KAKAKUONA: Bado tu malalamiko, wateule msaidieni Rais wetu

Nimefuatilia ziara za Rais John Magufuli na pengine ziara ya karibuni kabisa ya mkoa wa Mbeya, nimeona anakutana na kero ambazo zilipaswa kutatuliwa na wakuu wa mikoa au wilaya.

Mabango anayoonyeshwa Rais na kuyasoma kisha kutafuta ufumbuzi wa papo kwa hapo ni ishara kwamba viongozi anaowateua wamsaidie, ama hawamsaidii au hawana uwezo wa kumsaidia kwa sababu suala hili linajirudia mara kwa mara.

Rais anaelezwa suala la mama ambaye mtoto wake alibakwa, lakini Kamanda wa polisi wa mkoa yupo, mkuu wa wilaya yupo, mkuu wa mkoa yupo na bado tutamlaumu akiteua na kutumbua?

Ipo migogoro ya ardhi ambayo haihitaji hadi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi asafiri kilometa kwa kilometa kuitatua, au mpaka Rais afike ndio ipatiwe ufumbuzi.

Kunyanyuliwa kwa mabango katika ziara za Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri mkuu, Kassim Majaliwa ni kipimo tosha kuwa viongozi wa maeneo hayo hawatoshi.

Rais alipaswa aachwe ashughulikie mambo ya kitaifa, lakini leo analazimika hata kushughulikia mambo madogomadogo ambayo yangefanywa na wateule wake.

Ni kweli iko migogoro mizito hasa ya ardhi inayogonganisha taasisi mbili ama moja za Serikali ambayo inahitaji maamuzi magumu ya Rais, lakini si migogoro ya mtu kudhulumiwa ardhi yake.

Hivi kweli mawaziri Ma-RC, Ma-DC na wakurugenzi wa wilaya wanajisikiaje wanapoona mabango na kero ndogondogo ambazo wakati mwingine Rais alishazitolea maelekezo?

Mathalan, Rais ameshasema mjasiriamali ambaye mapato yake hayazidi Sh4 milioni asitozwe ushuru, na akawapa hadi vitambulisho vya mjasiriamali, bado halmashauri inaenda kumtoza ushuru.

Wakati mwingine huwa watendaji wanapenda kushika sharubu za simba, wenyewe halafu wakishukiwa kama mwewe wanaona kama wanaonewa. Kila mmoja atimize wajibu wake pale alipo.

Rais tumuache ashughulike na mambo makubwa kama diplomasia ya uchumi ili kuvutia wawekezaji wakubwa kutoka nje kuja kuwekeza nchini na kujenga mahusiano mazuri na mataifa mengine.

Tunamchosha Rais na kero ndogo ndogo ambazo zipo ndani ya uwezo wa mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya na hata wakurugenzi na ndio maana katika mikutano naye anageuka mlalamikaji.

Binafsi wapo wakuu wa mikoa wa chache ambao naweza kusema wana ujasiri wa kufanya maamuzi nao ni wa Dar es Salaam, Paul Makonda; Kilimanjaro, Anna Mghwira na Iringa, Ally Hapi.

Pale kwenye haki wanasema hapa kuna haki na pale ambapo wananchi wanaumizwa kutokana na udhaifu wa watendaji wenyewe wa Serikali watafanya maamuzi magumu. Huo ndio uongozi.

Kiongozi ni lazima awe na uthubutu wa kutenda na hata kama ni kusahihishwa lakini ametenda na kutoa uamuzi wa haki, lakini tukimuachia Rais kila kitu afanye yeye, tutamzeesha kabla ya siku zake.