Uandishi wetu ni aina ya ule wa Comical Ali au al-Sahhaf ?

Ninaamini mwandishi wa habari ni lazima asomee fani ya uandishi, maana kila fani inahitaji elimu.

Tatizo langu ni je, kusoma na kupata shahada kunaweza kumsaidia mwandishi kuandika ukweli na kuusimamia, kutetea haki, kulinda na kuheshimu uhai na utu wa mtu, kufanya uchambuzi na kukwepa hongo ya kupindisha habari?

Kuna mwandishi wa habari aliyepata kusema hivi: “Ukitaka kuwa mwandishi bora anayependwa, mwaminifu ‘asiyebore’ kwa maswali, fuata mfano wa Chemical (Comical) Ali, aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Irak enzi za Saddam Hussein au Mohammed Saeed (al- Sahaf) aliyekuwa waziri wa habari.

Katika nchi ambazo demokrasia inachechemea waandishi kama Comical ndio waandishi bora. Kinyume chake mwandishi anajitafutia moto kama uliomshukia Andrew Meldrum kule Zimbabwe.

Hoja yangu ni wamba haitoshi kuwa na shahada ya uandishi wa habari. Kuna kitu kingine zaidi. Unaweza kuwa na shahada ya juu kabisa katika uandishi wa habari lakini ukatenda kama Comical Ali.

Al-Sahaf alijipatia sifa nyingi wakati wa vita ya Irak kutokana na taarifa zake za uongo za ‘kushinda’ kwa majeshi ya Irak na ‘kushindwa vibaya’ kwa majeshi ya Marekani na washirika, hata wakati ilipoonekana dhahiri kuwa Irak imeelemewa.

Baada ya kutoka mafichoni Iraq iliposhindwa vibaya na kuulizwa kuhusu uongo wake, al-Sahaf alisisitiza kuwa kauli zake zilitokana na taarifa za uhakika.

Hata hivyo, alikana kuwa mmoja wa watu wa karibu na Rais Saddam, bali alikuwa anafanya kazi yake kwa kuzingatia fani yake ya uandishi wa habari na wajibu wake kama waziri wa habari.”

Alijua Rais Saddam wale wote waliokuwa wamemweka madarakani walichotaka kukisikia. Alitimiza wajibu wake.

Sampuli hii ya mwandishi wa habari ndiyo inahitajika katika nchi zenye demokrasia inayoyumbayumba au iliyokufa.

Kuna mhariri wa gazeti aliyesema hivi: “Ni kweli, haviendi hivyo, lakini mhariri hatakiwi kutenda yale tu anayoyataka. Kwa kiasi fulani yampasa kuvumilia unyonge wa watu, hasa katika mambo madogomadogo. Mbali ya yote, kitu cha maana si siasa - kwa hali zozote hasa kwa gazeti; na iwapo nataka watu wanifuate katika njia ya uhuru na maendeleo, ni lazima nisiwafukuze.

“Kama wanapata hadithi nzuri ya kufululiza yenye maadili katika mwisho wa ukurasa, basi hapo watakuwa na hamu zaidi ya kuona kuna nini mwanzo. Hiyo inajenga imani. Mhariri ni lazima awe na mchanganyiko wa unafiki na aina ya uovu.”

Akina Comical Ali, wanakuwa wamejaa unafiki na aina ya uovu. Daima wanataka watu wayaamini na kuyakubali yale ambayo wao hawayaamini. Comical Ali alijua wazi kwamba Marekani ilikuwa inaitwanga Irak, lakini alitaka watu na ulimwengu mzima uamini vinginevyo.

Hizo ndizo sifa za mwandishi Mtanzania: Ucheshi, utani, dhihaka na kubeba ujumbe mzito! Tanzania ni shwari! Na ushwari huu utaendelezwa na waandishi aina ya Comical-Ali na si vinginevyo.