Safari ya kuondoa mifuko ya plastiki yaanza

Muktasari:

Wadau wakiwemo wamiliki wa viwanda na wazalishaji  wa mifuko ya plastiki na mbadala wamekutana kujadiliana kwa ajili ya kutoa mapendekezo kwa Serikali namna ya kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki.


Dar es Salaam. Naibu Katibu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Balozi Joseph Sokoine amesema uwekezaji katika mifuko mbadala ni fursa muhimu kwa sababu teknolojia yake inatumia gharama nafuu ambayo ni rahisi kwa mazingira ya kiuchumi.

Balozi Sokoine amesema uwekezaji wa mifuko mbadala ni fursa pia kwa kila mtu wakiwamo wajasiriamali pamoja na vikundi vidogo na kampuni mbalimbali.

Naibu katibu huyo ametoa kauli hiyo, leo Jumanne Novemba 6, 2018 wakati akifungua kikao cha wadau kuhusu fursa za uwekezaji kwenye uzalishaji wa mifuko mbadala ili kuondokana na matumizi ya mifuko ya plastiki.

Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wa mazingira, wamiliki na wazalishaji wa mifuko ya plastiki na mbadala.

"Hii ni fursa ya kipekee kwa sababu mifuko mbadala ipo mingi, unaweza ukazalisha ya karatasi, nguo, ukili. Kila mmoja achangamkie kwa nafasi yake," amesema Balozi Sokoine.

Haya hivyo,  Balozi Sokoine amesema ni vyema mifuko hiyo mbadala ikawa na bei nafuu na kwa kiwango ambacho wananchi wengi wataimudu.

Kwa mujibu wa Balozi Sokoine, lengo la kikao hicho ni kupata mwelekeo na hatua muafaka za kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaochangiwa na matumizi ya mifuko ya plastiki.

Amesema matumizi ya mifuko ya plastiki yameongezeka kwa sababu hutolewa bure kwenye maduka, masoko, migahawa na maeneo mengine.

Enock Julius, kutoka Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, amesema bado matumizi ya mifuko ya plastiki ni makubwa na inakadiriwa  kila Mtanzania anatumia mifuko mitatu hadi minne kwa wiki.

"Kwa hesabu za haraka Watanzania wanatumia mifuko ya plastiki bilioni 7, 8 hadi 10 kwa mwaka. Mifuko ya plastiki inadumu kwa muda mrefu kuanzia miaka 100 hadi 500 bila kuoza (ardhini)," amesema.