Mvutano wa Uhuru, Ruto wakolezwa na vita ya ufisadi

Muktasari:

  • Kuna mpasuko mkubwa unaoendelea kati ya Rais Kenyatta na Makamu wake ukienda sambasamba na kashfa ya ufisadi iliyoibuliwa hivi karibuni.

Nchini Kenya kuna zozo unaendelea, unaoweza kuhitimisha uswahiba wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais, William Ruto.

Mpasuko ulianza kuchipuka mapema, lakini ukawa bayana Julai 22 baada ya kukamatwa kwa Waziri wa Fedha, Henry Rotich kwa tuhuma za rushwa na ufisadi.

Rotich aliyekanusha kosa hilo aliachiliwa kwa dhamana siku iliyofuata. Aliteuliwa na Rais kushika wadhifa huo tangu mwaka 2013 kwa ombi la Ruto.

Ruto hakufunua mdomo wake kufuatia kukamatwa kwa Rotich ambaye ni nguzo ya ngome yake katika Mkoa wa Rift Valley.

Wakati huohuo, mzozo mwingine wa kisiasa unatishia kuongeza mpasuko kati ya viongozi hao wakuu wa mrengo wa kulia wa chama cha Jubilee.

Agosti 9, kikosi kazi za Building Bridges Initiative (BBI) kiliitisha mkutano wa kusikiliza maoni kufuatia maombi ya kurekebisha Katiba. Kikosi hicho kinatarajiwa kukabidhi ripoti yake kwa Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga hivi karibuni.

Kambi ya Ruto haijawahi kuficha hisia zake kwa BBI, ikiwa ni matokeo ya muungano uliofikiwa Machi 2018 kati ya Rais Kenyatta na Odinga ambaye ni mpinzani wa muda mrefu. Mkakati huo ulifanyika kwa kushikana mikono kwa viongozi hao, jambo linalopata umaarufu kama ‘handshake (kushikana mikono).

Wafuasi wa Ruto wana hofu kuwepo kwa dalili za Rais Kenyatta kuvunja ahadi ya kushirikiana madaraka, ambayo ililenga kumsaidia Ruto kugombea urais mwaka 2022, baada ya kipindi chake kumalizika.

Marekebisho yoyote ya Katiba yatakayopendekezwa na BBI yatasababisha kura ya maoni ambayo kwa itapelekea uhusiano kati ya Kenyatta na Ruto kuvunjika na kuanzisha vuguvugu la upinzani.

Kama hiyo itatokea, siku za umakamu wa rais wa Ruto zitakuwa zinahesabika.

Migawanyiko hiyo inakuja wakati tayari kukiwa na mipasuko ndani ya chama cha Jubilee. Wanasiasa ndani ya chama hivyo wako mbali na muungano, kufuatia mkakati wa vita ya rushwa unaoendeshwa na Rais Kenyatta ambao kambi ya Ruto inadhani inalengwa.

Rotich na watendaji wengine wa juu karibu 20 wa Hazina na idara nyingine walikamatwa baada ya kufanyika kwa uchunguzi uliowahusisha na kupotea kwa Sh21 bilioni za Kenya (Dola 203 milioni) katika mradi hewa wa uchimbaji wa bwawa.

Upande wa Ruto unasema wamekuwa wakilengwa isivyo halali na kashfa za rushwa, wakigusia pia tukio la kukamatwa kwa gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu Julai 28.

Mwanasiasa mwingine ambaye ni mbunge, Ndindi Nyoro amehusisha kukamatwa kwake kwa tuhuma za rushwa kuwa amekuwa akilengwa kwa sababu anamuunga mkono mpango wa Ruto kugombea urais mwaka 2022.

Mara nyingi Ruto amekuwa akikwepa kujihusisha na kampeni za kupinga rushwa, ya inaonekana ndiyo mkakati wa sasa wa Kenyatta atakaouacha kwa wafuasi wake.

Hata hivyo, uchunguzi kwenye mabwawa ya Arror and Kimwarer imegusa vita mpya. Februari mwaka huu, polisi walipomhoji Rotich, Ruto alipinga hadharani akisema hakuna fedha zilizopotea.

Akizungumza na Jukwaa la viongozi wa wafugaji, Ruto aliufananisha uchunguzi huo kama mkakati wa uovu wa kuvuruga ngome yake katika Mkoa wa Rift Valley na kwa kuongezea alielezea shida ya kukosekana kwa maji kwa wafugaji wa kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa Kenya kama rasilimali muhimu. Wafuasi wa Ruto katika Mkoa wa Rift Valley wanaonekana wamevurugwa.

“Hakutakuwa na tatizo lolote katika Mkoa wa Rift Valley. Watu wameshaliona hilo na kumekuwa na mapatano. Wala hata kugawanyika kwa Uhuru na Ruto kunaweza kuvunja uhusiano huu,” alisema Seneta Aaron Cheruiyot anayemuunga mkono Ruto.

Cheruiyot aliongeza kuwa mashtaka yanayomkabili Rotich yamethibitisha anayosema Ruto kwa muda mrefu; “Serikali haijapoteza Sh21 bilioni (za Kenya). Suala litakuwa ni endapo mchakato wa ununuzi ulifuata taratibu.

“Msimamo wa Ruto unatokana na kile kinachoonekana kama vita ya upendeleo katika rushwa. Kama ukitumia akili kwa kesi za watu wakubwa zimekuwa zikilenga kuwaondoa madarakani na wala siyo rushwa.” Si upande tu wa Ruto, kuna mpasuko pia katika ngome ya Rais Kenyatta.

Chama chake cha zamani TNA kimegawanyika kati ya wanaomuunga mkono Ruto wakiwa na brigedi inayoitwa “Tangatanga” na kundi linalomuunga mkono Kenyatta likijulikana kwa jina la “Kieleweke”.

Wakati huohuo, kundi la Odinga la mrengo wa kushoto la chama cha Orange Democratic Movement (ODM) linamtetea Kenyatta kila anapotuhumiwa na upande wa Ruto.

Kwa ufupi, Odinga amekuwa ngao ya Kenyatta akionekana kuongoza upinzani bandia ndani ya Jubilee.

Wakati Ruto akikabiliana na majaribu na kuruka vikwazo vya migogoro, kuhusu masaibu yaliyompata Rotich, mmoja wa wafuasi wake ambaye ni kiongozi wa maseneta, Kipchumba Murkomen amekuwa wakili wa Rotich.

Ameahidi kumpambania Rotich mahakamani na uraiani.

Alipotafutwa na waandishi wa habari, hasimu wa kambi ya Ruto ambaye pia ni mbunge, Ngunjiri Wambugu aliwataka wakasome ujumbe wake kwenye mtandao wa Facebook ambao aliandika, “Hivi Makamu wa Rais Ruto anafikiri Wakenya ni wajinga?”

Alimshutumu Ruto kwa kuwashawishi baadhi ya wabunge kumuunga mkono katika mikutano ya hadhara nchini humo akikiuka agizo la Rais la kuzia kuanza kampeni mapema.

“Ruto anafikiri kuwa yeye ndiyo ana akili sana na kwamba Wakenya akiwemo mkuu wake ni wapumbavu,” anaongeza, akimshutumu Ruto kwa kujifanya kumuunga mkono Rais Kenyatta hadharani.

Swali kubwa nchini Kenya si lingine, bali ni pale Kenyatta na Ruto watakapotengana hadharani.