UCHAMBUZI: Mazombi walishindikana, wasiojulikana watawezekana?

Unaowaona wamefunika nyuso, wamebeba silaha za moto na za jadi ndani ya gari zinazofahamika.

Magari mawili yanapita kwa wakati mmoja yakiwa na watu waliojihami kwa silaha na kuficha nyuso. Jioni ya siku hiyo, katika mji wa Unguja zinaenea taarifa za watu kuvamiwa na kupigwa na mazombi.

Wazanzibari wanawatuhumu mazombi kuwa ni watu wanaotembea wakiwa wameficha nyuso, wakiwa na silaha za jadi na moto, pia wakiwa katika magari ya vikosi vya Serikali.

Siku na tarehe hiyohiyo, maoni ya mhariri katika gazeti hili yanahoji: “Mazombi ni nani, kwa nini wanatamba Zanzibar?” Mhariri akaendelea kuandika; “kuonyesha kwamba kundi hilo (mazombi) ni hatari, wakati wa uandikishaji wa BVR mwaka jana (2015), watu wawili waliuawa kwa risasi na wengine kujeruhiwa na kundi hilo”.

Vitendo hivi viovu vya mazombi vilianza wakati wa uandikishaji wapigakura katikati ya 2015 hadi siku kadhaa baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016.

Cha ajabu Jeshi la Polisi kupitia kamishna wa wake Zanzibar wakati ule, Hamdan Omar aliviambia vyombo vya habari kwamba polisi hawana taarifa juu ya mazombi.

Vyama vya siasa vya upinzani vilikuwa vikilalamika uwepo wa mazombi, wananchi wakalalamika, waathirika wakahojiwa na vyombo vya habari na vikaripoti. Picha pamoja na video za wanaotuhumiwa kuwa mazombi zikanaswa. Ila Polisi haikuwahi kumkamata mtuhumiwa wala kueleza chunguzi uchunguzi kama upo umefikia wapi. Wanasema hawajui chochote.

Makundi mfano wa mazombi yalikuwapo Zanzibar kati ya ya mwaka 1995 na 2000 na wananchi wakayapa jina la melodi. Kisha kati ya 2001 na 2005 yakapewa jina la janjawidi. Mara nyingi huzuka wakati wa joto la uchaguzi.

Matendo wanayoyafanya ni yaleyale ya kuvamia watu na kuwapiga. Isipokuwa tu Wazanzibari huwa wanayabadilisha majina yao.

Tusonge mbele sasa. Tanzania yetu ya sasa ina tatizo sugu la ama kutoweka au kutekwa kwa watu yanayofanywa na watu wasiojulikana. Baadhi ya wanaotekwa hurudi wakiwa wazima na wengine wamesubiriwa hadi wa leo hawajachomoza.

Mdude Nyagali maarufu Mdude Chadema, ni muhanga wa hivi karibuni kabisa kuingia katika mikono ya wasiojuulikana. Tushukuru Mungu kwamba kaachiwa akiwa mzima, ingawa katika maumivu makali ya kipigo na mateso.

Mdude si wa kwanza, na huenda hatakuwa wa mwisho. Orodha ya wanaotekwa inazidi kukua, bahati mbaya Jeshi la Polisi halijawahi kumkamata hata mtuhumiwa mmoja wa utekaji, wala haina jawabu ya maswali yanayoulizwa.

Maswali yenyewe ni nani yuko nyuma ya matukio haya? Yuko wapi Ben Saanane na Azory Gwanda? Polisi haijatoa majawabu. Nani aliwateka Msanii Roma na Mo Dewji? Nani walitaka kumuua Tundu Lissu? Taasisi nzima ya polisi kimyaa, majibu ya maswali hayo hayajatolewa.

Tofauti kubwa kati ya watu wasiojulikana na mazombi wa Zanzibar ni moja. Hawa mazombi wala hawaogopi kitu. Walikuwa wanapita mchana kweupe, wakiwa na silaha na magari yao. Na Wazanzibari wakawaona na hata kuwapiga picha.

Wasiojulikana hujificha na hufanya matukio yao kwa uangalifu sana. Cha ajabu hata wale mazombi wasiojificha hakuna hata mmoja amewahi kukamatwa. Hakuna uchunguzi ulioelezwa kufanyika wala matokeo yake. Hakuna taarifa rasmi hasa wale ni akina nani.

Hapa ndio kunazuka swali gumu sana; ikiwa mazombi wasiojificha walishindikana kukamatwa na kuchukuliwa hatua, Je, hawa watu wasiojulikana wanaojificha watawezekana?

Huku ndio kusema Jeshi la Polisi limeshindwa kuonyesha uwezo wake katika kuwakamata hawa watu? Limeshindwa kuja na majibu kuhusu kesi za kutatanisha zinazotokea? Mazombi na wasiojulikana wamekuwa na nguvu na ujanja zaidi hata kushinda taasisi nzima ya polisi? Au polisi wanajua kinachoendelea?

Watanzania nao wanataka kujua kinachoendelea. Hadi wale waliokuwa wakificha sura na kutumia magari ya vyombo vya serikali, silaha za moto, tulipaswa kuelezwa ni akina nani na wanafanya vile kwa dhumuni lipi.

Kimya cha polisi katika kesi hizi, hakitoi tafsiri nzuri. Ndiyo kushindwa? Kama wameshindwa kuja na jawabu, kwa nini wakitakiwa waombe msaada wa nje hukataa na kuwa wakali?