NEC yawaahidi wapinzani makubwa

Muktasari:

  • Uchaguzi mdogo unaohusisha ubunge Jimbo la Buyungu wilayani Kakonko unatarajiwa kufanyika sambamba na ule wa kata 79, Agosti 12.

Dar/Tanga. Wakati Kamati Kuu ya CCM ikimpitisha Christopher Chiza kugombea ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema itahakikisha inaondoa kasoro zilizojitokeza katika chaguzi za marudio zilizopita.

Uchaguzi mdogo unaohusisha ubunge Jimbo la Buyungu wilayani Kakonko unatarajiwa kufanyika sambamba na ule wa kata 79, Agosti 12.

Jimbo la Buyungu liko wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Kasuku Bilago (Chadema) aliyefariki dunia Mei 26. Pia uchaguzi huo utahusisha udiwani kwenye kata hizo zilizopo katika Halmashauri 43 kwenye mikoa 24 ya Tanzania Bara.

Akizungumza wakati akitangaza uchaguzi huo unaotarajiwa kugharimu kiasi cha Sh3 bilioni, mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema jana kuwa changamoto kubwa ni utambulisho wa mawakala.

Changamoto hiyo ni miongoni mwa zilizolalamikiwa na wapinzani katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha pamoja na kata nane, uliofanyika Februari 17.

Malalamiko mengine ya kambi hiyo yalihusu mawakala wao kuzuiwa kuingia katika vyumba vya kupigia kura, chama tawala kuwatumia viongozi wa Serikali katika kampeni, viongozi hao kutumia magari ya umma katika mikutano ya kampeni, vitisho na wagombea wa upinzani kunyimwa fursa ya kushuhudia upigaji kura vituoni.

Hata hivyo, Jaji Kaijage alisema jana kuwa wajibu wa utambulisho wa mawakala katika vituo vya kupigia kura siyo wa vyama vya siasa, bali ni wa msimamizi wa uchaguzi katika jimbo husika au wasaidizi wao.

“Hatutarajii vyama vya siasa kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi katika vituo, changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kwa kiwango kikubwa zimetokana na kutozingatia taratibu, kanuni na sheria zinazoongoza utambulisho wa mawakala wa vyama vya siasa,” alisema mwenyekiti huyo wakati akizungumzia uchaguzi huo.

“Wajibu wa kuwatambulisha mawakala upo kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, si wajibu wa chama cha siasa kumtambulisha wakala wake kwa msimamizi wa kituo cha kupiga kura.”

Alisema matatizo hayo hujitokeza kwa sababu ya watu kutosoma vizuri sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi.

“Ndiyo maana leo tumesisitiza vyama vyote vya siasa vifuate taratibu zilizowekwa kwa ufasaha.”

Mwenyekiti huyo alisema maandalizi yanaendelea, huku akisisitiza kuwa baadhi ya vifaa vinavyohitajika katika hatua zote za uchaguzi vimeshaandaliwa, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi katika ngazi za jimbo na kata wameshapewa mafunzo.

Hata hivyo alivikumbusha vyama vya siasa kuzingatia maadili ya uchaguzi ambayo yapo kwa mujibu wa sheria.

Hofu ya ADC, ACT

Awali katibu mkuu wa Chama cha ADC, Doyo Hassan alisema hawategemei mapya yatakayotokea katika uchaguzi huo, kwani purukushani na kupelekana polisi huenda vikatokea iwapo NEC haitafanya marekebisho yoyote.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema hawana matumaini makubwa na wasimamizi kwa sababu kwa miaka mingi vyama vya siasa vimekuwa vikilalamikia uchaguzi kutokuwa huru na haki.

CUF wavuana uanachama

Wakati NEC ikijiandaa na uchaguzi huo, madiwani watatu wa CUF katika Jiji la Tanga wamevuliwa uanachama.

Waliovuliwa uanachama na kupoteza sifa ya kuwa madiwani ni Rashid Jumbe wa Kata ya Mwanzange pamoja na madiwani wa viti maalumu, Fatma Hamza na Halima Mbwana. Fatma pia alikuwa mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Tanga.

Akizungumzia hatua hiyo, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Daud Mayeji alisema amepokea nakala za barua tatu zilizoandikwa na kusainiwa na kaimu katibu wa CUF, Magdalena Sakaya kwenda kwa madiwani hao kuwafahamisha juu ya suala hilo.

“Kwa hatua hiyo ni kwamba Halmashauri ya Jiji la Tanga ina nafasi tano za madiwani zilizo wazi, hawa waliovuliwa uanachama na waliojiondoa wiki iliyopita ambao ni Omari Mzee wa Makorora na Jumaa Ramadhani wa Kata ya Mabokweni,” alisema Mayeji.

Mkurugenzi huyo alisema jukumu lililobaki kwa sasa ni meya wa Jiji la Tanga kumjulisha waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) kushughulikia mchakato wa kutangaza uchaguzi mdogo katika kata hizo na kuziba nafasi za madiwani wa viti maalumu.

Wakati Mayeji akitangaza hayo, Jumbe aliitisha mkutano wa wanahabari na kusema hatambui kuvuliwa uanachama kwa sababu Sakaya si mwanachama halali wa CUF.

“Kwanza bado sijapokea barua yoyote na hata ikiletwa kama aliyeandika na kutia saini ni Sakaya itakuwa ni batili, kwa sababu tulishamvua uanachama na hii inajulikana pia kwenye chama chetu hakuna wadhifa wa kaimu katibu mkuu, hivyo ameandika kwa kutekeleza kazi ya kukivuruga CUF,” alisema Jumbe.

Alisema yeye na wenzake wawili watakwenda mahakamani kupinga adhabu hiyo kwa sababu njia zilizotumika ni batili kisheria.

“Tutakwenda mahakamani kupinga na tuna hakika tutarejea kwa sababu sisi ni madiwani halali.”

Jiji la Tanga lilikuwa na madiwani 37, CUF wakiwa 20 na CCM 17 ambapo kwa sasa CUF imebakiwa na madiwani 15 baada ya wawili kujivua uanachama na watatu kuvuliwa, kwa mujibu wa taarifa na mkurugenzi Mayeji.

Inaelezwa kuwa Sakaya alipeleka barua ya kuwavua uanachama madiwani hao wiki iliyopita, kwa kile alichosema walikataa kuweka mgombea katika kata ambazo zilibaki wazi baada ya madiwani wa CUF kuhamia CCM.

Sakaya awajibu

“Wale madiwani akiwamo mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, walikataa kuweka mgombea maeneo ambapo madiwani wetu walihamia CCM, wakaanza malumbano wakisema wamepewa maagizo tuweke wagombea wa Chadema,” alisema.

Sakaya alisema madiwani hao walionywa na kupewa barua ya kujieleza lakini walikataa, ndipo wakavuliwa uanachama.

“Hatuwezi kuvunja katiba bila sababu za msingi, chama kinaongozwa kwa katiba. Inashangaza mtu kukataa kuweka mgombea wa chama chako na kulazimisha awekwe wa chama kingine.”

Alisema baada ya madiwani hao kupinga kufanya uchaguzi wa wagombea katika kata hizo, kamati tendaji ilipelekwa kuhoji kwa nini asisimamishwe mgombea wa CUF.

“Huyu Jumbe akasema amepewa maagizo kuwa zile kata wasimamishwe wagombea wa Chadema, kwa hali ya kawaida hakuna chama kitakachofanya kitu kama hiki,” alisema Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua. “Kata ni za CUF, leo unasema awekwe mgombea wa Chadema hili linawezekana kweli?”

Alisema madiwani hao walionywa na wakapelekewa barua, lakini walikaidi kujibu na kujieleza.

Mtatiro amshukia

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF upande wa Maalim Seif Sharif, Julius Mtatiro alimtuhumu Sakaya kutumiwa na CCM ili kukivuruga chama chao.

Mtatiro aliandika katika ukurasa wake wa Facebook jana akisema Sakaya anatumika kuvuruga maeneo ambayo CUF ina nguvu.

“Mpango huo unafanywa ili kuhakikisha hadi mwaka 2020 maeneo ambayo CUF ina nguvu sana, madiwani na wabunge wawe wamesambaratishwa ili kuirahisishia kazi CCM,” aliandika.

Akijibu tuhuma hizo, Sakaya alisema hana sababu ya kujibizana na Mtatiro kwa sababu chama kinaongozwa na katiba.

“Sina sababu ya kubwabwaja. Kama ni suala la kutumiwa, wao ndio vibaraka na wanatumika na Chadema. Hakuna wa kunitumia mimi na sina sababu ya kufanya hivyo, nitawashughulikia wote,” alisema.

Udiwani Arusha

Wakati huohuo, CCM wilayani Arusha imependekeza majina ya waliokuwa madiwani wa Chadema waliohamia CCM kuwania nafasi za udiwani kupitia chama hicho.

Waliopendekezwa ni Prosper Msofe (Daraja Mbili), Elirehema Nko (Osunyai), Obeid Meng’oriki (Terat), Emmanuel Kessy (Kaloleni).

Madiwani hao walijiuzulu kwa nyakati tofauti huku wakitaja hatua hiyo imetokana na kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Akizungumza na gazeti hili, katibu wa CCM wilayani humo, Musa Matoroka alisema fomu zilipelekwa katika ngazi ya kata kama utaratibu unavyoelekeza na miongoni mwa waliojitokeza ni madiwani waliojiuzulu.

Alisema majina hayo wameyapeleka Kamati ya Siasa mkoa kwa ajili ya kujadiliwa na yatafikishwa katika Halmashauri ya CCM mkoa kwa ajili ya kupitishwa.

Imeandikwa na Burhani Yakubna Rais Said, Tanga na Herieth Makweta, Dar.