Wazee wetu waandike vitabu vyao mapema

President John Magufuli reads his former counterpart Benjamin Mkapa’s book after the launched it in Dar es Salaam yesterday.  From second left are, Jakaya Kikwete, Ali Hassan Mwinyi and Left is Mkapa. PHOTO|ERICKY BONIPHACE

Majuzi, Mzee Benjamin Mkapa alizindua kitabu chake kilichopewa jina la “Maisha yangu, Malengo yangu” kama fasiri yangu isiyo rasmi ya “My Life, My Purpose; A Tanzanian President Remembers”.

Kwa ambao wamekisoma kitabu hiki hata ukurasa mmoja tu, watakubaliana nami kuwa lugha iliyotumika ni nyepesi mno kuliko lugha iliyotumika kwenye kitabu cha Mzee Reginald kinachojulikana kama “I can, I must, I will” kiulinganifu.

Hoja yangu leo si ugumu wa lugha wala urahisi wa lugha wa vitabu, hoja yangu pia si kuhusu maudhui ya kitabu hiki mujarabu, hoja yangu ni kuhusu umuhimu wa watu wote wenye historia kubwa na muhimu kwenye nchi yetu kuandika vitabu vyao, kinyume chake ni kuwa, wengi wao huondoka duniani bila kuacha maandishi kuhusu mambo yao mbalimbali ambayo yanaweza kuwa mafunzo kwa kizazi kinachofuata baada yao.

Ninatambua kuwa Kikwete anaandika kitabu chake, pia najua kuwa Mzee Mwinyi yumo mbioni, tunatambua kuwa Mwalimu Julius Nyerere aliandika vitabu na kuacha maandishi na miongozo mingi. Yote haya hayana maana kuwa wazee wetu wanaandika sana, la hasha!

Ukifanya uchunguzi utagundua wazee wanaoandika sana ni walioshika wadhifa wa urais peke yao, wengi ambao hawakuwahi kuwa marais hawaandiki.

Wako wengi sana

Mtu kama Kingunge Ngombale-Mwiru, jina kubwa maarufu lakini alifariki dunia bila kuandika kitabu chake Mzee Kawawa vilevile hakuandika kitabu chake na wazee wengine kibao pia hawajaandika vitabu.

Kizazi cha wanawake kinapaswa kupewa haki yake kwa mfano, hadi leo mtaani hakuna kitabu kilichoandikwa na Mama Getrude Mongella.

Mtu kama Bakhressa alipaswa awe ametupatia vitabu kadhaa vya uzoefu wake mtaani, tajiri kama Mo alipaswa awe ameandika kitabu cha kwanza cha kuwaonyesha vijana wa Kitanzania kuwa na wao wanaweza kuwa Mo siku moja.

Tunao viongozi wengi wa kijamii, kiutamaduni, machifu na wazee wenye historia kubwa na hawajaandika vitabu.

Tunao majenerali wa jeshi na makamanda wa kijeshi wenye historia kubwa za kuipigania nchi na taifa letu lakini hawajawahi kuandika kitu chochote.

Hii yote ina maana kuwa tutatengeneza jamii yenye ombwe ambayo itakosa urithi wa historia kubwa za viongozi wa kizazi kilichopita, kilichopo na kijacho.

Historia hiyo ikibaki kwenye masimulizi ya abunuwasi na yasiyo na ushahidi wowote ule.

Mzee Kingunge

Mzee huyu kama nilivyosema alijijengea historia kubwa na ya mfano wa kipekee. Nakumbuka nikiwa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kama waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi, kuna wakati kulitokea shida kati ya wanachuo na menejimenti ya chuo. Wanafunzi wakawa na msimamo kuwa hawamtaki waziri au mtu yeyote kutoka wizara ya elimu kuja kusuluhisha na hawakutueleza wanamtaka nani, tukawa kwenye wakati mgumu sana.

Wakati huo Mwita Waitara, Naibu Waziri wa Tamisemi sasa akiwa ni Katibu wa UVCCM. akanipigia simu na kunieleza kuhusu mgogoro uliokuwapo chuoni, akanishawishi kuwa Mzee Kingunge ana uzoefu wa kipekee katika kutatua matatizo kama hayo na kunitaka twende tukazungumze naye.

Tulifunga safari hadi nyumbani kwake. Mzee akatokea chumbani, alipofika alishajulishwa majina yangu au alikuwa ananifuatilia, akaniita majina yangu yote, akanikumbusha mambo kadhaa aliyowahi kuona nikiyazungumza kwenye televisheni kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu.

Muda wote huo ananikumbushia tumesimama amenishika mkono, baadaye akaniambia keti kwenye kiti.

Palepale akanitaka nianze kumwelezea kiini cha mgogoro wa wanafunzi na menejimenti, akanisikiliza, nilipomaliza akanyanyua simu, akampigia mkurugenzi mmoja wa wizara ya elimu akamtaka aje nyumbani kwake.

Dakika 20 hazikupita akaingia mzee mmoja mrefu mweusi, sikulijua jina lake hadi leo, akampa maelekezo mahsusi ya kwenda kukutana na menejimenti ya chuo siku iliyofuata.

Palepale akanyanyua simu na kumpigia makamu mkuu wa chuo, akamshauri kitu, palepale akampigia mkurugenzi wa bodi ya mikopo na kumshauri kitu, alipomaliza akaniambia mwanangu rejea chuoni, asubuhi utapigiwa simu.

Kulipokucha nikapigiwa simu na namba ya ofisini ikinitaka nielekee utawala, nikawachukua wenzangu hadi utawala, tulipofika tukamkuta makamu mkuu wa chuo akatueleza kuwa matatizo ya mafunzo kwa vitendo katika baadhi ya vitivo yameisha na wanafunzi watakwenda wiki 8 badala ya 6 na kwamba menejimenti inaiacha bodi ya mikopo iwape wanafunzi fedha za miezi minane, mgogoro ukaisha na huyo ndiye Mzee Kingunge.

Huwa natafakari kuwa mzee wa namna hii tulimweka mchangani na hakutuachia kitabu cha historia yake kubwa.

Kama taifa tungelijiwekea utaratibu mzuri na kuanzisha kitengo maalumu kidogo cha kiserikali, ambacho kinaweza kuwa na watu 10 peke yake ambao mwaka hadi mwaka wanaweza kufanya kazi ya kuwafuatilia Watanzania mashuhuri katika kada mbalimbali na kuanza kurekodi historia zao, mikasa waliyopitia, mikwamo waliyowahi kukutana nayo, mifano mizuri waliyowahi kukumbana nayo na mmengine mengi.

Kitengo hiki kingekuwapo kingeliweza kutuibulia vitabu kabambe vya wazee kama kina Kingunge hata kama wangelikuwa wameshafariki, walau tungekuwa na sehemu ya kuanzia kufuatilia mambo makubwa yaliyowahi kufanywa na viongozi wetu na watu mashuhuri.

Tuzungumzavyo leo tunao mawaziri wakuu wengi wastaafu – kina Mzee Pinda, Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Cleopa Msuya, Joseph Warioba, John Malecela, Salim Ahmed Salim; wazee wote hawa hawajawahi kutuandikia vitabu hadi leo, kama vipo havijulikani.

Tunao magwiji wa siasa wa muda mrefu kama kina Stephen Wassira, William Lukuvi na wengine wengi na hawajawahi kutuandikia vitabu na wala hatuna utaratibu na kitengo cha kufuatilia na kurekodi historia za watu wa aina hiyo. Tusipoweka utaratibu, tutaendelea kukikosesha kizazi kijacho historia kubwa na muhimu sana kuhusu nchi.

Julius Mtatiro ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru. Simu; +255787536759.