Mwenyekiti wa CCM Dar kizimbani kwa tuhuma za kusambaza ARV feki
Muktasari:
Alidai kuwa washtakiwa hao waliweka viambatanisho hivyo wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halisi na kwamba zilitengenezwa Machi 2011 na muda wake wa kutumika ulikwisha Februari 2013 huku wakijua kwamba ni uongo.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI), Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa Operesheni wa TPI, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msofe, Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD), Sadick Materu na Evans Mwemezi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nyigulile Mwaseba, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika shtaka la kwanza, Aprili 5, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango wakiwa na nyadhifa hizo kwenye kiwanda cha TPI walisambaza makopo 7,776 ya dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) aina ya Antirectroviral.
Kimaro alidai kuwa washtakiwa hao, walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 76 (1)(2) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halali na kwamba zimetengenezwa Machi, 2011 na muda wake wa kutumika unakwisha 2013 wakati wakijua kuwa si kweli.
Katika shtaka la pili, Wakili Kimaro alidai kuwa Aprili 11, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango walisambaza na kuuza makopo 4,476 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral walizokuwa wakijaribu kuonyesha kuwa zilikuwa na viambatanisho vya Starudine 30mg, Nevirapine 200mg, Lamivudine 150mg pamoja na fungu namba OC 01.85.
Alidai kuwa washtakiwa hao waliweka viambatanisho hivyo wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halisi na kwamba zilitengenezwa Machi 2011 na muda wake wa kutumika ulikwisha Februari 2013 huku wakijua kwamba ni uongo.
Katika shtaka la tatu wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na Kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili Kimaro alidai kuwa kati ya Aprili 12 na 29, 2011, washtakiwa hao wakiwa na nia ya kulaghai, walijipatia Dola za Marekani 98,506 sawa na Sh148,350,156.48 wakijaribu kuonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni malipo halali ya makopo 12,252 ya dawa aina ya Antirectrovial yaliyokuwa katika fungu (batch) namba OC 1.85.
Alidai pia kuwa washtakiwa hao walikuwa wakionyesha dawa hizo bandia zilikuwa zimetengenezwa Machi, 2011 na kwamba muda wake wa kumalizika kutumika ni Februari, 2013 na wakafanikiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka MSD.
Katika shtaka la nne, Materu na Mwemezi wakiwa ni Meneja wa Udhibiti Viwango na Ofisa Udhibiti Viwango wa MSD, kati ya Aprili 2 na 13, 2011 huku wakijua nia ya kutendeka kwa makosa hayo ya usambazwaji wa dawa bandia, walishindwa kuzuia kinyume na Kifungu cha Sheria namba 383 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika shtaka la tano, wakili huyo wa Serikali alidai kuwa kati ya Aprili 5 na 30, 2011, washtakiwa Madabida, Shamte, Msofe, Shango pamoja na Materu na Mwemezi, kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi, walishindwa kutekeleza majukumu yao wakiwa watendaji.
Alidai kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kusambaza makopo 12,252 ya dawa bandia wakijaribu kuonyesha kuwa zilitengenezwa Machi 2011 na kwamba zitakwisha muda wake wa kutumika Februari 2013 na kuisababishia mamlaka hiyo ya Serikali hasara ya Sh148,350,156.48.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mwaseba alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao wanafanya kazi kwenye taasisi zinazotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini angesaini bondi ya Sh6,181, 256.
Pia alimtaka kila mshtakiwa kutoa kiasi cha Sh12, 362,513 milioni taslimu mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Madabida na Materu waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo huku wenzao wakipelekwa mahabusu kusubiri kuyakamilisha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, mwaka huu itakapotajwa.