Polisi wazungumzia vifo vya mahabusu, mfungwa jijini Mwanza

Wednesday April 15 2020

 

By Jesse Mikofu, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Mahabusu wawili na mfungwa mmoja katika gereza la Butimba jijini Mwanza nchini Tanzania wamefariki ikidaiwa walishambuliwa na wananchi wenye hasira na mwingine kupigwa risasi na askari wakati akijaribu kutoroka gerezani.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 15, 2020 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro inaeleza kuwa tukio hilo lilitokea jana Aprili 14. 2020 saa 12:30 jioni maeneo ya Butimba wilayani Nyamagana.

Amewataja mahabusu wanaodaiwa kushambuliwa na wananchi kuwa ni, Yusuph Benard (34) na Seleman Sif (28) waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji.

“Walijaribu kutoroka kwenye gereza ndipo askari magereza wakishirikiana na wananchi waliwakimbiza na kufanikiwa kuwakamata. Wananchi waliwashambulia kwa kipigo na kusababisha hali zao kuwa mbaya, walifariki dunia wakati wakiendelea na matibabu katika hospitali ya Mkoa ya Sekoutoure,” amesema.

Amebainisha mtuhumiwa wa tatu kati tukio hilo, George Aloyce (34) alipigwa risasi na askari eneo la Mabatini na na kufariki wakati akipatiwa matibabu hospitali.

Amesema Aloyce aliyekuwa amefungwa miaka 15 kwa kosa la uhujumu uchumi lakini akiwa na kifungo kingine cha kutoroka chini ya ulinzi miezi sita.

Advertisement

Amesema  baada ya kukamatwa katika jaribio hilo aliwaeleza askari kwamba kama wangefanikiwa kutoroka wangemchukua dereva taksi eneo la Mabatini kisha awasafirishe hadi Katoro mkoani Geita.

“Wakati akiwapeleka askari kuwaonyesha dereva huyo, waliposhuka eneo la Mabatini akajifanya anataka kuonesha alipo lakini akakimbia ndipo askari walipiga risasi hewani kumuamuru kusimama lakini akakataa na walimpiga risasi miguuni. Naye alipoteza maisha akipata matibabu hospitalini,” amesema

Advertisement