Pacha maarufu walioungana, Maria na Consolata, wafariki dunia

Muktasari:

Taarifa zilizoifikia Mwananchi Digital na kuthibitishwa na mkuu wa wilaya wa Iringa Richard Kasesela, zimebainisha kuwa mapacha hao wamefariki wakipishana kwa takribani saa 2.

 

Dar es Salaam. Pacha wa kipekee wa Tanzania walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti wamefariki dunia usiku wa leo (Jumamosi, June 2) katika hospitali ya mkoa ya Iringa.

Taarifa zilizoifikia Mwananchi Digital na kuthibitishwa na mkuu wa wilaya wa Iringa Richard Kasesela, zimebainisha kuwa mapacha hao wamefariki wakipishana kwa takribani saa 2.

"Wamepigania sana afya zao, mida ya saa moja hivi jioni ndio nimepokea taarifa za kifo chao na kwa sababu nilikuwa mazingira ya hospitali basi nilisogea kuwaona – na ni kweli hatunao,” amesema Kasesela.

Tanzia toka hospitali inaonyesha pacha wa kwanza alifariki majira ya saa 1 usiku, huku mwenzake akifariki saa 3 usiku.

"Kwa hiyo taarifa zaidi na nini kinaendelea kesho tutakipata. Mungu awapumzishe pema peponi, Amina.”

Mapacha hao wamekuwa na historia ya matatizo ya moyo. Tangu Disemba 2017 pacha hao walianza kuumwa na kulazwa hospitali ya mkoa ya Iringa.

Baadaye walihamishiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKIC) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walipolazwa kwa takribani miezi miwili kwa ajili ya matibabu mpaka waliporuhusiwa kurejea tena Iringa mnamo Mei 17.

Maria na Consolata walizaliwa wilayani Makete mkoani Njombe mwaka 1996.

Walihitimu darasa la saba katika shule ya msingi Ikonda, kisha wakajiunga na shule ya Maria Consolata iliyopo Kilolo mkoani Iringa ambapo walihitimu kidato cha nne.

Baada ya hapo, walijiunga na shule ya Sekondari ya Udzungwa wilani Kilolo walipohitimu kidato cha sita, ikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu) walipokuwa wakisomea fani ya ualimu.