Kilichomponza Lissu ni utambulisho wake

Kuna hadithi si maarufu sana ya paka na ng’ombe, waliokuwa wakifugwa na mmiliki mmoja. Ilifika wakati ng’ombe akashikwa wa wivu kupita kiasi.

Wivu wake ulitokana na kumuona mchungaji wake akimbeba paka, akimlaza ndani yeye analazwa nje, paka anachanwa manyoya na wakati mwingine hulala na mmiliki kwenye kochi.

Siku moja mchungaji alipotoka, ng’ombe akaingia ndani akaenda kujilaza sebuleni. Aliamini kufanya hivyo kusingeleta tatizo, kwani paka naye analala. Kiufupi alijiweka daraja moja na paka.

Matarajio yake yakaenda patupu baada ya mmiliki kuja na kumkuta sebuleni. Ng’ombe alitolewa sebuleni kwa fimbo na siku ya pili akapelekwa machinjioni.

Kimsingi kilichomponza ng’ombe ni ule utambulisho wake, yeye ni ng’ombe na mwenzake ni paka. Licha ya kuwa wote ni wanyama ila hawafanani katika huo utambulisho.

Katika siasa zetu za Tanzania kuna mtu anateseka kwa sababu ya utambulisho wake. Ni mwanasiasa, ila ana utambulisho zaidi ya huo ambao unamfanya akutane na vigingi vingi mno.

Ni Tundu Lissu, aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema.

Hadithi yake imeanza mbali sana. Binafsi nitaianza siku ya pili tangu kushambuliwa kwa risasi katika jaribio la kumuua Septemba 7, 2017, kule Dodoma.

Pale Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alipozungumza na vyombo vya habari nje ya Bunge, alisema:

“Niwahakikishie Watanzania hasa wapiga kura wake kwamba mgonjwa (Lissu) yuko katika mikono salama na Bunge tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunamsaidia mwenzetu aweze kupona.”

Bahati mbaya hadi inafika Januari 2018, Lissu alipohojiwa na chombo kimoja cha habari alisema: “Bunge na Serikali walitoa kauli ya kugharamia matibabu lakini hadi sasa hawajatoa hata senti moja ya matibabu”.

Hadithi ni ndefu tuifupishe; kwa mujibu wa Lissu si Bunge wala Serikali waliochangia matibabu yake hadi sasa, zaidi ya kumpa pesa ambazo ni stahiki yake kama wapewavyo wabunge wengine.

Pia anasema matibabu yake yametokana na michango kutoka kwa Watanzania na watu binafsi wanaojiweza.

Lissu kuwa mwanasiasa sio utambulisho pekee, upo utambulisho zaidi ya huo, ambao ni “mwanasiasa wa upinzani”. Na huo hasa ndiyo utambulisho unaomponza.

Nikisema anaponzwa na utambulisho wake sina maana ni kosa lake. Isipokuwa ni kosa la wale wanaoutazama utambulisho wa Lissu na kuuona ni tishio hadi kujikwamisha kutoa msaada kwa afya na uhai wake.

Naamini kama Lissu angekuwa ni mwanasiasa kutoka chama tawala, tusingeona ahadi hewa na vigingi vya kukwamisha matibabu yake.

Anaanzaje kwanza kukwamisha kumhudumia mwanasiasa wa utawala. Uthubutu huo haupo, maana mhusika angeundiwa vikao na pengine hata kupewa adhabu.

Siasa chafu huwasukuma wanasiasa kufanya mambo kwa itikadi na utambulisho wa mtu. Inasikitisha zaidi mambo hayo yakifanyika hadi linapohusika suala la uhai wa mtu.

Hilo ni moja. La pili, linahusu uamuzi wa Lissu kuvuliwa ubunge. Ni baada ya siku chache kutangaza yuko njiani kurudi nyumbani.

Wapo wanaoamini upo uhusiano wa tangazo lake na maamuzi ya Spika. Wala si dhambi kuamini hivyo.

Wakati Ndugai anamvua Lissu ubunge alitoa sababu mbili. Moja ambayo nitainukuu; “Spika kutokuwa na taarifa ya kimaandishi au vinginevyo ya alipo Lissu”.

Hiyo ni moja ya sababu. Ila kwa upande mwingine yapo maelezo mengi yanayoonyesha Spika alijua Lissu anapelekwa nje ya nchi.

Bado mjadala uko palepale, ikiwa sababu alizozitoa Spika ni za haki au za kisiasa juu ya ubunge wa Lissu.

Ila mjadala huo hautofuta ukweli kwamba kuwa watu hawakuwa na nia ya dhati ya kusimama na Lissu katika matibabu yake, hadi anapochukua uamuzi wa kukipiga teke kiti chake cha ubunge. Na huo ndio ukweli usiohitaji mjadala.

Haya yanaturudisha katika hadithi yangu ya paka na ng’ombe, wote ni wanyama lakini tatizo utambulisho.