Simbachawene ametuma ujumbe mkubwa kurejeshwa Baraza la Mawaziri

George Simbachawene

Septemba 7, 2017, siku ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipatwa na tetemeko la nafsi kufuatia aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupigwa risasi ndani ya nyumba za viongozi alikokuwa anaishi, ni siku pia Ikulu kulikuwa na tukio kubwa.

Ripoti mbili za kamati teule za Bunge, zilizoundwa maalumu kwa ajili ya kuchunguza shughuli za uchimbaji, biashara, usimamizi na udhibiti wa madini ya tanzanite na almasi zilisomwa Ikulu, mbele ya Rais John Magufuli.

Baada ya kusomwa kwa ripoti hizo, George Simbachawene, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, alijiuzulu. Simbachawene aliguswa na ripoti hizo kuwa hakutimiza wajibu wake alipokuwa waziri wa Nishati na Madini katika mwaka wa mwisho wa utawala wa awamu ya nne.

Julai 21, mwaka huu, Simbachawene, aliteuliwa tena na Rais Magufuli kushika wadhifa wa waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Ikiwa ni mwaka mmoja, miezi 10 na siku 14 tangu alipojiuzulu uwaziri wa Tamisemi.

Kwa kuweka kumbukumbu sawa, si kwamba Simbachawene alijiuzulu kwa matakwa yake, alitii agizo la Rais Magufuli aliyetaka wote waliokutwa na madoa katika ripoti za Bunge zilizosomwa Ikulu, wajiuzulu na wachunguzwe.

Ukiwa umebaki mwezi mmoja na siku 17 kutimia miaka miwili tangu Simbachawene aondoke Baraza la Mawaziri, imempendeza Rais Magufuli kumrejesha tena barazani. Hapa ndipo ujumbe ulipo.

Vyeo vya kisiasa vina nyakati za kuchanua na kusinyaa. Kuna wakati wanasiasa huteleza na kuanguka. Walio na dira huwa hawatetereki. Wakati unapofika huchanua tena. Septemba 7, 2017 c heo cha Simbachawene kilisinyaa, Julai 21, mwaka huu, kimechanua upya!

Miaka ya 1970, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Shinyanga, Michael Mabawa alitumia askari, kufanya operesheni ya kusaka wachawi. Wananchi wasio na hatia walipigwa na kudhalilishwa kwa tuhuma za kujihusisha na ushirikina.

Kwa kitendo hicho, Ali Hassan Mwinyi, akiwa waziri wa Mambo ya Ndani, alimwandikia barua ya kujiuzulu, Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, kwa sababu polisi ambao walikuwa chini ya wizara aliyoiongoza, walipiga na kutesa raia.

Mwaka 1984, kikao cha Halmashauri Kuu CCM kilimvua urais wa Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe na kikampitisha Mwinyi kuwa Rais wa visiwa hivyo. Mwaka mmopja baadaye, 1985, Mwinyi akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akamrithi Mwalimu Nyerere.

Mwinyi ‘Mzee Ruksa’ alipojiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani kwa makosa ya Polisi wa Shinyanga kilikuwa kipindi chake cha kusinyaa, mwaka 1984 alichanua upya kisha kustawi zaidi mwaka 1985.

Sasa basi, Mwinyi ni alama yenye kutoa hamasa kwa viongozi hasa vijana, kutambua kuwa zipo nyakati za kuteleza na kuanguka, lakini muhimu ni kujikusanya, kunyanyuka na kuendelea na mwendo.

Simbachawene amerejea somo hilo la Mzee Ruksa. Kwamba vyeo vya kisiasa havifanani na vile vya koo za kifalme, bali wakati mwingine upepo huvuma vizuri, hutokea pia ukakuvumia vibaya. Uwe tayari.

Nchini Malaysia, Mahathir bin Mohamad, alipokuwa mbunge na mwanachama hai wa chama tawala cha United Malays National Organization (UMNO), alipaza sauti kupinga ushirikiano wa nchi yake na China, kwamba uliwaumiza kuliko kuwafaidisha kama Taifa.

Chini ya utawala wa Waziri Mkuu, Abdul Rahman, Mahathir alifukuzwa kwenye chama cha UMNO na kutimuliwa ubunge. Hiyo ilikuwa mwaka 1964.

Mahathir alivumilia miaka sita tu, kwani mwaka 1970, Abdul Rahman alilazimishwa kujiuzulu uwaziri mkuu, vilevile urais wa UMNO. Ni hapo Mahathir alirejeshwa kwenye chama, akarejeshewa ubunge wake kisha akateuliwa uwaziri.

Mwaka 1976 Mahathir akawa naibu waziri mkuu na mwaka 1981 alichaguliwa na chama chake kuwa waziri mkuu wa Malaysia, kwa maana ya Mkuu wa Serikali. Mahathir aliiongoza Malaysia mpaka mwaka 2003.

Mahathir ndiye waziri mkuu wa Malaysia aliyedumu madarakani kwa muda mrefu kuliko yeyote. Hivyo, mwaka 1964 alipovuliwa ubunge na kufukuzwa uanachama wa UMNO, Mahathir alisinyaa, mwaka 1970 alianza kustawi upya.

Septemba 2016, miaka 13 tangu alipoondoka madarakani, Mahathir alijitenga na chama tawala cha UMNO ambacho kinaunda muungano wa Barisan Nasional, alichokuwa mwanachama wake tangu mwaka 1946 na kuanzisha chama cha Malaysian United Indigenous, kilichojiunga na muungano wa Pakatan Harapan.

Katika Uchaguzi Mkuu Malaysia Mei, mwaka jana, Mahathir aliuongoza muungano wa Pakatan Harapan (PH) kushinda viti vingi vya ubunge, hivyo kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa waziri mkuu, akiwa na miaka 93 kasoro miezi miwili kamili. Kwa sasa Mahathir ana miaka 94. Anaendelea kuongoza.

Mifano ya Simbachawene, Mwinyi na Mahathir kwa uchache, inafundisha unyenyekevu katika jukwaa la siasa. Ajali zipo nyingi. Wakati wowote upepo ukikuvumia vibaya, unaweza kujikuta unaichukia siasa. Ukifika wakati huo tulia. Vuta subira, zinaweza kuja nyakati nyingine ukastawi, pia uwe na akiba, unaweza kusinyaa, ukastawi na kusinyaa tena.

Tangu alipojiuzulu, Simbachawene alibaki mkimya, akijielekeza kwenye shughuli zake za ubunge. Pengine ni kwa utulivu wake, au kwa kuona tuhuma zilizotajwa na kamati za Bunge zilikuwa hazimgusi moja kwa moja, ndio maana Rais Magufuli ameona amrejeshe ofisini.

Ni elimu kuwa ukiteuliwa na Rais kufanya kazi ya nchi chapa kazi, ukiondolewa isiwe nongwa, usimalize makaratasi kunung’unika au kujaza mafumbo katika mitandao ya kijamii. Vuta subira. Muda wako ukifika unaweza kung’ara upya.

Aprili mwaka huu, mbunge wa Bumbuli, January Makamba, alipokuwa waziri wa nNchi, Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, alisema kuwa uongozi wa wananchi ni sawa na koti la kuazima, wakati wowote unapovaa lazima ujiandae kuwa bila koti pale mwenye nalo anapolihitaji.