Serikali yasitisha Sh50 milioni kwa kila kijiji

Muktasari:

Makamu wa Rais akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma alisema wananchi hawatapelekewa fedha hizo na badala yake zitakwenda kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Uvinza. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema wananchi wasitegemee kupelekewa Sh50 milioni kila kijiji zilizoahidiwa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015.
Makamu wa Rais akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma alisema wananchi hawatapelekewa fedha hizo na badala yake zitakwenda kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kuliko kutoa fedha hizo kwa kila kijiji, Serikali imeamua kuwekeza katika elimu, afya, barabara pamoja na maji lengo likiwa ni kupeleka maendeleo kwa wananchi.

“Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujitegemea, lazima tujiwekee mikakati ya kuleta maendeleo katika nchi yetu, tumeanza kuwekeza katika masuala ya usafiri wa anga na nyie ni mashahidi mmeshuhudia tukinunua ndege zetu,” alisema Samia.
Alisema kujitegemea huko si kwa asilimia 100, wataomba msaada lakini ni kidogo kwasababu kuna changamoto au vipaumbele vya kitaifa na fedha itakayopatikana itashuka hadi kwa mwananchi wa chini.
“Tumeamua kujenga reli itakayokuwa inaenda haraka na kubeba mizigo, ikifanya kazi faida yake itamfikia hadi mwananchi wa chini.”
Alisema Serikali pia imeamua kuanzisha mradi wa umeme mkubwa utakaowaka nchi nzima bila kuzimika ambao utatumika hadi kwenye viwanda vitakavyojengwa na faida yake itawafikia pia wananchi wote.
“Fedha ambazo tumesema tutawapa katika kila kijiji tungeweza (kugawa) kwa kila mtu tusingeweza kuona faida yake, kwa hiyo sisemi tunaifuta ahadi yetu ipo kwenye ilani ya uchaguzi chama kimetuagiza na ni wajibu wetu Serikali kutekeleza, lakini katika kutafuta maendeleo kuna kupanga na kuchagua,” alisema Makamu wa Rais.

Alisema, “Katika mipango yetu ya sasa hilo la Sh50 milioni tumeliweka pembeni kwanza.”

Alisema wananchi wasikae na kudanganywa kwamba kuna fedha zinatoka serikalini, lakini zitaingizwa katika miradi muhimu.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, mkuu wa mkoa huo, Emmanuel Maganga alisema wananchi wa Kijiji cha Kazuramimba ni muhimu wakazingatia afya zao na lishe kwa watoto kwa kuwapa chakula bora.

Kauli hiyo ya Makamu wa Rais inahitimisha ahadi aliyoitoa Rais John Magufuli katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 alipoinadi Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, Ibara 57(d).
Ibara hiyo inasema, “Kutenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa kila kijiji kama Mfuko wa Mzunguko (Revolving Fund) kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa (Saccos) katika vijiji husika.”
Kifungu hicho cha 57, pamoja na hilo la Sh50 milioni kinaeleza kuwa Serikali ya CCM itahakikisha shughuli zote zenye mwelekeo wa ushirika zinapewa msukumo stahiki kwa kuhamasisha na kusimamia kwa nguvu uanzishaji wa vikundi vya ushirika kama vile Saccos na Vicoba.
Pia, inaendelea kueleza kuweka mfumo wa kuvitambua, kuvisajili na kuviwezesha vikundi vyote vyenye mwelekeo wa ushirika na ujasiriamali.
Katika mkutano wa Bunge la Bajeti lilipokuwa likijadili mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango Juni 4 na 5, wabunge walilibua na kuitaka Serikali iitekeleze la sivyo watakuwa na wakati mgumu mwakani katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Miongoni mwa wabunge waliozungumzia suala hilo bungeni alikuwa mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajabu aliyesema suala la Sh50 milioni kwa kila kijiji limeleta matatizo makubwa na kutaka Serikali kutoa majibu.
“Mwaka wa Fedha 2016/17 suala hilo lilitengewa Sh60 bilioni na katika mwaka wa fedha 2017/18 zilitengwa tena Sh60 bilioni lakini hadi sasa (Juni) hakuna hata senti moja iliyotolewa,” alisema Balozi Adadi.