Ndalichako aagiza Ofisa manunuzi wa Wizara kusimamishwa kazi

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako

Muktasari:

Chuo hicho kilipokea vifaa hivyo ambavyo viko chini ya kiwango huku vingine kutohitajika kwa matumizi ya maabara. 

Kasulu. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako, amemtaka katibu Mkuu wa wizara hiyo, Leonard Akwilapo kumsimamisha kazi Ofisa manunuzi wa wizara Audifasy Myonga kwa kufanya manunuzi ya vifaa vya maabara visivyo hitajika na kuvisambaza katika vyuo vya ualimu.

Ndalichako ametoa maamuzi hayo leo Julai 12, alipotembelea chuo cha ualimu Kasulu, mkoani Kigoma na kufanya kikao na watumishi kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Alisema chuo hicho kilipokea vifaa hivyo ambavyo viko chini ya kiwango huku vingine kutohitajika kwa matumizi ya maabara. 

“Serikali inaanza na ofisa manunuzi na baadaye itawachukulia hatua stahiki baada ya kukamilika kwa uchunguzi watu watakaokuwa wamehusika kupokea vifaa hivyo chuoni hapo kwani kama walijua vifaa hivyo havihitajiki kwanini walivipokea,” amesema Profesa Ndalichako

Amesema serikali kupitia wizara yake walinunua vifaa vya maabara kwa awamu mbili, awamu ya kwanza vifaa vya zaidi ya Sh298 milioni na awamu ya pili zaidi ya Sh759 milioni ambavyo vifaa hivyo vilisambazwa katika vyuo mbalimbali vya ualimu nchini.

"Nimeona shehena ya vifaa chuoni hapa ambavyo vimekaa tu tangu mwaka 2016 walipopokea ambavyo ukiwauliza wanasema havina kazi kwanini wapokee vitu ambavyo havina kazi na kukaa navyo?" amehoji waziri huyo.

"Niwaombe mniandalie taarifa ya kuomba vifaa hivyo na taarifa ya upokeaji wa hivyo vifaa baada ya hapo nitajua cha kufanya kwani hapa kila mtu anamtupia mpira mwenzie, na ikibainika kama kuna kitu kinaendelea serikali itaondoka na vichwa vya watu waliohusika, "amesema waziri Ndalichako.

Boharia chuoni hapo Meckisedeck Waziri, amesema wao walipokea vifaa hivyo vya maabara kutoka wizarani Desemba 13, 2016 na awamu ya pili walipokea Juni 23, 2017.