Programu kuendeleza ubunifu wa vijana yaanzishwa

Wednesday September 11 2019

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom kwa kushirikiana na mtandao wa Smart Lab wameanzisha programu maalumu kwa ajili ya kuwaendeleza na kuendeleza ubunifu wa vijana.

Programu hiyo ambayo imetengewa Dola 150,000 za Marekani sawa na Sh345.2 milioni itawanufaisha Watanzania 15 wenye mawazo ya ubunifu yanayohusu huduma za kifedha, elimu, afya na simu.

Katika uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika leo Jumatano Septemba 10, 2019 mkurugenzi mkuu wa Vodacom, Hisham Hendi amesema lengo ni kuwaunga mkono wabunifu kwa kuufanya ubunifu wao kuwa wa manufaa.

"Vodacom tunaunga mkono masuala ya ubunifu, vijana wana mawazo mazuri lakini walikosa kuungwa mkono, kupitia programu hii tutapokea maombi ya vijana wengi na 15 watakaochaguliwa. Tutawaunga mkono mkono kupitia kituo kitakachokuwa hapa makao makuu na baada ya hapo tutawapata washindi watatu," amesema Hendi.

Ofisa Mshiriki wa Smartlab Edwin Bruno amesema  wahusika wa programu hiyo ni lazima wawe Watanzania na manufaa watakayoyapata ni kujengewe ujuzi, kusaidiwa mahitaji ya kufanikisha ubunifu wao kuwa biashara, promosheni na kutafutiwa masoko ya bidhaa au huduma watakazozibuni.

"Katika nchi nyingine programu hizi zinafanyika kwa ukubwa sisi bado tuko nyuma kidogo lakini tunataka kesho na kesho kutwa ubunifu uchukue nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi yetu, nchi hii ina wabunifu wengi na tunatarajia watu wengi zaidi kuomba kushiriki katika programu hiyo," amesema Bruno.

Advertisement

Amesema baada ya programu hiyo anaamini mawazo ya sasa ya vijana yatakuwa ni huduma au bidhaa ambayo itakuwa bishara inayoingiza fedha na kutoa ajira kwa Watanzania.

Advertisement