Sendeka asema taarifa zinasambazwa na wabaya wake

Muktasari:

Adai lengo ni kumchonganisha na viongozi wa Serikali

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ametoa lugha mbaya dhidi ya Bunge na Serikali ni za uzushi zenye lengo la kumchonganisha na vyombo hivyo vya Dola.

Akizungumza leo Jumatano Januari 10, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Longido, Sendeka amesema taarifa hiyo iliyoanza kusambaa tangu juzi inapaswa kupuuzwa.

“… umahiri na heshima niliyoipata nchini na kwenye Bunge ni kubwa. Nilikwenda bungeni kutimiza wajibu kama mtuhumishi makini, sikwenda bungeni kuongeza idadi ya wabunge, nilikuwa mwakilishi nyinyi mnajua na Tanzania inajua"alisema.

Amesema vyama vya upinzani vimepata kiwewe na kuanza kumgombanisha na viongozi wa Serikali kwa kusambaza habari za uongo.

“Habari hizi mzipuuze kwa kiwango kinachostahili, wananchi wa Longido wekeni fikra zenu katika uchaguzi wa jumapili,” amesema.

Wakati Ole Sendeka akieleza hayo, Spika wa Bunge, Job Ndugai jana aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji mkuu huyo wa mkoa kuhusu kauli anayodaiwa kuitoa.

Sendeka aliyewahi kuwa mbunge wa Simanjiro anadaiwa kutoa kauli zilizoashiria kejeli kwa chombo hicho cha kutunga sheria ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa kwa kipande cha sauti inayodaiwa kuwa ni yake, akieleza jinsi Bunge lisivyokuwa mathubuti.