Serikali ilivyoamua kuweka jicho katika gharama sekta ya gesi, mafuta

Tuesday June 11 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Wahenga walisema kupotea njia ndiyo kufahamu njia na kila binadamu hujifunza kutokana na makosa, hivyo kufanya kosa bila kujua pengine si kosa ila kurejea kosa lile lile hutafsiriwa kuwa uzembe.

Wadau wa sekta ya gesi wanasema Mikataba ya Uendelezaji wa Madini (MDA), Sheria ya kodi ya mwaka 1997 na Sheria ya madini ya mwaka 1998 kabla ya mabadiliko ya 2010, zilishawishi mwekezaji kudanganya gharama zake halisi za uwekezaji kwa unafuu wa matangazo ya hasara za kila mwaka.

Kwa mfano, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’i anasema kosa kubwa lilionekana katika Sheria ya kodi ya 1997 kupitia kipengele kilichoitaka Serikali kuchangia asilimia 15 ya hasara aliyotangaza mwekezaji katika mtaji wake husika.

Hii inamaanisha kwamba, endapo mwekezaji alitangaza kupata hasara ya dola 30 kati ya dola 100 alizowekeza mwaka uliopita katika uzalishaji, basi mwekezaji huyo hatalipa chochote serikalini na badala yake Serikali itamwongezea asilimia 15 ya dola 30 aliyotangaza hasara katika mwaka unaofuata wa uzalishaji.

Kutokana na makosa hayo yaliyoathiri mapato kwa Taifa, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) iliyopewa nguvu chini ya Sheria ya Petroli ya 2015, imeanzisha ukaguzi wa Mikataba ya ugawaji mapato (PSA) kuhusu matumizi halisi ya fedha zilizotumika wakati shughuli za utafiti wa gesi asilia katika vitalu 11 nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni anasema sababu ya ukaguzi huo ni kuhakikisha kampuni zote zinafanya matumizi kwa misingi ya PSA.

Advertisement

Anasema ukaguzi huo unazingatia gharama zilizotumika ikiwamo maeneo ya ununuzi, ajira na matengenzo. “Ataeleza anatarajia kuleta wataalamu wangapi wa kufanya matengenezo kila baada ya miezi mingapi ili ukaguzi ukianza iwe ndani ya makubaliano.”

“Kwa mfano mtafiti anasema alitumia dola 58 milioni kwenye utafiti, je mishahara, ununuzi, alilipa PURA, alisafiri, alilipa bima kiasi gani. Lazima matumizi yaakisi uhalisia wa fedha hizo,” anasema Sangweni.

Changamoto katika PSA

Sangweni anasema kaguzi za awali kwa mwaka 2016 zilikamilika katika mikataba yote 11 lakini majadiliano bado yanaendelea kwa baadhi ya kampuni. Aidha, ukaguzi wa hesabu za mwaka 2017 umeshafikia mikataba mitano kati ya 11.

Kwa mujibu wa PURA, ukaguzi huo unahusisha tafiti zilizoanza tangu mwaka 1952, zinazoendelea na zilizoingia hatua ya uzalishaji kupitia vitalu vya Songosongo, Mnazi Bay na Kiliwani. Vitalu vinane bado viko katika hatua ya utafiti.

Ukaguzi huo kwa mwaka 2017, unahusisha kampuni zote zenye PSA, ambazo ni Shell Tanzania, Pan African Energy Tanzania (PAET), Kampuni ya TPDC, Heritage Oil, Ndovu Resources Ltd, Equinor na Swala, ukijikita katika gharama zilizokubalika.

Hata hivyo, Sangweni anasema changamoto nyingine zinaweza kujitokeza kutokana na makubaliano yaliyofanyika ndani ya mikataba. “Kwa mfano unaweza kukuta kwenye mkataba ilikubaliwa gharama za usafiri wa ndege za kikazi, na mkataba haukuweka ukomo. Utafanya nini?” anahoji Sangweni.

“Wakati wa makubaliano ilidhaniwa mtafiti atasafiri mara nne kwa mwezi lakini sasa ana safari za kila siku asubuhi na jioni, kwa hiyo inabidi mrudi mezani ili kupunguza angalau mara nne kwa mwezi lakini wakati mwingine bado mwekezaji hataki, anaendelea kusimamia makubaliano ya mkataba, kwa hiyo kuna mabishano kama hayo.”

Joto la majadiliano

Katika hatua nyingine Sangweni anasema baadhi ya kampuni ambazo hakuzitaja zimekataa kukubaliana na baadhi ya hesabu zilizofanywa na mamlaka hiyo, akisema ni jambo la kawaida kutofautiana hadi mwafaka utakapopatikana.

Anasema changamoto inajitokeza katika ufafanuzi wa kila muamala uliohusika kwenye matumizi ya fedha kwa kila kitalu. “Tumekuwa na mvutano wa kutokukubaliana baadhi ya hesabu zilizotilliwa shaka na PURA.”

“Kawaida ya kaguzi kuna kukubaliana na kutokubaliana. Kwa mfano, tunakagua na tunawapelekea ‘recommendations’ (mapendekezo) yetu kwamba sisi tumeona katika 100 uliyodai, labda 30 tu ndiyo gharama halisi, 70 ni feki. Na wao wanajibu wanasema 70 ni gharama halisi,” anasema.

“Mhasibu wao lazima aweke vitu vya ‘kui-challenge’ Serikali. Kwa hiyo bado ni kaguzi za awali kwa sababu kuna kujibizana kabla ya kufikia consensus (maridhiano ya pamoja).”

Kampuni ya mafuta ya Shell inakiri kuwa miongoni mwa kampuni zilizoendelea na mazungumzo baada ya kufayiwa ukaguzi wa hesabu za PSA, katika gharama za uwekezaji wa shughuli za utafiti wa gesi na mafuta. Kauli hiyo imekuja baada ya kuulizwa endapo kuna hatua yoyote ya ukaguzi huo iliyofanyika na haijafikia makubaliano.

Genevieve Kasanga, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Kamapuni ya Equinor kupitia taarifa ya baruapepe anasema shughuli za ukaguzi wa vitabu na oparesheni zake zimekuwa zikifanyika mara kadhaa katika kitalu namba (2) na bado kampuni hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa kaguzi zijazo.

“Tutashirikiana nao (PURA), katika kipindi cha ukaguzi ili kuhakikisha hili linafanikiwa kwa ufanisi,” anasema Genevieve kupitia taarifa hiyo ya Equinor iliyowekeza zaidi ya dola 2 bilioni za Marekani tangu mwaka 2011 ilipoanza uchunguzi wa uchorongaji katika Kitalu namba (2) na kufanikisha zaidi ya futi za ujazo trilioni 20 katika kina kirefu cha bahari ya Hindi, Kusini mwaka Tanzania.

Ukaguzi huo unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kupitia hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2018/19, akisema pamoja na mambo mengine, PURA itaanza ukaguzi wa hesabu za PSA.

Kalemani kupitia hotuba yake anasema ukaguzi wa PSA ya kitalu namba (2) umekamilika.

Umuhimu wa ukaguzi

Kwa mujibu wa PSA, mwekezaji amepewa vipindi vitatu vya miaka tisa ili kukamilisha shughuli za utafiti kwa gharama zake na baada ya kuanza uzalishaji, atajirejeshea gharama hizo (Cost recovery) bila udanganyifu kwa utaratibu uliobainishwa na mkataba wa PSA ndani ya miaka 25 ya uzalishaji.

Pamoja na faragha ya mikataba hiyo, Sangweni anasema makadirio katika urejeshaji wa fidia hizo za mwekezaji ni wastani wa asilimia 70 ya mapato katika kila mwaka. Aidha, asilimia 30 inayobaki kama faida, Serikali hugawana na mwekezaji, ikichukua kiasi kisichopungua asilimia 75 huku mwekezaji akichukua asilimia 25.

Katika hatua nyingine, Olang’i anasema ukaguzi huo unatoa mwelekeo wa Serikali kupata mapato yake halisi baada ya kuanza uzalishaji.

“Kwa sababu mwekezaji akifanya udanganyifu kwa kujiongezea gharama wakati wa utafiti, ‘cost recovery’ itakuwa kubwa kwa hiyo Serikali itachelewa kuanza kupata faida yake stahiki, kama ilitakiwa kuanza kupatikana baada ya miaka 10 inaanza kupata baada ya miaka 20 kwa sababu ya udanganyifu, hivyo Serikali inakuwa imeibiwa mapato kwa miaka zaidi ya 10,” anasema Olang’i.

Advertisement