Ufisadi na demokrasia, mambo yasiyokaa zizi moja

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (kulia) akizungumzaakizungumza wakati wa mjadala wa Demokrasia Yetu ulioandaliwa na taasisi ya Twaweza, uliofanyika katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam jana. Pembeni mwake kuanzia kushoto ni Kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze na Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya Siasa, John Shibuda. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Wakati tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Rais John Magufuli imekuwa ikitajwa na kutolewa mfano katika vita dhidi ya ufisadi, lakini kwa upande mwingine imekuwa ikielezwa kutetereka kwa demokrasia ambapo sababu mbalimbali zimetajwa. Shirika lisilo la kiserikali linalochambua maendeleo ya kidemokrasia duniani la Freedom House, katika ripoti yake ya hivi karibuni linaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kiwango kidogo cha demokrasia na kuiweka katika kundi moja na Venezuela na Nicaragua.

Kimtazamo, vita dhidi ya ufisadi nchini tangu Rais John Magufuli aingie madarakani miaka mitatu iliyopita inazaa matunda. Kinyume chake vilevile, maendeleo ya demokrasia nchini yanaelezwa kuteteleka siku hadi siku.

Kwa kiasi kikubwa hali hii inawaacha njiapanda wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya siasa na utawala bora nchini, wakishindwa kupata uhusiano kati ya masuala haya mawili ya ufisadi na demokrasia ambayo kwa kawaida hayakai zizi momoja.

Wakati wachambuzi wanaendelea kuumiza vichwa, shirika la kimataifa linalopima mitazamo ya wananchi kuhusu viwango vya ufisadi katika nchi mbalimbali, Transparency International (TI), linasisitiza kuwa mifumo thabiti na imara ya kidemokrasia na utawala bora huchangia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kwa nchi katika vita dhidi ya ufisadi.

Shirika hilo lenye makao makuu yake Berlin, Ujerumani linabainisha katika ripoti yake ya hivi karibuni kuwa nchi nyingi ulimwenguni zimeshuhudia maendeleo hafifu katika mapambano yao dhidi ya ufisadi.

Katika uchambuzi wake, shirika hilo linaonyesha uhusiano wa karibu baina ya ufisadi katika sekta ya umma na udhaifu wa taasisi kidemokrasia.

Kuna sababu nyingi ambazo hupelekea nchi fulani kushindwa kukabiliana kikamilifu na tatizo la ufisadi kwa mujibu wa TI.

Hizi ni pamoja na serikali kuwa katili, machafuko ya kisiasa, taasisi dhaifu na mifumo mibovu ya kisiasa. TI inatoa mfano wa nchi za Seychelles na Botswana ambazo zimeonekana kufanya vizuri, kwa Afrika, katika mapambano dhidi ya ufisadi ikihusisha mafanikio hayo na mifumo yao imara ya kidemokrasia na utawala bora.

Kama hali ni hiyo, ni kwa kiasi gani mifumo ya kidemokrasia na utawala bora ipo imara kiasi cha kutegemewa kutoa mchango katika vita dhidi ya ufisadi?

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, shirika lisilo la kiserikali linalochambua maendeleo ya kidemokrasia duniani la Freedom House inaitaja Tanzania kama moja kati ya nchi ambazo zina demokrasia ya kiwango kisichoridhisha, ikiwekwa katika kundi moja na Venezuela na Nicaragua.

Hali hiyo inatokana na kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa nchini, huku viongozi kadhaa wa upinzani wakikabiliwa na kesi mbalimbali pamoja na utungwaji wa sheria zinazoongeza udhibiti wa vyama vya siasa.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala anaamini kwamba taasisi imara za kidemokrasia na mapambano dhidi ya ufisadi ni vitu viwili visivyoweza kutenganishwa.

Kuhusu nafasi ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa kuimarika, Profesa Mpangala anadhani kwamba hiyo haipaswi kumshangaza yeyote, ukizingatia ukweli kwamba ni kwa kutoa ahadi hiyo, ndiyo maana Rais Magufuli alichaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano ya taifa hili.

“Kiuhalisia, vita dhidi ya ufisadi lazima iende sambamba na mchakato wa kupanua demokrasia katika nchi husika,” anasema.

Profesa Mpangala anashawishika kwamba ufisadi hukithiri katika mazingira yanayotawaliwa na woga, usiri na ukimya.

“Mabadiliko ya kweli hutokea kufuatia shinikizo la wananchi walio na uelewa wa masuala mbalimbali ambao wanaweza kufanya maamuzi sahihi katika masuala ambayo huathiri maisha yao ya kila siku.

“Sasa hii haiwezekani katika mazingira ambapo mikutano ya kisiasa imepigwa marufuku au taasisi huru ambazo husimamia uwajibikaji serikalini zinatishwa,” anaonya msomi huyo ambaye anafikiri pia kama vyombo vya habari haviko huru kufichua matendo ya kifisadi ni dhahiri kwamba mtazamo wa wananchi utakuwa ni ule wa kutoona uwepo wa ufisadi serikalini.

Mbali na mtazamo wa msomi huyo, mhadhiri mwingine wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Luisulie anadhani kwamba, licha ya taasisi imara za kidemokrasia kuwa muhimu katika mapambano dhidi ya ufisadi, hiyo pekee haitoshi kukabiliana na adui huyo.

Anasema utayari wa kisiasa miongoni mwa waliokabidhiwa dhima ya uongozi, hususani Rais, ni muhimu katika kufanikisha vita hiyo.

Dk Luisulie anatoa mfano wa nchi jirani ya Kenya ambayo taasisi zake za uwajibikaji ziko huru na imara zaidi kuliko zile za Tanzania, lakini bado nchi hiyo inaburuza mkia katika mapambano yake dhidi ya ufisadi.

“Hata vyombo vyake vya habari ni huru zaidi kuliko vyetu na hufichua kashfa baada ya kashfa. Lakini hakuna kinachotokea. Sidharau mchango wa vyombo vya habari, ninachotaka kusema ni kwamba peke yake havihakikishi uwepo wa taifa lisilo la kifisadi, hususani katika mazingira ambapo hakuna utashi wa kisiasa wa kufanikisha lengo hilo,” anasema Dk Luisulie.

Akiamini kwamba ufisadi kwa sasa nchini uko chini ukilinganisha na ulivyokuwa hapo awali, , Dk Luisulie anampongeza Rais Magufuli kwa utashi wake wa kupambana na ufisadi uliokuwa umeota mizizi katika taasisi mbalimbali za umma na za binafsi.

“Nina imani kwamba kwa utayari huu wa kuchukua hatua ambao Rais Magufuli ameendelea kuuonyesha, ushindi wa kutokomeza ufisadi hauko mbali sana,” alisema.

Ni matamko kama haya ambayo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole anadhani hukiongezea chama hicho na serikali yake ari ya kufanya mambo mazuri zaidi.

Kufuatia uchapishwaji wa ripoti ya Transparency International iliyoonyesha kupanda kwa nafasi ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ufisadi, Polepole aliandika katika mtandao wa Twitter: “Tumedhamiria kuwatumikia Watanzania kwa heshima na uthubutu wa hali ya juu huku tukihakikishia tunatokeza tatizo la ufisadi nchini.”