Nape afunguka Malima ‘kulipuliwa’ risasi na polisi

Muktasari:

Nape ametoa kauli hiyo takriban siku 55 baada ya askari kanzu mmoja kumtishia bastola wakati akijaribu kumzuia kwenda jengo la Hoteli ya Protea kuzungumza na waandishi wa habari.

Dar es Salaam. Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amevitaka vyombo vya dola kuangalia upya nguvu inayotumika kukamata raia ambao hawana silaha.

Nape ametoa kauli hiyo takriban siku 55 baada ya askari kanzu mmoja kumtishia bastola wakati akijaribu kumzuia kwenda jengo la Hoteli ya Protea kuzungumza na waandishi wa habari.

Pia ametoa kauli hiyo baada ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima ‘kufyatuliwa’ risasi na askari wa Jeshi la Polisi katika mzozo uliotokana na dereva wa mbunge huyo wa zamani wa Mkuranga kuegesha gari sehemu isiyoruhusiwa.

Na Nape hakusita kulinganisha matukio hayo mawili wakati alipoulizwa na mwandishi wetu.

“Jambo lililotokea kwa Malima ni sawa na lile lililonitokea,” alisema na kutoa hoja tofauti kufananisha matukio hayo mawili akionekana kukwepa kuzungumzia kesi iliyofunguliwa dhidi ya Malima ambaye ameshtakiwa kwa kosa la kuwazuia polisi kutekeleza wajibu wao.

“Ndiyo maana mimi ninaendelea kuishauri Serikali kuendelea kuilinda nchini yetu kwa namna tuliyoizoea,” alisema Nape.

Nnauye alisema kila nchi ina utaratibu wake ambao raia wameuzoea na hapa nchini utaratibu uliozoeleka tangu kudai uhuru ni mazungumzo ya diplomasia kwa raia msikivu na ambaye hana silaha yoyote.

Tukio la Malima kufyatuliwa risasi na polisi lilisambaa kwa kasi Jumatatu mchana baada ya watu tofauti kutuma picha za video katika mitandao ya kijamii.

Picha hizo zinamuonyesha Malima akizozana na askari mmoja wa Jeshi la Polisi ambaye baadaye alifyatua risasi hewani.

Baadaye askari huyo na wenzake waliokuwa wakijaribu kumzuia, walimchukua na kwenda naye kituo cha polisi ambako siku iliyofuata walimfikisha mahakamani.

Tukio la Nape lilitokea siku moja baada ya kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Harrison Mwakyembe.

Nape, ambaye wakati mabadiliko hayo yanafanyika alikuwa Arusha, aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, lakini kabla ya kuwasili eneo hilo waandishi waliondolewa hotelini na wakiwa nje walimuona akiwasili.

Wakati aliposhuka kutoka kwenye gari na kuanza kuelekea hotelini, askari wawili walijitokeza na kumzuia wakati akijibishana nao, mmoja alisogea nyuma na kutoa bastole na kumuelekezea, lakini askari mwingine ambaye pia hakuvalia sare, alimzuia.