Serikali yaandaa kiama cha wakeketaji

Dk Faustine Ndugulile.

Muktasari:

  • Imebainika kuwa wahusika wa ukeketaji kila siku wanabuni mbinu mpya kuhakikisha wanaukwepa mkono wa Serikali

Dar es Salaam. Serikali imesema haitawafumbia macho watu watakaobainika kuhusika kwenye ndoa za utotoni na ukeketaji kwa sababu hali bado ni mbaya.

 

Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba,8 ,2018 na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Mtoto wa Kike.

 

"Mijadala inayoendelea nchi nzima itakuja na mbinu mbalimbali na sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha tunabaini kila mbinu inayopangwa na wakeketaji,’’amesema

 

Amesema licha ya takwimu za tafiti ya idadi ya watu na afya ya mwaka 2015/16 kuonyesha kuwa kiwango cha ukeketaji kwa watoto na wanawake katika umri wa miaka 15 hadi 49 kimepungua kutoka asilimia 18  ya mwaka 1996 hadi kufikia asilimia 10, ipo mikoa 10 inayoongoza kwa vitendo hivyo.

 

Amefafanua kuwa pamoja na kupungua kwa ukeketaji kwa kipindi cha miaka 10 hadi kufikia asilimia 10 kutoka asilimia 18, kuna mikoa bado inaongoza kwa vitendo hivyo ikiwamo Manyara wenye asilimia 58, Dodoma (47), Arusha ( 41), Mara (32), Singida ( 31) na Tanga asilimia 14.

Ameitaja mikoa mingine kuwa ni Kilimanjaro wenye asilimia 10, Morogoro ( 9), Iringa ( 8), Pwani ( 5 ) na Dar es Salaam asilimia 4.

"Serikali imamua hapana hatutaki mtoto wa kike hata mmoja akeketwe, kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki za binadamu na hakina tija"amesema Dk Ndugulile.

Dk Ndugulile amefafanua kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya wote watakaothibitika kujihusisha na ukeketaji.

 

Mbali na ukeketaji Dk Ndugulile amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni ndoa za utotoni imekuwa ni mojawapo ya matatizo makuu yanayokiuka haki za binadamu ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) limekadiria katika kipindi cha miaka 10 ijayo wasichana wapatao 100,000 wenye umri chini ya miaka 18 wanatarajia kuwa wameolewa kote duniani.

 

"Katika bara la Afrika asilimia 42 ya wasichana wote kuolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18, hii ni sawa na watoto wa kike 42 kati ya watoto 100 na haiwezi kufumbiwa macho, lazima hatua kali ziendelee kuchukuliwa kukabiliana na tatizo hili,"amesema Dk Ndugulile.

 

Dk Ndugulile amesema kwa mujibu wa tafiti kutoka ofisi ya taifa ya takwimu ipo mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ikiongozwa na Shinyanga yenye asilimia 59 na wa mwisho ni Iringa wenye asilimia nane.

 

Amesema changamoto hiyo ipo kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya vijijini ukilinganisha na maeneo ya mijini.

Kwa upande wa Naibu Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake (Tamwa) David Lumala amesema kuwa sheria bado kikwazo katika safari ya kupinga ndoa za utotoni na ukeketaji.

 

Amesema wadau na Serikali wajadili kwa kina na kupata majibu ya Sheria ya Ndoa kandamizi kwa mtoto wa kike ikiwamo inayoruhusu atolewe akiwa na miaka 14.

 

Amesema katika kukabiliana na hilo Tamwa ina miradi saba Tanzania Bara na mitatu Visiwani yenye lengo la kutoa elimu kwa jamii.

"Miradi hii inahusisha mijadala kwa jamii ya maeneo ambako unafanyika kutoa maoni na ushauri nini kifanyike.

 

"Lakini tatizo bado kubwa kwa jamii na wazazi, yupo mzazi mmoja alikubali  kupewa kipini cha kuvaa puani cha dhahabu kumaliza kesi ya binti yake kubakwa"amesema.

Amesema hiyo inaonyesha kwa kiasi gani wazazi nao wanahitaji elimu kukabiliana na hali hiyo