Mnyika: Spika amepepesa ripoti ya rushwa bungeni

Sunday November 11 2012

 

By Ibrahim Yamola

WAZIRI  Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika amesema anakusudia kukata rufaa  akitaka taarifa kamili juu ya tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge, iwasilishwe bungeni kwa sababu Spika Anne Makinda amekiuka taratibu katika uamuzi wake.

Mbali na hilo, atakata rufaa kupinga kiwango cha adhabu kilichotolewa na Spika  wa Bunge, Anne Makinda kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi kwa maelezo ni kidogo na inalishushia  heshima Bunge.

Hatua hiyo inatokana na Spika Makinda kutoa uamuzi  wa ripoti ya Ngwilizi bungeni juzi huku akiwasafisha wabunge waliotuhumiwa kwa rushwa na wakati huo akiwakaanga Profesa Muhongo na Katibu wake, Maswi.

Spika Makinda alisema tuhuma zilizotolewa dhidi ya wabunge hao zimethibitika kuwa ni za uongo.

Alisema kamati ndogo ya Bunge ya Haki, Kinga , Madaraka ya Bunge ambayo iliongozwa na Mbunge wa Malalo, (CCM), Hassan Ngwilizi ilifanya uchunguzi  wa kina kuhusu  tuhuma hizo na kugundua kuwa tuhuma hizo zilikuwa hazina uthibitisho.

Taarifa kwa umma aliyoitoa Mnyika jana ilisema Spika amefikia uamuzi wa moja kwa moja wa kutoa adhabu ya ‘onyo kali’ kinyume na masharti ya kanuni ya 5 (1).

“Taarifa kamili iwasilishwe na kujadiliwa bungeni ili ‘mbivu na mbichi’ zijulikane na masuala yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada na vyombo vingine vya nje ya Bunge yaendelee kwa hatua zaidi badala ya uamuzi huu wa funika kombe,” alisema Mnyika.

“Kuna masuala ya ziada ambayo binafsi niliyaeleza  mbele ya kamati ndogo chini ya kiapo ambayo sitakiwi kuyaeleza nje ya Bunge kwa mujibu wa kanuni na sheria… Hata hivyo taarifa kamili ikiingia bungeni kutakuwa na uhuru wa majadiliano kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba ya Nchi,” alisema.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo alisema Spika alifanya uamuzi chini ya Kanuni ya 5(1) na 72 (1) lakini hakuzingatia kanuni ya 72 (3) ambayo inaeleza iwapo mbunge ameshindwa kuthibitisha ukweli Spika ana mamlaka ya kumsimamisha mbunge huyo kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi vitano.

“Kwa kuzingatia rufaa huchukua muda kusikilizwa nilitaka niombe mwongozo wa Spika  kabla ya Mkutano wa Bunge kuahirishwa kwa kuwa katika uamuzi wake hakueleza hatima ya Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa,” alisema Mnyika.

Aliongeza: “Spika anapaswa bado kuueleza umma iwapo kamati hiyo inarejeshwa au inaundwa kamati nyingine."

Alisema ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kamati ni sahihi Maswi anapaswa kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Advertisement