Muswada wa vyama vya siasa umekwaza wengi kwa mengi – 3

Nilieleza katika makala zilizotangulia kuwa ukiacha kasoro za kimchakato, maudhui ya muswada wa sheria ya vyama vya siasa yalikuwa na shida kiasi cha kusononesha tulio wengi.

Mambo mawili ya utangulizi niliyoyagusa – kukosekana sehemu mahsusi mwanzoni mwa muswada inayoweka nia, lengo na madhumuni ya kutungwa kwa sheria hiyo wakati huu.

Aidha, kukosekana kwa vifungu vinavyolinda usawa wa kijinsia pamoja na ushiriki madhubuti wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika siasa za Tanzania ni upungufu mkubwa wa sheria hiyo mpya.

Pia, kuna suala la tafsiri ya chama cha siasa na vyombo vyake mbalimbali. Hapa, kulikuwa na makosa makubwa ya maana ya maneno yaliyotumika. Kwa mfano, muswada unatamka katika kifungu cha 2 kuwa mkutano mkuu wa chama cha Siasa utakuwa ndicho kikao au chombo kikuu cha utawala.

Hata kwa tafsiri ya mtaani, mkutano mkuu wa chama si chombo cha kiutawala, ni chombo au kikao kikuu cha maamuzi ya chama.

Imenifariji sana kuwa katika nakala ya mwisho iliyopitishwa na Bunge, kuhusu kifungu hiki maoni ya wadau yameingizwa na sasa muswada unatambua mkutano mkuu kama chombo kikuu cha maamuzi, si utawala. Hapa ndipo unaweza kuona umuhimu wa maoni ya wadau katika mchakato wa utungaji sheria.

Jingine lililokuwa na kasoro kubwa katika muswada ni kuhusu elimu ya uraia kwa vyama vya siasa. Hapa niseme palinishangaza na kunikwaza sana. Kwa ujumla, nchi yetu ina tatizo la kukosekana kwa elimu ya uraia kwa jamii na vyama vya siasa. Mambo mengi yanafanywa na vyama isivyo kutokana na kukosekana uelewa ndani ya vyama kuhusu masuala hayo. Kwa mfano, chama cha Siasa ni nini na kinapaswa kuwa na majukumu gani? Je, wakati usio wa uchaguzi, vyama vinaweza kufanya majukumu gani ya kujenga nchi? Je, uongozi wa chama unapaswa kupangwa vipi?

Au chama kinawezaje kuendeshwa kiubunifu na kimkakati katika mazingira ya uchumi duni kama wa Afrika au Tanzania? Haya na mengine mengi ni mambo muhimu yanayoweza kuwamo katika elimu ya uraia inayopaswa kutolewa kwa vyama vya siasa. Badala ya muswada kuhamasisha wadau kuandaa na kutoa elimu ya uraia kwa vyama vya siasa, imeduwaza wengi kwa kuweka ‘figisufigisu’ kwenye eneo la elimu ya uraia. Kuanzia kifungu cha 3 (5) (g) mpaka kifungu cha 5 (5B) (2), kinaweka masharti magumu ya mazingira ya wadau kutoa elimu hiyo.

Pia, msajili wa vyama vya siasa anapewa mamlaka ya kudhibiti elimu yoyote inayotolewa kwa vyama vya siasa. Katika hili, mtu au kikundi au taasisi au shirika lolote linalotaka kufanya mkutano, mafunzo, semina, uchambuzi, kongamano, warsha au shughuli yoyote inayohusisha chama au vyama vya siasa ni lazima amwandikie msajili kumpa taarifa huku akimpelekea nyaraka, vitini na makabrasha yote ya maudhui ya shughuli husika ili akavikague kuona kama vinafaa kutumika kufundishia au kuwezeshea elimu ya uraia.

Bila kusema msajili atapaswa kuchukua muda gani tangu kupokea vitini hadi kujibu, muswada unaweka mazingira ambapo mdau hawezi kuendelea na chochote mpaka apate idhini ya msajili.

Kwa maoni yangu, huu ni ukiritimba wa hali ya juu na unaweza kuchelewesha au kuzuia kabisa utoaji wa elimu ya uraia na kukwaza shughuli mbalimbali zinazopaswa kufanywa na wadau wa demokrasia kwa vyama vya siasa.

Hivi msajili ataweza kushughulikia maombi na makabrasha yote yanayopendekeza shughuli na vyama vya siasa? Je, endapo chama kimemwalika mtaalamu kama mimi kuwezesha uchambuzi wa muswada fulani wa sheria au sera siku kadhaa kabla ya kusomwa bungeni, inawezekanaje kusubiri mpaka msajili atoe ruhusa? Kwa muswada huu, naiona Tanzania ikirudi enzi za ujima.

Pili, Msajili anaweza kuzuia kufanyika kwa shughuli iliyopangwa na vyama mpaka apate ufafanuzi wa jambo fulani kuhusu maudhui ya vitini vya kufundishia. Tunataka udhibiti wa ngazi ya shule ya chekechea kama huu, nimesononeka sana.

Kwa upande mwingine, naelewa kuwa nia ya vifungu hivi inaweza kuwa ililenga kuikinga nchi na mafundisho mabaya kama ya vikundi vya ugaidi na uharamia vinavyoweza kulenga kuharibu amani ya nchi.

Hata hivyo, kwa mwalimu na mtaalamu wa masuala ya ujenzi wa demokrasia, naona dhahiri kuwa kulikosekana ubunifu katika timu ya waandishi wa muswada kuhusu namna ya kudhibiti elimu mbaya kwa vyama.

Moja ya taasisi hizo ni Idara ya Usalama wa Taifa. Kwingineko, yapo mabaraza yanayodhibiti maudhui yenye kukinzana na utamaduni, mila na desturi zetu na mengineyo. Hatuwezi kuwa na sheria ya kibaguzi ambayo inalenga kudhibiti elimu ya uraia au programu za kuhamasisha kundi moja tu la vyama vya siasa na kuacha makundi mengine.

Kama msajili anadhibiti elimu inayotolewa kwa vyama, nani anadhibiti elimu inayotolewa kwa wakulima, wavuvi, wachimbaji madini, wajasiriamali na wauza senene?

Mengineyo yenye ukakasi katika muswada huu ni pamoja na msajili kutawazwa kuwa ndiye mwezeshaji wa mawasiliano yote kati ya vyama na serikali. Msajili kuwa mshauri mkuu wa serikali kuhusu masuala ya vyama na demokrasia kana kwamba hakuna wadau wengine anaoweza kuwashauri.

Uwezo na mamlaka ya msajili kuviadhibu vyama au wadau wa demokrasia ya vyama bila kusubiri mahakama na mambo mengine kadhaa nitayajadili kwa kina katika safu hii siku zijazo.

Lengo ni kumwomba Rais afikirie kutosaini muswada huu mpaka ufanyiwe marekebisho kwa kuwa fursa na uwezo huo anao kikatiba.

Deus Kibamba ni mtafiti, mchambuzi na mhadhiri katika masuala ya siasa, uchumi na uhusiano wa Kimataifa. Ameshiriki mazungumzo ya hali ya baadaye ya Sudani. Simu: 0788 758581; email: [email protected]