Ndege ya ATC ilivyotekwa 1982 kushinikiza Nyerere ajiuzulu- 12

Wednesday December 5 2018

 

By William Shao

Ingawa mambo haya yalitokea na yaliihusu sana Tanzania, habari za tukio la kutekwa kwa ndege ya Shirika la Tanzania (ATC) hazikuonekana sana katika vyombo vya habari vya ndani ukilinganisha na vya nje.

Katika utafiti wake, jarida la Africa Now la Aprili 1982 (uk 15) linasema: “Makumi kwa maelfu ya Watanzania walipenda kusikiliza vituo vya redio vya Sauti ya Kenya, Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Sauti ya Amerika (VoA) na hata Radio South Africa ili kupata habari za utekaji kuliko kufungulia redio ya nchi yao wenyewe.

Wakati huo, kituo cha Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), kinachomilikiwa na Serikali ndicho kilikuwa kikitamba nchi nzima wakati vituo vingine vilikuwa vidogo na vya sehemu au muda maalumu.

“Hakukuwa na sababu ya kuacha kutoa taarifa za utekaji wenyewe. Redio Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa redio za kwanza kabisa kutangaza kuwa ndege imetekwa,” liliandika jarida hilo.

“Kilichowafanya wahariri kubabaika ni yale madai ya watekaji kwamba Rais Nyerere ajiuzulu na pia madai yao kuwakilisha kundi la upinzani lililojiunda.”

Africa Now ilisema gazeti la chama tawala cha CCM wakati huo na kituo cha redio cha Serikali viliendelea kuchuja habari za kutekwa kwa ndege hiyo kwa lengo la kushinikiza Rais Julius Nyerere ajiuzulu.

Lakini angalau magazeti ya Serikali ya Daily News na Sunday News yalitumia busara kiasi.

“Sunday News la Februari 28 (1982), ambalo lilichapishwa siku mbili baada ya ndege kutekwa na hata baada ya kujulikana kwa madai yao yaliyorudiwa tena na tena ya kutaka Rais Nyerere ajiuzulu na hata baada ya kujitambulisha kuwa watekaji ni wanachama wa kikundi cha Harakati za Kidemokrasia za Vijana wa Tanzania, lilichapisha taarifa kuonyesha kuwa vijana hao hawajafahamika.

“Watekaji, ambao hawajatambuliwa bado na ambao shabaha yao haijajulikana, waliiteka ndege na kuamuru ipelekwe Nairobi, Jeddah, Athens kabla haijaenda London,” liliandika gazeti la Sunday News likikaririwa na Africa Now.

“Kwa siku kadhaa, hasa katika mji wa Dar es Salaam, makundi ya watu yalikuwa yakijikusanya kila eneo lenye redio, angalau waweze kupata habari nyingine tofauti na zile za Redio Tanzania.

“Hata familia za wale abiria waliotekwa, zilifungulia BBC kupata habari hizo ... Maneno kama ‘redio zetu wenyewe zinatudanganya’ yalisikika mara kwa mara mitaani.”

Hata hivyo, kwa wakati huo hakukuwa na Waziri wa Habari wa kujibu madai hayo. Aliyekuwa Waziri wa Habari, Benjamin William Mkapa, ndiyo kwanza alikuwa ameteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Canada.

Ijumaa ya Februari 19—ikiwa ni siku saba kabla ya kutekwa kwa ndege ya Tanzania—Rais Nyerere alimteua Mkapa kuwa balozi, hadi wakati wa uteuzi huo, Mkapa alikuwa Waziri wa Habari na Utamaduni tangu Novemba 1980.

Africa Now lilisema katika makala yake kuwa “jukumu la mwisho linabaki kwa wahariri walioonyesha kuwa ahadi yao ya kuandika habari za kweli inaelemewa na woga wa kuwaudhi wakubwa”.

Ndipo Jumanne ya Machi 2, 1982, toleo la 5834 la gazeti la Uhuru liliandika: “Serikali imesema kwamba watu na ndege ya ATC aina ya Boeing 737 iliyotekwa na kutua Uingereza Jumapili (iliyopita), inatarajiwa kurejea nyumbane baadaye wiki hii.

Lilinukuu taarifa iliyotolewa na Ikulu mjini Dar es Salaam kuwa abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo wangerejea kwa ndege nyingine

“Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Ndugu John Malecela, alisema kwamba abiria na wanahewa wa ndege hiyo watarejea nchini Alhamisi (Machi 4),” liliandika.

“Waziri alisema wizara yake imeteua kamati chini ya katibu mkuu wake, Ndugu Odira Ongara, ili kusimamia kurejeshwa kwa watu hao. Serikali pia imetoa shukrani nyingi kwa marubani na abiria waliokuwamo katika ndege hiyo kwa utulivu walioonyesha wakati wote wa mkasa.

“’Mashujaa hao wanastahili mapokezi makubwa siku watakaporejea nyumbani,’ taarifa hiyo ya Serikali imeeleza.”

Jumatano ya Machi 3, katibu mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Odira Ongara aliwaita waandishi wa habari na kuwaambia haja ya wananchi kujitokeza kwa wingi kuwalaki waliokuwa mateka.

“Tunawaomba wananchi wajitokeze na kuwapokea waliokuwa wametekwa,” liliandika gazeti hilo

Alhamisi ya Machi 4, gazeti la Uhuru liliripoti habari hiyo likisema: “Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameombwa kuwapokea kwa shangwe abiria 74 na wafanyakazi watano wa ndege ya ATC iliyokuwa imetekwa watakapowasili na ndege hiyo Dar es Salaam asubuhi hii (Alhamisi kutoka London, Uingereza.”

Ndege hiyo iliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam saa 3:05 asubuhi. Abiria waliokuwa wametekwa walipokewa kama mashujaa. Uwanjani hapo walikuwapo viongozi wa CCM na Serikali ambao waliwapokea na kwenda nao kwenye banda la mapumziko.

Pia kulikuwepo na vikundi mbalimbali vya ngoma kama cha Bora (kikundi cha utamaduni cha kiwanda cha viatu), Shirika la Nyumba la Taifa, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Muungano. Vyote hivi vilianza kutumbuiza saa 2:00 asubuhi.

Kuanzia Jumatatu ijayo usikose kusoma mfululizo wa makala maalumu kuhusu vita ya Tanzania na Uganda maarufu kama vita ya Kagera ambayo nchini Uganda ilijulikana kama vita ya Ukombozi iliyopiganwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Novemba 1978 hadi Aprili 1979.
Ni mambo gani yalijiri katika vita hiyo? Usikose ni ndani ya gazeti hili.

Advertisement