Ruto ataweza kuruka kihunzi cha Daniel Moi?

Ikiwa imebaki miaka miwili kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya, makamu wa rais, Dk William Ruto ameanza mbio za kutaka kumrithi rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.

Wapo wanaompinga kuwa katika mbio hizo anatumia uwezo wake wa kifedha, matamshi yake na kuhusisha kauli aliyoitoa hivi karibuni kwamba hana deni la kisiasa na jamii au mtu yeyote isipokuwa kutumikia Wakenya, kujihalalisha kwa wananchi.

Wakati mengi yakizungumzwa, wachambuzi waliozungumza na Mwananchi wamesema Ruto ana nafasi ya kurithi kiti hicho, wakati wengine wanasema itakuwa vigumu kwake kwa kuwa siasa anazozifanya zinatafsiriwa kuwa zinaegemea upande mmoja.

Baadhi wanasema anaweza kupenya licha ya ukweli kwamba atakumbana na upinzani mkali.

Kiongozi huyo ambaye alimuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2017 kwa matumaini kwamba atapokea kijiti baada ya kipindi chake kumalizika, ameshaonyesha nia ya kutaka nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini Kenya.

Hata hivyo, suala hilo huenda lisitimie na badala yake nafasi hiyo ikachukuliwa na mtu mwingine tofauti na matamanio yake.

Washirika wake wa kisiasa wanaamini kuwa kiongozi huyo anapigwa vita na kwamba miongoni mwa mbinu zinazotumiwa ni kutumia muafaka wa Rais Kenyatta na kinara wa upinzani wa nchi hiyo, Raila Odinga kuunganisha familia za viongozi wenye ushawishi.

Wadadisi pia wanasema muafaka huo ulikuwa ni mbinu ya kuunganisha familia za viongozi hao maarufu zenye uwezo wa kifedha kama njia moja ya kumzima Ruto katika kampeni za urais za 2022.

Wakati kiongozi huyo akijiandaa kwa uchaguzi ujao, inaelezwa kuwa familia za Odinga, Kenyatta na Moi zinaweza kuungana kumdhalilisha.

“Kuungana kwa familia hizo kumpinga Ruto kunaweza kuwa pigo kubwa kwake,” anasema mchambuzi wa siasa, Godfrey Sang.

Huo ni mwendelezo tu wa ugumu ambao kiongozi huyo amekuwa akikutana nao katika safari yake ya kuwania urais.

Mapema wiki hii, Ruto alifichua uhusiano wake na aliyekuwa mlezi wake kisiasa, hayati Daniel arap Moi, rais wa zamani wa Kenya, ulivyovurugika mara tu alipotangaza nia yake ya kugombea urais.

Dk Ruto anasema uhusiano wake na Moi ulianza kuwa mbaya baada ya kutangaza azma yake.

“Tulikuwa na mkutano mjini Eldama Ravine ambako nilitangaza azma yangu ya kuwania urais. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mafarakano yetu,” alisema Ruto.

Kuanzia wakati huo, Moi ambaye alizikwa kijijini kwake Kabarak Jumatano iliyopita, aliacha kumchangamkia kama awali na hata kumdhalilisha hadharani.

Makamu huyo wa rais alisema hakuchukulia tukio hilo kwa uzito hadi alipofungiwa nje ya mlango wa Moi akiwa na wabunge wengine 15 walioenda kumtembelea.

Ruto anasema walinzi waliwaarifu kwamba kiongozi huyo hakutaka kukutana na mtu yeyote kwa wakati huo.

Anasema hapo ndipo alipogundua kwamba mtu aliyemtazama kama kielelezo chake kisiasa, alikuwa na mawazo tofauti na yake.

“Alitamka maneno ya kudhalilisha mno, akipuuza azma yangu na kusema nilikuwa ninapotosha jamii. Moi alijitokeza na kusema Ruto hawezi kuwa kiongozi, mnapaswa kuchagua watu wenye ujuzi kama Henry Kosgei na Nicholas Biwott,” alisema Dk Ruto.

Licha ya ‘laana’ hiyo, bado Ruto ameendelea na ndoto yake ya kuwa rais.

Ingawa Ruto haelezi mwaka gani hasa alipokatazwa na Moi, lakini ukweli ni kwamba imepita miongo kadhaa sasa. Swali ni je, ameamua kupuuza ushauri huo? Na je, atavuka kiunzi hicho ambacho wachambuzi wa wanafananisha na laana.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo anasema Ruto bado ana nafasi kubwa ya kushinda urais wa Kenya licha ya kukataliwa na kiongozi huyo.

Shoo anasema wakati Moi anatoka madarakani, hakuwa na uhusiano mzuri na Wakenya na wengi walifurahi na kunywa pombe siku alipotangaza azma yake ya kupumzika.

“Naweza kusema maneno yake dhidi ya Ruto hayakuwa na nguvu kwa sababu hakupendwa sana na Wakenya,” anasema.

“Lakini ukweli utabaki palepale kuwa Ruto bado ana nafasi kubwa ya kuwa rais wa Kenya katika uchaguzi ujao kwa sababu ya umri wake kuwa bado mdogo tofauti na Odinga, na sidhani kama Wakenya watamkubali tena (Odinga) kwa sababu amegombea sana.

“Kenya ina vijana wengi ambao ni wapigakura wenye uchungu na nchi yao kutokana na masuala mbalimbali wanayoyapitia, kama changamoto za ajira. Ruto kwa sababu ni kijana, ana uwezo mkubwa wa kuliteka kundi hili.”

Anasema jambo jingine linalompa nafasi kubwa Ruto ni Mpango wa Maridhiano (BBI) wenye lengo la kuijenga Kenya bila mgawanyiko wa kisiasa, ukabila na matabaka.

Anasema sababu nyingine ni hali ya ukabila kubadilika. Awali Wakikuyu na Wajaluo walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kugombea na kushinda urais tofauti na kabila la Wakalenjii ambalo Ruto anatoka.

“BBI ni mpango mzuri kwa sababu umelenga kuondoa ukabila, hapa Ruto atapata faida kubwa kwa sababu hakutakuwa na ukabila,” anasema.

Hata kabila lake la Kalenjin litakubalika na kumbuka kuwa Ruto ni makamu wa rais, kwa hiyo bado ana nguvu na ushawishi katika mchakato huu,” anasema.

Hata hivyo, Profesa Macharia Munene wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani (USIU), anasema baadhi ya matatizo ya Ruto ni ya kujitakia.

“Na mengine yamebuniwa dhidi yake. Hiyo ni kawaida katika siasa na kwa kuwa ni mwanasiasa mweledi anajua hayo yote,” anasema Profesa Munene.

Profesa Munene anasema baadhi ya maadui wa Ruto wanatoka ngome yake.

“Ingekuwa ajabu kama asingekuwa na maadui kutoka ngome yake na maeneo yote nchini,” anasema.

Kwa upande wake, seneta wa Nandi, Kiprotich Cherargei anasema kuna watu wanaotumia jina la Rais Kenyatta na Moi kupanga njama za kumzima Ruto.

Wanaopanga kuzamisha azma yake wanapanga kuzua taharuki ili kusambaratisha chama cha Jubilee ambacho anapaswa kukitumia kugombea urais kwa mwaka 2022.

Hata hivyo, Sang anasema itakuwa vigumu kwa Ruto kuiacha Jubilee wakati huu na kwa kuwa bado ana nafasi ya kuwania kiti hicho na kushinda.