Ripoti mali za CCM yabaini wizi, utapeli

Muktasari:

Kamati imepitia nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo.

Dar es Salaam. Ripoti ya tume ya kuhakiki mali za CCM iliyoundwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maalidili katika uendeshaji wa miradi ya chama.

Baada ya Rais Magufuli kupokea ripoti ya tume hiyo iliyoongozwa na Dk Bashiru Ally, alisema itapelekwa katika kamati kuu na halmashauri kuu ndani ya mwezi huu ili kuijadili na viongozi kutoa maelekezo.

“Huwezi ukaanza kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi, chama nacho tunataka tukisafishe, mambo ya rushwa na ufisadi yaishe ili Tanzania iende vizuri, ndio maana tumeunda tume ya Dk Bashiru Ally, imefanya kazi nzuri sana na ripoti hii tutaipeleka kamati kuu na halmashauri kuu ndani ya mwezi huu ili tuijadili na viongozi watoe maelekezo.”

Rais Magufuli aliwaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria hafla ya uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vya juu vya chama.

Akizungumzia changamoto ilizokabiliana nazo, Rais Magufuli alisema, “Nilipokuwa nateua tume hii nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi.”

Awali, Dk Bashiru alisema uhakiki huo umefanywa kwa mali za chama hicho tawala zilizo chini ya baraza kuu, jumuiya za chama na kampuni zake.

Alisema wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo, walitembelea maeneo yenye mali za chama hicho, kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa.

Alisema kamati imepitia nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo.

Akizungumzia ripoti hiyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Phillip Mangula aliipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na kusisitiza taarifa yake imedhihirisha kuwa baadhi ya watu waliooneka kukisaidia chama hawakuwa wanakisaidia, bali walijinufaisha.

Tume hiyo ilitangazwa Desemba 20, mwaka jana ikiwa na wajumbe tisa. mbali ya Dk Bashiru, wengine ni Walter Msigwa, Albert Msando, Galala Wabanhu (Hananasif), Albert Chalamila, William Sarakikya, Komanya Kitwara, Dk Fenela Mkangara na Mariam Mungula.