Saratani ya kizazi yaua 300,000 kwa mwaka

Tuesday February 5 2019

 

By Harieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kuwapatia chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi (HPV) mabinti wenye miaka tisa hadi 14; Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa saratani hiyo inaua zaidi ya wanawake 300,000 kila mwaka duniani, wengi kutoka nchi zinazoendelea.

Jana, ilikuwa Siku ya Saratani Duniani kaulimbiu ya Tanzania ikiwa ni ‘Mimi ninaweza, nitapiga vita saratani.’

WHO inaeleza kuwa saratani ya shingo ya kizazi ambayo ikigundilika mapema inatibika, husababishwa na kirusi cha ‘Human Pappiloma Virus’ na huambukizwa kwa njia ya kujamiiana.

Princess Nothemba Simelela ambaye ni mkurugenzi mkuu msaidizi wa WHO alisema jana kuwa tatizo lililopo katika nchi zinazoendelea ni ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi wa kuwapima wanawake na kuwatambua kama wana saratani ya shingo ya kizazi.

“Wanawake katika maeneo ya vijijini, mara nyingi ni vigumu kufika kliniki ambako wanaweza kupimwa saratani na kutibiwa,” alisema Simelela.

Mwaka jana katika uzinduzi wa chanjo ya saratani nchini, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali ilikuwa na chanjo 600,000 kwa ajili ya mabinti, lakini changamoto ni kuwafikia wote nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), mwaka 2017 waliougua saratani ya shingo ya kizazi nchini ni 1,958.

Akitoa tamko la Siku ya Saratani Duniani mjini Dodoma jana, Ummy alisema mwaka 2018 wagonjwa wapya wa saratani kwa jumla waliohudumiwa ni 14,028 ambao ni sawa na asilimia 25.5 ya wagonjwa wote waliokadiriwa kuwapo nchini.

“Wagonjwa waliohudumiwa walifika kupata huduma katika hospitali ya Ocean Road (7,649) Bugando (2,790), KCMC (1050), Muhimbili (1,321) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ni 218 na wengine 1,000 walipata huduma katika hospitali binafsi ikiwamo Aga Khan, Kairuki, Hindu Mandal, Besta na kwingineko mikoani,” alisema Mwalimu.

Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya saratani, Mkurugenzi wa Tiba ORCI, Dk Crispin Kahesa alisema: “Miaka mitatu iliyopita saratani ya kwanza ilikuwa ni ya shingo ya kizazi inayosababishwa na virusi vya HPV ikifuatiwa na ya ngozi inayosababishwa na kirusi cha HHV8 ambayo ina uhusiano mkubwa na virusi vya Ukimwi (VVU), lakini hii kwa sasa inashuka.”

Dk Kahesa ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya satarani, alisema zamani Ocean Road pekee ilitoa huduma lakini kwa sasa KCMC, Bugando, Mbeya, Benjamin Mkapa na binafsi kama Aga Khan, Besta kote wanatoa na imesaidia kuwavuta wengi.

Mkazi wa Mbeya, Pili Sankwa anayetibiwa saratani ya shingo ya kizazi alisema alianza kuumwa mwaka 2015 wakati huo alikuwa akisikia maumivu kiasi kabla ya kupima kwa hiyari kujua nini kinachomsumbua.

“Nilisikia kampeni ya wanawake kupima saratani ya shingo ya kizazi na matiti, wakanipima vipimo vikaenda Muhimbili, walisema nina saratani. Nililetwa Ocean Road nikapokea matibabu bure. Nashauri kina mama wengine huko vijijini waje kwa wingi kwa maana tunapona kila baada ya miezi mitatu ninahudhuria kliniki.”

Saratani ya koo

Mbali na saratani ya shingo ya kizazi, nyingine ambayo imeelezwa kushika kasi nchini ni ya koo.

Mkurugenzi wa kitengo cha magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Harrison Chuwa alisema kitengo chake kinapokea zaidi wagonjwa wa saratani hiyo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Saratani hizi nyingi zimetokana na mtindo wa maisha na kula vyakula vya mafuta, pombe kali, kutofanya mazoezi, vyakula vilivyokaushwa kwa moshi, vilivyosindikwa na nyama nyekundu zimeonyesha kusababisha kwa kasi tatizo hili.

“Kutokana na mfumo wa maisha, tumeanza kuona vijana wa miaka 30 wakiwa wameanza kupata saratani ya mfumo wa chakula (koo), ikiwa inatuambia kwamba labda katika jamii yetu kuna vinasaba vya saratani, hivyo ni fursa ya kufanya uchunguzi ili kubaini tatizo hilo chanzo chake,” alisema Dk Chuwa.

Pia, alisema saratani hiyo ikimpata kijana mwenye chini ya miaka 30, mara nyingi huwa ni za kurithi.

Dk Chuwa alisema ni wakati muafaka kwa wengi kuanza kupima mapema ili kubaini iwapo wana matatizo ya saratani au vinginevyo.

Mgonjwa aliyelazwa ORCI akitibiwa saratani ya koo, Baltazari Tarimo (51) alisema aliugua maradhi hayo mwaka jana na anaamini yametokana na mfumo wake wa maisha.

“Nilikuwa mnywaji mzuri tu wa bia na konyagi. Sigara nilikuwa navuta na mpaka naanza kuugua maradhi haya nilikuwa bado navuta, awali nilipougua nilitibiwa kwa muda mrefu na tiba asili ila nashukuru baada ya matibabu hospitalini ninaendelea vizuri,” alisema Tarimo.

Advertisement