Kenya kuanzisha somo la demokrasia na uchaguzi kwa shule za msingi

Mkurugenzi wa IEBC anayehusika na Elimu kuhusu Uchaguzi, Ushirikiano na Mawasiliano Immaculate Kassait

Mombasa. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeanzisha mikakati ya kutaka kuingizwa kwa somo la demokrasia na uchaguzi katika shule za msingi ili kuzima ukabila na machafuko yanayoweza kusababishwa na michakato ya uchaguzi siku zijazo.

Akizungumza katika Chuo cha Serikali cha mafunzo ya ushuru kwenye kongamano la walimu wakuu mjini Mombasa, Mkurugenzi wa IEBC anayehusika na Elimu kuhusu Uchaguzi, Ushirikiano na Mawasiliano, Immaculate Kassait amesema somo hilo litawapa wanafunzi mwanga kuhusu uongozi bora.

“Tumekuwa tukishuhudia machafuko wakati wa uchaguzi katika nchi yetu. Somo hili litawaelimisha watoto kuhusu umuhimu wa demokrasia na uongozi bora katika taifa,” ameeleza Kassait.

Amesema kuwa somo hilo litawafunza wanafunzi wa shule za msingi kuhusu hatua muhimu na namna ya kupiga kura, umuhimu wa kupiga kura na umuhimu wa kuchagua kiongozi kutokana na ubora wake na si kwa misingi ya kikabila.

“Tunataka kukuza jamii ambayo itakuwa inafikiria katika misingi ya ubora wa kitaifa na sio tu jamii yao au jimbo la ubunge wanalotoka,” amesema mkurugenzi huyo.

Kiongozi mwingine wa IEBC, Lawrence Baraza amesema bado wanajadiliana na Wizara ya Elimu kuhusu vipi somo hilo litaingizwa katika mfumo mpya unaojikita katika uadilifu.

“Tutajadiliana kujua iwapo litakuwa ni somo au mada katika mojawapo ya masomo wanayofunzwa,” ameeleza Baraza.

Ameeleza kuwa somo hilo litafunza sehemu ya demokrasia na elimu kuhusu uchaguzi na kupiga kura.

Kwa sasa tume hiyo inasimamia uchaguzi unaoendeshwa katika baadhi ya shule za msingi kuchagua viongozi.

“Tunatembelea shule za msingi kuona jinsi wanavyoshawishi wenzao kuwachangua na tunawaongoza namna wanavyopaswa kutekeleza uchaguzi huo,” ameeleza Baraza.

Walichagua shule za msingi kuhamasisha wanafunzi kwa sababu wao ndio viongozi wa kesho.

Mradi huo unadhaminiwa na serikali ya Canada, Wizara ya Elimu na Taasisi ya Kukuza Mitaala Nchini (KICD).