Mawimbi, misukosuko Chadema kinapoelekea uchaguzi mkuu 2020

Viongozi wa Chadema wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam. Picha na Omar Fungo

Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 utaendelea kuishi katika mioyo ya wanamabadiliko ambao walikabidhi matumaini yao kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Uchaguzi huo ulijiandikia historia ya uhai wa chama hicho baada ya kupata asilimia 39.97 ya kura zote za urais chini ya Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa aliyegombea nafasi ya Urais baada ya kukihama chama chake cha CCM.

Lakini pia ndiyo uchaguzi ambao chama hicho kiliongeza uwakilishi ndani ya Bunge kwa zaidi ya wabunge 30 ikilinganishwa na 2010.

Wakizungumzia uimara wa chama hicho hivi karibuni, baadhi ya wataalamu na wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, uhai wa chama hicho umeonekana kuyumba kutokana na mazingira ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Wanataja baadhi ya viashiria vinavyofanya waone hali hiyo ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu Lowassa na Frederick Sumaye kurejea CCM sambamba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Pia wapo wabunge wanane kati ya 35 na madiwani zaidi ya 80 wa chama hicho ambao nao wamejiunga na CCM.

Lakini pia kitanzi cha zuio la siasa za kuuza sera majukwaani ikimaanisha mikutano ya hadhara.

Wabunge waliohamia CCM ni Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Chacha Marwa Ryoba (Serengeti), Godwin Mollel (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati), Joseph Mkundi (Ukerewe) na Cesil Mwambe (Ndanda). Pamoja na hali hiyo, bado viongozi waandamizi wa Chadema nao wanakabiliwa kesi kadhaa mahakamani.

Sasa wapo wanaojiuliza, wimbi na misukosuko hiyo itakuwa imedhoofisha Chadema ile ya mwaka 2015?

Profesa wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala bora ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari anasema viashiria hivyo vinaonyesha kukiathiri chama hicho katika uhai wake, japokuwa ni vigumu kutabiri kwa sasa nguvu yake itakuwaje Oktoba.

“Kwa sababu kilichofanya wafanikiwe Chadema siyo umadhubuti wa chama ila kuna wimbi la mabadiliko lililokikumba hata baadhi ya vigogo wa CCM ambao walihamia upinzani.

“Lakini pia kulikuwa na wimbi la Ukawa ambalo lilikuwa limekubalika sana, hata mwaka 1995 ilikuwa ni wimbi kwa upinzani,” anasema Profesa huyo.

Hivyo, anasema upo uwezekano mkubwa kwa chama hicho kudhoofishwa kwa namna moja ama nyingine kama hakitatafuta mbinu mbadala.

“Ila tukumbuke uchaguzi ni uchaguzi tu, tunaweza fikiri hivi lakini kikaja kufanya vizuri kwa sababu bado kuna watu wanaotaka mabadiliko, kwa miezi iliyobakia lolote linaweza kutokea.”

Naye Dk Muhidini Shangwe wa Idara hiyo hiyo kutoka UDSM anakubaliana na mtazamo wa Profesa Bakari akifafanua nadharia yake kuhusu ukimya wa vyama majukwaani unaweza kutengeneza matamanio makubwa ya kusikika kwa Watanzania kuliko sauti zilizozoeleka kwa sasa majukwaani.

“Wapo wananchi ambao wanatamani kusikia jambo gani Chadema watazungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuruhusiwa kufanya siasa majukwaani,” anasema.

Pamoja na fursa hiyo kwa upinzani, Dk Shangwe anatazama siasa za Tanzania zimejengwa katika uwezo wa mwanasiasa mmoja mmoja zaidi kuliko chama. “Kwa hiyo nina shaka, Chadema ya mwaka 2015 huenda isitokee tena mwaka huu labda utokee mpasuko CCM.”

Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema pamoja na changamoto hizo, Chadema haijaathiri uhai wake na badala yake imeendelea kujiimarisha.

“Lowassa aliingia na mafuriko ya vigogo Chadema, lakini hakuondoka nao wote kurudi CCM, Sumaye alikuja na kuondoka peke yake, Dk Mashinji ameondoka mwenyewe, sasa unapimaje athari zao?

Pili, Mrema anasema kwa mara ya kwanza Chama hicho kilifanikiwa kusimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa zaidi ya asilimia 80 licha ya figisu zilizofanyika na kuamua kujitoa.

“Jambo la tatu ni kwamba licha ya kuzuiliwa kufanya mikutano ya kisiasa, Chadema tumetekeleza program ya Chadema ni msingi kwa asilimia 100, kwa sasa tuna kiongozi wa chama kila kijiji Tanzania Bara, tunajua wako wapi, namba zao na majina yao, kwa hiyo wapo wanaoondoka na wapo wanaoingia kujenga uhai wa chama, uchaguzi ujao tutakuwa vizuri sana,” anasema Mrema.

Kada wa Chadema aliyejiunga na NCCR Mageuzi, Wakili Boniface Mwabukusi anasema mahitaji ya vyama vya upinzani hayapo katika matakwa ya vyama au viongozi wake ila ni mahitaji ya wananchi.

Lakini Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu anasema mwanachama kuondoka ni jambo la kawaida huku akikiri kuwapo kwa shida ndani ya chama hicho licha ya kutoweka wazi.

“Kushindwa Chadema ni kawaida kwa sababu vyama siyo mama yetu, lakini vyama vitaendelea kuwepo, vyama ni mali ya wanachama, wanachama ni roho ya vyama, Niwaambie watu wa Moshi, kama Chadema kutanishinda, nguvu zangu nitazipeleka kwingine kuimarisha upinzani zaidi.”
“Kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika 2015, aliondoka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk, Wilbrod Slaa lakini Chadema ikaimarika zaidi, kwa hiyo kuondoka kwa baadhi ya watu hakuwezi kukiyumbisha chama,” anasema Mrema. Tayari uongozi wa Chadema umetoa tamko la kuwataka wanaotaka kuondoka kwa sasa wafanye hivyo huku kikijipanga kuandaa mchujo wa wagombea watakaosimama kupeperusha bendera ya chama.

Kati ya mwaka 2015 hadi Februari mwaka huu, chama hicho kimepoteza majimbo 12.

Kuhusu mazingira hayo, Mrema anakiri kwamba imekuwa changamoto na doa kwa chama na wapiga kura waliokatishwa tamaa na wanaohamia CCM.

“Lakini tumejipanga kuwa na mchujo, wagombea wote watakaojitokeza tutawaweka katika program maalumu ya mafunzo. Baada ya mafunzo hayo, kutakuwa na mchujo chini ya Kamati Kuu ya chama kupitia kanuni za uteuzi za mwaka 2015, zitakazoboreshwa kwa kuzingatia sifa za mgombea, vigezo na masharti yatakayowekwa.”

Pamoja na tathmini ya wadadisi katika duru za kisiasa, mbinu za chama hicho zikilinganishwa na changamoto zilizojitokeza, wanajiuliza je kitarejea katika ushindani kama ilivyokuwa mwaka 2015?
 Tutafakari kwa pamoja.