Profesa Mjerumani azitahadharisha nchi za EAC kuhusu Epa

Monday April 15 2019

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kufanya tathmini mpya kwenye mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara (Epa) baina yao na Umoja wa Ulaya (EU).

Akizungumza na vyombo vya habari leo Aprili 15 jijini Dar es Salaam, mshauri mwelekezi katika suala la Epa, Profesa Helmut Asche kutoka Ujerumani amesema uhusiano kati ya pande hizo bado ni muhimu.

Amesisitiza kwamba nchi za EAC bado zina nafasi ya kutunza umoja wao katika suala la Epa ili kwa pamoja watoke na msimamo mmoja unaokubaliwa.

"Kuna haja ya kuifanyia tathmini rasimu ya mkataba kati EAC na EU ili kupata msingi mpya wa makubaliano ambao utamaliza kabisa suala hili," amesema Profesa Asche.

Profesa Asche ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Leipzig cha Ujerumani, amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa Tanzania hasa sekta binafsi na pia kwa nchi za Ulaya.

Amesema endapo nchi zote za EAC zitasaini makubaliano hayo itasaidia kuimarisha tozo za pamoja kwa bidhaa kutoka nje, pia kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya pande hizo.

"Rwanda na Kenya tayari wamesaini mkataba huo lakini Tanzania bado haijasaini. Pia huko Afrika Magharibi, Nigeria nayo haijatia saini, sababu zao wote zina maana. Wanataka kulinda viwanda vyao, lakini tunatokaje hapa," amesema profesa huyo.

Advertisement