NHIF yapunguza gharama za matibabu

Muktasari:

Uamuzi huo umepokewa kwa shangwe na madaktari, wakisema utasaidia kuwafikia wananchi wengi hususan wa vijijini ambao wamekuwa wakihaha kupata huduma za afya nchini.

Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepunguza gharama za matibabu katika hospitali na vituo vya afya.

Uamuzi huo umepokewa kwa shangwe na madaktari, wakisema utasaidia kuwafikia wananchi wengi hususan wa vijijini ambao wamekuwa wakihaha kupata huduma za afya nchini.

Katika uamuzi huo, gazeti la The Citizen liliandika jana kuwa mfuko huo sasa utakuwa ukiwalipa madaktari bingwa Sh15,000 badala ya Sh30,000 za awali na madaktari wa kawaida watalipwa Sh7,000 badala ya Sh10,000.

Mkurugenzi wa Masoko wa NHIF, Anjela Mziray alisema jana kuwa lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha wanachama wa mfuko wanapata huduma bora za afya zinazoendana na thamani ya fedha zao.

Pia, katika bei hizo mpya, NHIF imeshusha malipo ya gharama za matibabu zikiwamo za upasuaji ambao awali ungegharimu Sh600,000 sasa utalipiwa Sh150,000.