SMZ: Idadi ndogo ya mabalozi kisiwe chanzo cha vurugu

Muktasari:

Wawakilishi wataka kujua vigezo vinavyotumika

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema licha ya kutoa mabalozi tisa kati ya 41 wa Tanzania wanaowakilisha nje, idadi hiyo haijawa sababu ya kuanzisha migongano katika masuala ya Muungano.

Waziri ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alisema hayo jana katika mkutano wa baraza la wawakilishi alipojibu swali la nyongeza la mwakilishi wa Paje, Jaki Hashim Ayoub.

Mwakilishi huyo alihoji sababu za msingi zinazozingatiwa hadi Zanzibar kupata idadi ndogo ya mgawanyo wa mabalozi.

Akijibu swali hilo, Aboud alisema suala la uteuzi wa mabalozi linaangalia zaidi vigezo kwa mteuliwa anayeiwakilisha nchi.

Waziri alisema licha ya kiwango hicho, ni wazi kuwa Zanzibar imenufaika na inaendelea kunufaika kwa kupata nafasi za ubalozi.

Aliwataja baadhi ya Wazanzibari walionufaika na nafasi za ubalozi kuwa ni Ali Karume, Amina Salum Ali, Seif Ali Iddi na Mohamed Ramia. Akijibu swali la msingi la mwakilishi wa Tunguu, Simai Mohamed Said aliyetaka kujua utaratibu kwa Wazanzibari waliopo nje ya nchi kupata huduma za ubadilishiwaji wa pasipoti, waziri alisema hilo si suala la Zanzibar au Tanzania Bara bali ni la Muungano.

Alisema kila raia wa Tanzania ana haki sawa ya kupatiwa huduma hiyo na kwamba, utaratibu uliopo ni wa aina moja kwa Watanzania kufika ofisi za ubalozi kwenye nchi husika na kupatiwa huduma.

Waziri alisema Serikali imejipanga kupeleka mashine maalumu Pemba ili kurahisisha kazi ya ubadilishwaji pasipoti ili kupata mpya za kisasa.

Kwa mujibu wa sheria licha ya kuwa pasipoti hutolewa kwa jina na maelezo ya mwombaji, hati hiyo hubaki kuwa mali ya Serikali. Hii ndiyo sababu Serikali huweza kumnyang’anya mtu pasipoti inapohisi jambo fulani.

Haki ya mwombaji aliyepewa pasipoti anayo haki ya matumizi na uhifadhi wake lakini mmiliki mkuu ni Serikali.