Polisi waliohusishwa mauaji ya Akwilina waachiwa huru

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa

Muktasari:

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala eneo la Mkwajuni jijini hapa, wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema askari waliokamatwa wakihusishwa na kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini wameachiwa huru.

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala eneo la Mkwajuni jijini hapa, wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.

Aprili 20, 2018 Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP), Biswalo Mganga alisema jalada la kesi ya Akwilina amelifunga rasmi, kubainisha kuwa Jeshi la Polisi linapotumia nguvu kuzuia maandamano au vurugu na kusababisha mauaji, haliwezi kushtakiwa.

Leo Jumanne Julai 24, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuulizwa hatima ya askari hao, Mambosasa amesema wameachiwa, “ni kweli kuna askari tulikuwa tunawashikilia kwa ajili ya uchunguzi, upelelezi ulipomalizika imebainika hawahusiki.”

“Wale askari waliachiwa kwa maelekezo ya mwanasheria na ushahidi ulikuwa hafifu wa kuwatia hatiana.”

Awali, Mambosasa amewaonya watumiaji wa barabara kuwa makini na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa madereva wazembe hususan wa bodaboda ambao hawatii alama za barabarani.

 

Pia amezungumzia watuhumiwa wawili wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuhujumu mawasiliano ya Shirika la Mwasiliano Tanzania (TTCL).

Amewataja watu hao kuwa ni Kelvin Same, mkazi wa Tabata Segerea ambaye ni mfanyakazi wa TTCL kitengo cha huduma kwa wateja na Lilian Hosea ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach na mhasibu wa shirika hilo.

Amebainisha kuwa Julai 12, 2018 walipata taarifa kutoka kwa ofisa upelelezi wa TTCL  kuwa kuna wafanyakazi wa shirika hilo wanajihusisha na udukuzi wa data za kampuni kutoka taasisi za Serikali zinazotumia mtandao  wa TTCL.

Taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Maendele ya Jamii (Tasaf), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema watumishi hao wamesabishia hasara ya Sh46 milioni na kwamba uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.