Raia watano Rwanda kortini kwa kuwatishia mashahidi

Muktasari:

  • Ni katika kesi za mauji ya kimbari zinazoendelea jijini Arusha

Arusha. Watuhumiwa watano raia wa Rwanda wamepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za mauaji ya kimbari wakituhumiwa kwa makosa matatu ikiwamo kutishia mashahidi.

 Watuhumiwa hao, Maximilien Turinabo, Jean De Dieu Ndagijimana, Dick Prudence Munyeshuli, Anselme Nzabonimpa na Marie Rose Fatuma wamepandishwa kizimbani leo mbele ya Jaji Seon Ki Park.

Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka matatu ikiwamo kuingilia uhuru wa mashahidi, kuwachochea wengine kuvunja ushahidi na kosa la kuvujisha utambulisho wa mashahidi linalomkabili Munyeshuli na Turinabo kinyume cha amri ya Mahakama kulinda haki za mashahidi.

 Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kwa lengo la kuvuruga kesi dhidi ya waziri wa zamani wa Rwanda, Augustin Ngirabatware iliyotolewa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela na ambaye rufaa yake itasikilizwa Septemba 24 juu ya mauaji ya kimbari.

Baada ya kusomewa mashtaka yao watuhumiwa wote walikana kuhusika  na wameendelea kuwekwa kizuizini hadi watakapoomba dhamana.

 Hata hivyo dhamana yao itategemea na majadiliano ya Serikali ya Rwanda na mahakama hiyo.

 Kwa mujibu wa Jaji Seon Ki Park kuna baadhi ya vipengele vya sheria vinapendekeza kesi kama hiyo ifanyike katika nchi husika ya Rwanda, hivyo Mahakama itajadiliana na Serikali ya nchi hiyo kama itakubali kuendeleza kesi hiyo.

“Kama watuhumiwa wataridhia jambo hilo basi utaratibu ufanyike wa kuhamisha na ikishindikana watatangaza tarehe ya kuanza kusikiliza,” alisema.

 Vibali vya kukamatwa watuhumiwa hao vilitolewa Agosti 24 na walikamatwa Rwanda Jumatatu wiki hii na kufikishwa katika Mahakama hiyo ya kimataifa yenye makao yake makuu jijini Arusha.