Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.com

IN SUMMARY

  • Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa baadhi ya wanakwaya hasa waliposhindwa kuimba, kuaga mwili wa mwenzao baada ya kuishiwa nguvu na kuzimia

Advertisement

Haikuwa rahisi kuvumilia wingu zito la simanzi lililokuwa limeugubika msiba wa mwimbaji wa Kwaya ya Vijana ya Kanisa la AICT-Chang’ombe (CVC) jijini Dar es Salaam, Mariam Lutonja.

Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa baadhi ya wanakwaya hasa waliposhindwa kuimba, kuaga mwili wa mwenzao baada ya kuishiwa nguvu na kuzimia.

Wakati ibada ikiendelea, viongozi wa kanisa walilazimika kutoa huduma ya kwanza kila waombolezaji wanapoishiwa nguvu.

Mariam alifariki Septemba 4, mwaka huu, akidaiwa kunyongwa na mchumba wake Frank Magulu, siku chache kabla hajamlipia mahari.

Mwili wake ulikutwa katika nyumba ya kulala wageni ya East London, iliyoko eneo la Buza, wilayani Temeke.

“Sielewi nia ya huyu kijana kuingia nyumbani kwangu! Alimtafuta Mariam ili amfanyie ubaya? Ningemuuliza Mariam kabla hajalala kulikuwa na ugomvi angeniambia! Lakini hata katika yote namshukuru Mungu,” anasema baba wa Mariam, Charles Lutonja.

Kila mmoja aliongea lake baada ya taarifa za binti huyo kuuawa kuanza kusambaa kwenye mitandao.

Hata hivyo, baada ya kujua ukweli kuhusu mahusiano ya wazi ya uchumba wa wawili hao ambao wote walikuwa wanakwaya, simanzi miongoni mwa wengi iliongezeka.

Lutonja anasema baada ya kupewa taarifa kuwa mwanawe angelipiwa mahari Ijumaa, aliona ni jambo jema hakujua kama mwanawe angeuawa.

Msichana huyo,, Mariam alikuwa akijishughulisha na biashara ndogo ndogo ikiwemo kuuza dagaa huku akiutumia muda wake kuhudumu kama mwanakwaya wa CVC.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Lukula, anasema walimkamata mtuhumiwa huyo, wakati akijiandaa kuingia kwenye nyumba ya kulala wageni ya Kisuma, iliyoko katika Mtaa wa Sokota.

Alivyolipiwa posa

Baba wa Mariam, Charles Lutonja anasema alimuamini mkwewe, Frank na kukubali kupokea posa bila kujua siku moja atasababisha msiba kwenye familia yake.

“Nilimwamini, alikuja kwangu kupitia uongozi wa kanisa, hivyo sikuwa na neno nilipokea ujumbe wa binti yangu kuposwa,” anasema na kuongeza;

“Nilimkabidhi jukumu hilo mjomba wake, kwa sababu nilikuwa safarini, posa ilipopokelewa mjomba aliniambia ni kijana mzuri na muonekano wake hauna tatizo.”

Anaeleza kuwa aliendelea kumwamini mkwewe hadi alipopata taarifa kwamba amehamia mkoani Dodoma ambako alielezwa kuwa amepata kazi.

“Kwa hiyo akiwa huko sikufahamu hadi siku ya Jumanne nilipoambiwa kuwa amemuandikia ujumbe mama yake Mariam kuwa Ijumaa angeleta mahari,” anasema.

Anasema alishtuka kupata ujumbe huo wa ghafla kwa sababu hawakuwa wamejiandaa kupokea jambo hilo.

Hata hivyo, anasema ilibidi wakubali kupokea, hasa walipobaini kuwa mkwe wao amehamia mkoani Dodoma kikazi, hivyo itampasa akamilishe masuala yake mapema.

“Kiukweli sikuelewa huyu kijana alikuwa na nia gani kuingia nyumbani kwangu, sikujua kwa nini alimtafuta Mariam ili amfanyie ubaya. Kwa yote namshukuru Mungu,” anasema.

Anasema kama angekuwa na nafasi ya kumuuliza binti yake kabla ya mauti labda angeeleza kama kulikuwa na ugomvi miongoni mwao.

“Labda Mariam angeniambia kulikuwa na hiki na kile, lakini mwanangu alipoitwa alienda maana ni mchumba wake,” anasisitiza.

Siku moja kabla ya tukio

Rafiki wa karibu wa Mariam, Jesca Julius anasema siku moja kabla Mariam hajauawa, mchumba wake (Frank) alimtafuta baada ya kumkosa kwenye simu.

“Aliponiuliza Mariam nilimwambia yuko kwao. Nikamtaarifu Mariam kwamba anatafutwa, hivyo tukakaa kidogo, akapiga simu kumbe alikuwa ameshakuja,” anasema.

Anasimulia kuwa, Mariam alitoka kwenda kumpokea mchumba wake wakaja hadi kwake kumsalimia.

“Kwa hiyo alikuja naye hadi hapa, nikamuuliza shem mbona ghafla au ni ‘surprise’? Akajibu ndiyo hivyo, baada ya salamu hatukuongea sana nikawaacha,” anasema.

Jesca anasema hakujua kama shemeji yake alikuwa akipanga njama za kumuangamiza rafiki yake Mariam, tukio ambalo kamwe hatalisahau.

Siku ya tukio

Jirani yao, Rachel Ephrahim anasema, siku ya tukio Mariam alimpelekea dagaa ili amuungishe akiwanadi kuwa mali mpya.

“Alikuja akaniambia ni dagaa watamu sana, nilionja nikaona hivyo. Basi tukaongea hapa na pale nakumbuka wakati huo ilikuwa kama saa kumi jioni,” anasema.

Anasema baadaye waliagana na Mariam aliondoka japo hakujua kwa wakati huo alikuwa anaelekea wapi.

Simulizi ya mama

Mama yake mzazi Mariam, Easter Lutambi anasema mwanawe aliaga anaelekea kanisani kabla ya kumtumia ujumbe wa simu kwamba, ataenda kwa mchumba wake kwa kuwa amemuita.

“Aliniambia mama nitachelewa kurudi, basi sikuwa na neno, lakini usiku ule wa Jumanne hakurudi, ilipofika Jumatano asubuhi nilipokea ujumbe kuwa tayari amemuua mwanangu,”anasema mama huyo.

Anasema baada ya hapo walianza kumtafuta Mariam bila mafanikio.

“Tulipokwenda kituoni tukaambiwa kuna mwili umekutwa gesti tulipoukagua tukagundua ni Mariam,” anasema.

Ujumbe wa vitisho

Dada wa Mariam, Lucy Enock anasema naye ni miongoni mwa watu waliotumiwa ujumbe wa vitisho baada ya kifo cha mdogo wake.

“Alinitumia ujumbe huu ‘Nimemuua Mariam kwa ajili ya uongo wake kwangu, alinitengenezea njama kwa mama (anataja jina) ili nikamatwe, nikamgundua baada ya mama huyo kumpigia akiwa anaoga’” anasema.

Ujumbe mwingine uliotumwa kwa ndugu wa Mariam, Paul Makelele unasema ‘mtindo wako wa kushindwa kutunza siri nina silaha, au nikufuate? Ni meseji nyingi napokea,” anasema.

Mwili waagwa

Vilio, huzuni na maombolezo ndivyo vilivyokuwa vimetawala siku ya kuagwa kwa mwili wa mwanakwaya huyo.

Wanakwaya wenzake ndio waliokuwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Mariam tangu ulipowasili kanisani kwa ajili ya ibada.

“Ni ngumu kueleza lakini tunamuachia Mungu, tunapitia huzuni kubwa kuondokewa na mwenzetu, lakini hatuna budi kumshukuru Mungu kwa jaribu hili,” anasema katibu wa kwaya ya CVC, Dickson Seni.

Anasema wataendelea kumuenzi mwenzao pamoja na wazazi wake kwa kuwa wanaamini hata katika hilo, Mungu hajawaacha.

Polisi wamkamata mtuhumiwa

Wakati ibada ikiendelea, Mchungaji Kiongozi wa AICT-Chang’ombe Elisha Isabula aliwapooza waombelezaji baada ya kutoa taarifa za kukamatwa kwa mtuhumiwa wa mauaji hayo.

“Wakati tunaendelea na ibada walikuja polisi, mtuhumiwa alikuwa maeneo haya ameshakamatwa,” alitangaza mchungaji huyo.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Lukula anasema mtuhumiwa huyo ni mtaalamu wa maabara na mkazi wa Mtaa wa Kilakala, Temeke.

“Mtuhumiwa amekamatwa na daftari aliloandika kujutia kumuua Mariam kwa wivu wa mapenzi,” anasema Kamanda.

Simulizi kabla ya kukamatwa

Meneja wa nyumba ya kulala wageni ya Kisuma, alikokamatwa mtuhumiwa huyo, Damian Urio anasema Frank alifika siku moja kabla ya kukamatwa.

Anasema baada ya kufika kwenye gesti hiyo, mhudumu alimpangia chumba namba 230 alimolala hadi Jumamosi, siku ya mazishi ya mchumba wake.

“Alipofika aliingia ndani hakukaa sana akatoka, baadaye kidogo alirejea na kulala hadi asubuhi,” anasema.

Anasema asubuhi ilipofika, kijana huyo alichelewa kuamka hadi alipogongewa mlango, kuwa ni muda wa usafi.

“Basi aliondoka akaenda kunywa chai, ilikuwa kama saa tano hivi asubuhi. Alirudi na akaingia tena chumbani,” anasema.

Alivyojiunga kwaya

Baadhi ya wanakwaya ambao hawakutaka kuandikwa majina yao gazetini, wanasema Frank alijiunga na kwaya hiyo mwaka mmoja uliopita akitokea mkoani Shinyanga.

Wanasema wakati anafika hakuwa na kazi, lakini baadae aliajiriwa kama mtaalamu wa maabara kwenye maabara moja.

“Kwa hiyo alisaidiwa kupata hiyo kazi lakini baadae ikaja taarifa ikidai ameiba. Aliondoka na aliporejea ndipo alipofanya hili tukio, inaumiza sana,” anasema mmoja wa wanakwaya.

Viongozi wa kanisa

Askofu wa AICT, Dayosisi ya Pwani, Charles Salala anasema yanapotokea matukio magumu na yanayoumiza ni wakati ambao watu wa Mungu wanapaswa kuomba.

Anasema kifo cha Mariam kisiligawe kanisa hilo lakini iwe njia ya kumtafakari Mungu.

“Nitoe pole kwa wazazi, ndugu jamaa, marafiki na wanakwaya wenzake. Hili lituache mikononi mwa Mungu,” anasema Askofu Salala.

Mariam alikuwaje

Mama yake Mariam, Ester anasema binti yake huyo wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto sita, wakike wakiwa wanne alikuwa mpole, mtiifu na mcheshi.

“Mara zote aliniaga kila alikokuwa anakwenda, nimeumia sana,” anasema.

Baadhi ya majirani wanasema, Mariam alikuwa rafiki wa wote na hakubagua.

“Kusema kweli huyu kijana amemwaga damu isiyo na hatia, huyu binti sijawahi kusikia hata kama alikuwa na tabia yoyote mbaya. Namfahamu tangu mdogo hadi anakua,” anasema Mwenyekiti wa madereva katika mtaa aliokuwa akiishi Mariam, Paul Peter.

Rafiki yake, Rachel Ephrahim anasema kifo hicho kimeacha pengo kubwa.

“Mariam alikuwa rafiki yangu, mara nyingi nilikuwa naye. Kuondoka kwake ni pigo kubwa kwangu,” anasema.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept