Shule iliyoboronga mara mbili kidato cha IV yachunguzwa Dar

Muktasari:

  • Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas alisema jana kuwa kamati hiyo imeundwa kuchunguza chanzo cha shule hiyo na nyingine ya Furaha kufanya vibaya licha ya kuwapo mkakati maalumu wa kuhakikisha shule zote katika manispaa hiyo zinafanya vizuri.

Manispaa ya Ilala imewazuia waandishi wa habari kuitembelea Shule ya Sekondari Nyeburu iliyofanya vibaya miaka miwili mfululizo katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne kwa maelezo kuwa imeundwa kamati inayoendelea na uchunguzi.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas alisema jana kuwa kamati hiyo imeundwa kuchunguza chanzo cha shule hiyo na nyingine ya Furaha kufanya vibaya licha ya kuwapo mkakati maalumu wa kuhakikisha shule zote katika manispaa hiyo zinafanya vizuri.

Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana yaliyotangazwa wiki iliyopita na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), shule hizo mbili zimefanya vibaya, Nyeburu ikirejea katika kundi hilo sawa na mwaka 2016.

Elizabeth alisema manispaa kwa kushirikiana na mamlaka husika za elimu ilitoa mwongozo wa ufundishaji uliotilia mkazo masomo ya Kiingereza, Historia, Baiolojia, Kiswahili na Hisabati, huku masomo ya Sayansi yakisisitiziwa kuwa ya vitendo zaidi.

“Tuliwapa mbinu, ikiwamo kuwagawanya wanafunzi kulingana na uwezo wao ili iwe rahisi kuwasaidia, ndiyo maana tumeunda kamati kujua ni kwa nini shule hizo zimefanya vibaya kiasi hiki,” alisema.

Alisema, “Kulikuwa na maazimio maalumu ya kuinua ufaulu katika kikao cha ofisa elimu, wakuu wa shule na maofisa elimu kata, lazima wahojiwe kamati ijiridhishe sababu za kushindwa kufikia malengo.”

Alisema waliandaa semina elekezi kwa walimu za kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji.

“Tuliwapa walimu wa shule zote mwongozo wenye maazimio 19 ya utekelezaji ili kuhakikisha hakuna shule hata moja katika Manispaa ya Ilala inafanya vibaya, pia tulikuwa tukiwatembelea kukagua kazi zao na utendaji wa kila siku,” alisema.

Alisema kamati ikikamilisha kazi watajua walipokwama na kitu gani wanachotakiwa kufanya.

Mkurugenzi huyo msaidizi alisema baadhi ya maelekezo waliyopewa walimu awali ni kuwapo sanduku la maoni katika kila shule ili kuwatumia walimu na wanafunzi kupata taarifa, changamoto na kuzifanyia kazi. Mwongozo pia ulionya wakuu wa shule wasiwagawe walimu katika makundi, badala yake kuwafanya wawe wamoja ili wafanye kazi kwa pamoja na kubuni miradi ya shule ili isaidie matumizi madogomadogo shuleni.

Pia, wakuu wa shule walitakiwa kuunda kamati kusimamia usafiri wa wanafunzi na walimu kwa shule za pembezoni, wakihusisha bodi za shule katika kutoa uamuzi na kuzitaka zifanye kazi kama inavyotakiwa.

“Tuliwataka wakuu wa shule washirikiane na maofisa elimu kata, wazazi na jamii ili wafanye kazi kwa pamoja, kwa sababu kuna baadhi ya vitu vinavyokwamisha ilionekana vipo katika jamii inayowazunguka wanafunzi, ikiwamo familia,” alisema.

Kuhusu utoro wa wanafunzi alisema walitoa mwongozo kwamba watoro wa muda mrefu wasisajiliwe kufanya mitihani badala yake wazazi washauriwe kukariri kidato.