Tanzania bado tunao maadui walioshindikana tangu tupate uhuru

Mapema tu baada ya uhuru, Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere alitangaza maadui watatu wakubwa wa Taifa kuwa ni ujinga, umasikini na maradhi.

Ili kupambana na maadui hao, Nyerere aliweka msisitizo mkubwa katika elimu kwa watoto na elimu ya watu wazima akinuia japo wajue kusoma, kuandika na kuhesabu na alifanikiwa.

Mwalimu pia katika maandiko yake amewahi kutaja vitu vinavyohitajika ili kuleta maendeleo kuwa pamoja na watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Leo karibu miaka 60 tangu Tanzania ipate uhuru wake, haishangazi kuona bado maadui wale watatu wametamalaki nchini.

Mathalan, tukio hili la wakazi wa Morogoro kukimbilia lori la mafuta lililopinduka na kuchota mafuta ni kielelezo cha ujinga na umasikini miongoni mwa Watanzania.

Endapo wangekuwa werevu, wangejua mafuta ya petroli ni hatari, si ya kukimbilia asilani. Kama wangekuwa wanajitosheleza, wasingekwenda kuchota mafuta waliyomwagika ili kupata kipato cha haraka.

Wakati tukisikitika kuwapoteza Watanzania zaidi ya 95 kwa ajali ya moto huku wengine wakiugulia majeraha, ni wakati wa Watanzania kufikiria upya tulikotoka na tunakokwenda. Je, tunamshindaje adui umasikini na ujinga?

Matukio ya kuanguka kwa malori ya mafuta yameshatokea sana, lakini hatujifunzi. Fikiria ajali ile ya mwaka 2002 mkoani Mbeya. Watu walikufa hivyohivyo. Kwa nini matukio haya yanajirudia? Ni ujinga na umasikini.

Ujinga na umasikini umewafanya watu kukosa uadilifu kiasi cha kuwa tayari kuhatarisha maisha yao na ya wengine ili wapate japo tone la mafuta au kuiba mali za wengine.

Ni wakati wa viongozi kutueleza kama kweli kinatekeleza ahadi zao za kuboresha maisha ya wananchi. Mbona umasikini unaendelea kuwa tatizo sugu? Kila awamu inakuja na ahadi zake, zote za kupambana na ujinga, umasikini na maradhi.

Kila mara tunaambiwa uchumi unakua lakini hatuoni unakua kwenda wapi wakati wananchi wana maisha ya dhiki kiasi hiki.

Ni mara chache sana kusikia matukio kama haya yakitokea kwenye nchi zilizoendelea, pengine ni kwa sababu ya kuwa na miundombinu mizuri, lakini pia hakuna umasikini uliotopea.

Nchi nyingi za Afrika zimeendelea kuwa masikini baada ya kupata uhuru, huku wanasiasa wachache wakineemeka.

Wanachojua wao ni kupambana ili kubaki madarakani wakitumia makundi ya wagombea urais. Leo utasikia kundi hili linatukana jingine, hawa wanaitwa wasaliti kwenye chama, huku vibaraka wa mwanasiasa huyu wakifagia njia ili apewe fursa au wale wa yule wakitaka aongezewe muda wa kutawala.

Kundi lingine likiingia madarakani nalo linanyanyasa mengine, basi ndiyo siasa za Afrika. Ni wakati sasa wa viongozi kutekeleza ahadi zao ili kuwapa wananchi maisha bora.