Sekretarieti ya Maadili kuwahakiki viongozi 600

Tuesday June 11 2019

 

By Tausi Mbowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza kufanya uhakiki wa mgangano wa kimasilahi wa viongozi wa umma 600 walioko kwenye mikoa 12.

Lengo la uhakiki huo ni kuangalia taarifa za mali na madeni kupitia tamko la rasilimali na madeni walizojaza viongozi hao, wenza wao pamoja na watoto wao walio chini ya miaka 18 kama zinawiana.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu, Harold Nsekela imeitaja mikoa hiyo kuwa ni; Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Dodoma, Tabora, Singida, Dar es Salaam na Shinyanga.

Jaji Nsekela alisema shughuli hiyo ni ya kawaida kwa sababu sekretarieti ilianzishwa ili kusimamia mienendo na tabia za viongozi wa umma pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 pamoja na marekebisho yake.

“Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma inatoa wito kwa wote ambao watahusika katika shughuli hii kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo,” Inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa viongozi hao 600 wanaohusika na uhakiki huo, mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini wa taasisi hiyo, Honoratus Ishengoma alisema, “sheria yetu ukiiangalia vizuri kifungu cha 4 kinataja aina ya viongozi tunaowasimamia kutoka mihimili yote mitatu. Aina za viongozi wanaohakikiwa wanatokana na mihimili hiyo.”

Advertisement

Ingawa Ishengoma hakutaka kuwataka moja kwa moja majina yao baadhi yao ni; madiwani, wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, mahakimu pamoja na majaji.

Ishengoma alipoulizwa shughuli hiyo ya uhakiki imeanza lini alisema, “kazi imeanza rasmi jana tunahakiki mali za viongozi dhidi ya tamko lake la rasilimali na madeni yake ili kujiridhisha endapo taarifa alizozijaza zinawiana.”

Alisema viongozi wa mikoa hiyo watafanyiwa uhakiki pamoja na wenza na watoto wao walio na chini ya miaka 18 ambao hawajaoa wala kuolewa.

Alisema katika utendaji wa kiongozi anatakiwa kuzingatia masilahi ya umma badala ya yake binafsi ili kuepuka mgongano. Iwapo itatokea hivyo kiongozi anapaswa kueleza bayana jambo hilo.

Alisema mgongano wa masilahi hutokea pale kiongozi anapozingatia mambo yake binafsi badala ya umma katika utoaji wa uamuzi. “Mfano kiongozi anapotoa zabuni kwa kampuni yake binafsi au mtu wa karibu ni kosa kimaadili hivyo Sekretarieti ya Maadili itaangalia yote hayo,” alisema.

Ishengoma alisema katika uhakiki huo Seketareti itamfuata kiongozi mwenyewe mahali halipo.

Alipoulizwa baada ya uhakiki watakaobainisha na ukiukwaji wa maadili kipi kitafuata alisema, “wanaobainika kwenda kinyume na sheria watafikishwa katika Baraza la Maadili.”

Advertisement