Ndugu asimulia bosi wa TCCIA alivyofyatukiwa risasi nyumbani

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwa marehemu, Mbezi Africana jijini Dar es Salaam jana, Faustus alisema kaka yake alipigwa na risasi iliyojifyatua wakati akisafisha bunduki yake.

Dar es Salaam. Faustus Mayanja, mdogo wa aliyekuwa rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Ndibalema Mayanja aliyefariki dunia kwa kufyatukiwa risasi ameeleza tukio hilo lilivyotokea.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwa marehemu, Mbezi Africana jijini Dar es Salaam jana, Faustus alisema kaka yake alipigwa na risasi iliyojifyatua wakati akisafisha bunduki yake.

“Tulikuwa watatu; mimi, kaka yangu na mdogo wetu. Kaka yetu alikuwa mgonjwa ndiyo maana nilitoka Bukoba nikaja kumuuguza. Mpaka anafikwa na mauti alikuwa kwenye wheel chair (kiti cha magurudumu).

“Alikuwa anasafisha bunduki nadhani kwa sababu afya yake ilikuwa imedhoofu ndiyo maana ilimponyoka,” alisema Faustus.

Alisema Ndibalema alikuwa akisafisha silaha hiyo ili kuirejesha kwa Jeshi la Polisi ndipo ilipomponyoka na kufyatuka risasi.

Faustus alisema walijaribu kumuwahisha hospitali, lakini kabla ya kushuka kutoka ghorofani waligundua kuwa alishafariki dunia.

Alisema mwili wa Ndibalema aliyefariki dunia Juni 14, umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo.

Faustus alisema kaka yake alikuwa mpenda watu, mcha Mungu na kiongozi wa familia.

Alisema kaka yake aliwahi kuwa kapteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na alistaafu mwaka 2015.

Kauli ya Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia tukio hilo, alisema taarifa za awali zilizopo ni kwamba Ndibalema alijiua kwa bahati mbaya. Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kujiridhisha na ukweli kuhusu tukio hilo.

Mazishi

Mwili wa Ndibalema unatarajiwa kuzikwa wiki ijayo baada ya ndugu na watoto wake waliopo nje ya nchi kuwasili. Msemaji wa familia hiyo, Gumbo Steven alisema mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumanne lakini bado wanasubiri kuwasili kwa ndugu na watoto wake.

Steven alisema iwapo kutakuwa na mabadiliko watatoa taarifa.

Juzi, makamu wa Rais wa TCCIA, Octavian Mshiu alisema Ndibalema alikuwa akiugua maradhi ya mifupa na maumivu ya viungo kwa muda mrefu na amewahi kutibiwa ndani na nje ya nchi.

Kabla ya kifo cha Ndibalema alikuwa mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ya Afrika Mashariki, mjumbe wa bodi mbalimbali ikiwamo ya TCCIA, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Baraza la Taifa la Ujenzi na Baraza la Taifa la Wafanyabiashara.