Polisi yawashikilia wawili kwa kutorosha wanafunzi

Muktasari:

Wanafunzi hao walitoroshwa kwa lengo la kutafutiwa kazi za ndani Dar es Salaam na Morogoro

Iringa. Polisi mkoani Iringa inawashikilia watu wawili wakazi wa wilaya ya Kilolo kwa tuhuma ya kuwatorosha wanafunzi watano wa Shule ya Sekondari Mlafi kwa lengo la kuwapeleka jijini Dar es salam kwa ajili ya kufanya kazi za ndani.

Akizungumza leo Ijumaa Agosti 10, 2018 kamanda wa polisi mkoani humo, Juma Bwire amesema tukio hilo lilitokea mji mdogo wa Ilula tarafa ya Mazombe wilayani Kilolo.

Bwire amesema wanafunzi hao walitoweka majumbani mwao tangu Julai 29, 2018, kwamba walisafirishwa kwa bodaboda kutoka eneo la Mlafi hadi Ilula.

 

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Tulizo Mtega (19) na Rosemary Msasalage (18) wote wakazi wa Ilula.

 

Amebainisha kuwa watuhumiwa hao waliwarubuni wanafunzi hao kuwa kuna kazi za kuuza sukari Morogoro na Dar es Salaam.

 

Amewataka wazazi kuwa makini na watoto wao kwa maelezo kuwa Serikali imepiga marufuku watoto kutumikishwa kazi za ndani.

 

Katika hatua nyingine, mkazi wa Mwangata mkoani hapa, Dina Juma(45) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumtumikisha kingono mtoto wake wa miaka 14, kwa lengo la kujipatia kipato na alipogoma alimshushia kipigo

 

Amesema uchunguzi wa daktari umeonyesha kuwa mtoto huyo amefanyiwa vitendo vibaya kwa muda mrefu.