Msuguano wa Dk Kigwangala, Makamba nani amepotea njia?

Ukishakuwa mwanasiasa maarufu basi ni vema kufahamu kuwa kile unachokiandika kwenye mitandao ya kijamii kinaweza kukujenga au kukubomoa.

Mabishano kati ya mawaziri wawili, January Makamba na Dk Hamis Kigwangala kwenye mtandao wa Twitter hivi karibuni umetupa nafasi ya kuangalia mchango wa wafuasi wa wanasiasa na busara za viongozi tunaowachagua.

Kilichotokea

Mwandishi wa blogu kwa jina la Haki Ngowi alichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhusu nia ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha mradi wa magari ya kupandisha watalii Mlima Kilimanjaro kupitia kwenye nyaya (cable cars). Baadaye Waziri January Makamba alimjibu Haki Ngowi kuwa hata kama hilo wazo la kuwa na mradi kama huo linaonekana kuwa zuri lakini bado ipo haja ya tathmini ya mazingira kufanyika kabla ya kuanza kuutekeleza.

Ndipo waziri mwenzake wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangala alipoibuka na kumjibu January Makamba kuwa masuala ya tathmini za mazingira yanachelewesha maendeleo na yeye kama waziri analenga zaidi kuongeza mapato kupitia utalii. Akaenda mbali zaidi na kumshutumu mwenzake kuwa watu wa mazingira wanapenda sana makongamano. Kigwangala aliendelea kurusha mashambulizi ambayo hayawezi kuelezwa yote katika makala haya.

Baadaye Waziri Makamba akaona isiwe taabu, akaomba kutoendelea na malumbano na waziri mwenzake ambaye kwa hakika ameonyesha dhamira ya kuchapa kazi katika wizara yake na kuleta maendeleo. Hata hivyo, kauli ya Makamba haikumnyamazisha Kigwangala, aliendelea kumshambulia mwenzake. Hali hiyo iliwaibua mashabiki wa Makamba na kumshambulia Kigwangala kwa kumwita ni kiongozi aliyekosa busara.

Baadaye tulisoma katika mtandao wa kijamii wa chombo moja cha habari kuwa Kigwangala alimwomba radhi Makamba na kusema kuwa alighafirika na kumsihi wasameheane waendelee kuchapa kazi.

Magufuli na Mwandosya

Mabishano ya Makamba na Kigwangalla yamenikumbusha kipindi cha miaka ya mwanzoni mwa 2000 wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa. Wakati huo, John Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi na Profesa Mark Mwandosya akiwa waziri wa Uchukuzi.

Mwandosya alitaka boti za mwendokasi za Azim Dewji ziende kutoa huduma Ziwa Victoria na zisafirishwe kwa njia ya barabara kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. Magufuli alipinga wazo hilo akisisitiza kuwa labda boti zibomolewe kwanza ili zisafirishwe vipande vipande halafu zikaunganishwe tena zikifika Mwanza.

Magufuli alieleza kuwa malori yatakayobeba boti hizo yangevunja madaraja na kuharibu barabara zetu. Kukawa na mjadala kila kona kwenye vijiwe kuhusu nani alikuwa sahihi na nani hakuwa sahihi. Na kila waziri akivuta mashabiki wa kumtetea na bahati nzuri au mbaya hakukuwa na mitandao ya kijamii kwa wakati ule.

Hatimaye ikaonekana Magufuli ameshinda kwa hoja kwakuwa wakati daraja la Ruvu lilikuwa dogo lisiloweza kuhimili uzito wa malori ya kubeba zile boti. Lakini, pia pale Vigwaza pana daraja la treni lenye urefu wa mita 5.5 na ule mzigo ulikuwa unazidi mita 5.5. Baadaye boti zile zilisafirishwa kupitia Mombasa hadi Kisumu. Hata hivyo, boti zile hazikudumu sana Ziwa Victoria.

Magufuli alikuwa na mtifuano na Mwandosya, na sasa mawaziri wake wawili wameingia kwenye mgogoro baina yao kuhusu mradi wa kujenga njia ya gari za kubebea watalii kupandisha Mlima Kilimanjaro (cable cars).

Ni mtifuano kati ya Waziri wa Utalii anayepigia chapuo mradi huo kwa madai kuwa utalinufaisha taifa kwa kuongeza mapato na kuvutia makundi yote kupanda Mlima Kilimanjaro.

Upande wa pili ni Waziri wa Mazingira January Makamba aliyeshauri kuwa kabla ya kuutekeleza ni vema tathmini ya athari za kimazingira, kijamii na kiuchumi ifanyike.

Kilichofurahisha zaidi ni kuwa wote wawili walionyesha nia ya urais mwaka 2015. Kigwangala jina lilikatwa mapema lakini mwenzake Makamba alifika tano bora. Naweza kusema kisiasa, Makamba ana ushawishi zaidi na wachambuzi wengi walimpigia upatu wa kuwa Waziri Mkuu lakini bahati haikuwa upande wake, kama ambavyo mwaka 2005 wengi walimpigia chapuo Mheshimiwa Magufuli kuwa anafaa kwa cheo cha uwaziri mkuu kwenye serikali ya Jakaya Kikwete.

Wanaofuatilia siasa za Tanzania wanamlinganisha January Makamba wa awamu ya tano kuwa sawa na alivyokuwa John Magufuli enzi za Kikwete. Mashabiki wa Kikwete walimpiga vita sana Magufuli na hawakutaka kabisa arudi kwenye baraza la mawaziri lakini, hata hivyo Jakaya Kikwete alimteua kwenye Baraza la Mawaziri kwani kwa kumwacha angethibitisha zile fununu kuwa anamchukia.

Hali hii ilijitokeza pia kwa Makamba baada ya uchaguzi wa 2015. Mashabiki na wafuasi wa karibu na JPM walionyesha kutotaka Makamba awepo kwenye Serikali ya Magufuli lakini kisiasa ikaonekana haitakuwa jambo la busara kufanya hivyo.

Ikumbukwe kuwa Makamba alifanya kazi kubwa ya kuongoza kikosi cha Tehama upande wa CCM ambacho kilifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kampeni za JPM zinaenda sawa huku wakijibu mashambulizi ya kikosi kikali cha Tehama cha Ukawa (Chadema) kule Kawe.

Mradi wa cable cars kwa kifupi

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu, mwishoni mwa mwezi wa nne akiwa mkoani Kilimanjaro alieleza nia ya Serikali kuanzisha mradi wa magari hayo ya kupandisha watalii kwenye Mlima Kilimanjaro. Alieleza kuwa hayatafika kileleni lakini yataishia kwenye uwanda wa Shira. Kwa mujibu wa gazeti la The East African la tarehe 4 Mei, mradi huo ungejengwa katika njia ya Machame na ungefanywa na kampuni ya kimarekani iitwayo Avan Kilimanjaro. Gazeti hilo linaenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa wazo hilo siyo geni kwani lilitolewa mwaka 1968 na kampuni ya Kifaransa lakini serikali ya wakati huo iliona hakukuwa na sababu za kuwa na mradi kama huo.

Nani alikuwa sahihi?

Naomba nijipe jukumu la kuwa refarii huru wa mchuano huu. Kimsingi Kigwangala hakupaswa kumshambulia kwa maneno makali mwenzake kwa sababu kwanza Makamba alikuwa anamjibu Haki Ngowi na si waziri mwenzake. Pili, Kigwangala alitakiwa akumbuke kuwa Sheria ya Utalii ya Mwaka 2008 itakuwa imekiukwa.

Kwanza kabisa kitendo cha kuipa kampuni ya kimarekani ya Avan Kilimanjaro kuendesha mradi huo ni cha kukiuka Kifungu cha 58 (1) na (2) cha Sheria ya Utalii ya Mwaka 2008 kinachoelekeza kuwa shughuli za kuendesha utalii nchini lazima zifanywe na kampuni za ndani na za watanzania.

Pili, suala la tathmini ya athari za mazingira, utamaduni na kijamii limeelekezwa katika kifungu cha 11(4) cha Sheria ya Utalii ya Mwaka 2008. Kifungu hicho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Utalii kusajili kampuni za utalii baada ya kampuni hizo kukidhi masharti ya tathmini za mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.

Kwa kuangalia vifungu hivyo vya sheria utagundua kuwa Makamba alikuwa sahihi kushauri kuwa ni mapema kutangaza kuwa mradi utafanyika wakati bado mchakato wa tathmini ya kimazingira haijafanyika. Inasemekana kuwa mradi huo utahusisha ukataji mkubwa wa miti pamoja na uharibifu wa uoto kwenye safu za Mlima Kilimanjaro.

Kigwangala ni mwepesi wa kuomba radhi akiona mambo yamemkalia vibaya, lakini kisiasa hiyo inaonyesha kuwa ni kiongozi asiyetafakari vizuri maamuzi yake kama hajaongea.

Ni vema watu wakafahamu kuwa Makamba ana mtaji mkubwa kisiasa kuliko Kigwangala. Isitoshe walianza uwaziri kwa hatua tofauti kabisa. Kigwangala alianza kwa mguu mbaya wa kufanya maamuzi mengi ya kukurupuka alipokuwa Naibu Waziri Wizara ya Afya, ili hali mwenzake Makamba alianza kuonyesha kuwa maamuzi yake yaligusa hisia za wananchi alipoingilia kati suala la ubomoaji Jangwani na mafuriko ya mara kwa mara bonde la Msimbazi.

Ni jambo la busara kwa viongozi wetu kuchutama na kukubali yaishe mapema kabla ya kukuza jambo. Ukiendelea kukomaa na hoja ambayo mwenzio kakubali yaishe utaumbuka na kuonekana huna busara.

(Faraja Kristomus ni Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kwa 0787525396)