Shamba lililodaiwa mali ya diwani larejeshwa kwa mjane

Wednesday August 14 2019

Zuhura Mohammed (mwenye nguo za kijani) akiwa

Zuhura Mohammed (mwenye nguo za kijani) akiwa na mwanaye na ndugu zake wakifurahia baada ya shamba walilokuwa wakigombea kuamuliwa kuwa ni mali yao. Picha na Haika Kimaro 

By Haika Kimaro,Mwananchi [email protected]

Mtwara. “Nilianza kukata tamaa baada ya kudhulumiwa shamba la urithi nililoachiwa na mume wangu baada ya kufariki, lakini binti yangu akanieleza mimi ni mama na mali tuliyodhulumiwa ni ya baba yao hivyo tuungane kudai haki yetu na leo 2019 tumeipata.”

Hayo ni maneno ya Zuhura Mohammed mkazi wa kijiji cha Kitangali wilayani Newala mkoani Mtwara nchini Tanzania baada ya mkuu wa mkoa huo, Gelasius Byakanwa kutangaza shamba linalokadiriwa kuwa na takribani ekari tisa kuwa mali yao na mkataba wa mauziano unaodaiwa kuwepo ni batili kwa kuwa ulifanyika nje ya lilipo shamba na hakukuwa na mashahidi.

Zuhura anasema mgogoro wa shamba hilo lililopo kijiji cha Chaume wilayani Tandahimba ulianza kusikilizwa kwenye baraza la ardhi la kata na kutolewa maamuzi kuwa ni mali yao lakini uamuzi huo ulibatilishwa na baraza la ardhi la wilaya.

Uamuzi huo umekuja baada ya aliyekuwa msimamizi wa mirathi kufariki na mmoja wa madiwani kudai ni mali yake aliyouziwa Sh2.7 milioni na mtu aliyefahamika kama Bakari Sefu pasipo mashahidi zaidi ya aliyekuwa mtendaji wa kijiji kutoka wilaya ya Newala ambaye kwa sasa ni mtendaji kata na wala hafahamu lilipo shamba hilo.

Akitoa uamuzi huo leo Jumatano Agusti 14,2019 Byakanwa amesema kutokana na ushauri uliotolewa na kamati shamba hilo ni mali ya Zuhura na wanaye na Ahmad Kulinga aliyekuwa ameteuliwa kusimamia mirathi ataendelea na majukumu yake kulingana na katiba.

“Hanafi Namtaka ameshindwa kuthibitisha umiliki wa shamba hilo, shahidi aliye naye ni mtendaji wa kijiji cha Majengo ambaye hata hajui shamba lilipo, wala hajui mipaka na aliyemuuzia kwa bahati mbaya ni marehemu na kwenye historia na uchunguzi hakuna palipothibitishwa Bakari Sefu aliwahi kulimiliki lile shamba,” amesema Bykanwa

Advertisement

Hata hivyo, amemzuia Hanafi Namaka au watu wake kuingia kwenye shamba hilo na kutaka uongozi wa wilaya ya Tandahimba kusimamia hilo na kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Newala kuchukua hatua za kiutendaji na kinidhamu dhidi ya mtendaji kata kwa kusimamia mauzo asiyoyajua uhalali wake.

Advertisement